TUHUMA ZIMEISAIDIA TAIFA STARS
Basi Taifa Stars ikapambana na Benin inayoshika nafasi ya 78 katika viwango vya FIFA huku Tanzania ikihangaika katika nafasi 115. Wakati Tanzania ikimkosa Mwana Samatta ambaye ni mmoja kati ya wachezaji wake tegemeo wanne wanaocheza soka la kulipwa nchi ya nchi, Benin nao walikua wakimkosa nyota wao Razak Omotoyossi. Lakini walikua na nyota wao wengi tu wanaocheza soka nje ya Benin wakiwemo Abdel Fadel Suanon anaekipiga huko Sportive Club Du Sahel ya Tunisia pamoja nae Steve Mounie kutoka Montpellier ya Ufaransa. Wakiwa chini ya unahodha wa Stephane Sessegnon, mwanandinga tegemeo sana katika klabu ya West Bromwich Albion ya Uingereza.
Nilikua nawatazama wachezaji wetu wa Tanzania, wiki chache zilizopita kulizuka tuhuma dhidi yao kwamba wanaihujumu timu. Kuihujumu timu ya taifa ni sawa na kulihujumu taifa lenyewe. Hebu jaribu kuvaa viatu vya mtu anayetuhumiwa kuwasaliti watanzania wenzake zaidi ya milioni 45, unajisikiaje? Tuhuma hizo hazikuthibitishwa na wala aliyezitoa hakuwajibika kwa kutoa tuhuma za uongo. Nilizitazama sura za wachezaji wengi wa Taifa Stars nikagundua zina kitu rohoni. Roho zao zilikuwa na kitu ambacho nilikitegemea kabisa na ndicho kilichowafanya wajitume zaidi na kushinda kwa mabao 4-1.
Ndugu zangu, sisi watanzania ni wazalendo. Mwalimu Nyerere alitufundisha kujivunia utaifa wetu. Tuhuma za kulihujumu taifa hili zinauma zaidi ya kaa la moto kupita kooni hata kama si za kweli.
Lakini hata kama ni kweli, ni lazima moyo wako upate joto kwa tuhuma za aina hiyo. Wachezaji wetu walicheza mchezo huo huku wakiwa na hisia mbaya zinazotokana na kushindwa kukonga nyoyo za Watanzania katika siku za karibuni huku taifa likiwa limewapa kila kitu wanachostahili kupewa. Kama unashindwa kulitumikia taifa lako kwa moyo, akili, nguvu na uwezo wako wote ikiwa wewe ndiye uliyeaminiwa kwa ajili ya kuliwakilisha na huku ukiwa umepewa rasilimali zote ni sawa na kulihujumu tu.
Sura za wachezaji wa Tafa Stars zilikua zinaonesha hilo, walikubali kuibeba hatia na wakajituma ili kuijibu kwa vitendo. Unamtazama nahodha Nadir Haroub akifunga bao dakika ya 14, kwa furaha anataka kuvua fulana yake, lakini mlinzi mwenzake, Agrey Morris anamsihi asifanye hivyo kwa sababu angepata kadi na kuligharimu taifa. Sote tunajua kwamba ule ni haukua mchezo wa mashindano, lakini umekua na faida kubwa sana kwetu. Umetudhihirishia kwamba uwezo tunao japo si mkubwa sana. Tunaweza kushindana na wenzetu na tukapata matokeo mazuri. Mchezo umemdhihirishia mwalimu kwamba wachezaji wake wana uwezo japo wengine wamekuwa hawapati nafasi katika vilabu vyao.
Anachohitaji kukifanya Mart Nooij ni kuwafanya wampe 100% ya uwezo wao ndani ya uwanja. Anahitaji kumfanya Mwinyi Kazimoto ajue ni kwa nini anakatiwa tiketi ya ndege ili atoke Doha, Quatar wakati Hassan Dilunga yupo hapa. Amfanye Haroun Chanongo aitumie vema fursa adimu ya kucheza na Thomas Ulimwengu katika kikosi kimoja. Awafanye wachezaji watambue jukumu lao kwa taifa, watambue umuhimu wa ile jezi na bendera wanayoipeperusha.
Tutapata matokeo tu. Kama kila mchezaji atacheza akiwa na sura kama ya Amri Kiemba, hasira
kama ya Mwinyi Kazimoto na nguvu kama ya Thomas Ulimwengu katika mchezo huo wa Oktoba 12, halitakua jambo adimu kuwafunga watu magoli manne nyumbani. Kama nyavu za akina Sessegnon zinacheza mara nne katika mchezo wa kirafiki, tunashindwaje kuzitikisa za akina Andy Mwesigwa walau mara mbili katika mchezo wa mashindano? Au ni mpaka kuwa na tuhuma?
Facebook: Richard Leonce Chardboy
Twitter: @chardboy77
Email: chardboy74@gmail.com
Simu: 0766399341
No comments