WAFAHAMU TAI WALIOVAMIA LIGI YA MABINGWA ULAYA MSIMU HUU
PFC LUDOGORETS RAZGRAD AU KIFUPI "LUDOGORETS" ni moja ya klabu iliyofanikiwa kufuzu katika hatua ya makundi ya klabu bingwa ulaya msimu huu wa 2014-2015.Wakiwa katika kundi B linalojumuisha timu kama
1)REAL MADRID 2)FC BASEL 3) LIVERPOOL pamoja na wao LUDOGORETS.
PFC LUDOGORETS NI NANI HAWA???
Hili ni swali ambalo watu wengi hasa wapenda Soka wangependa kulijua au kupata majibu yake kwa undani zaidi.
PFC LUDOGORETS ni klabu kutoka katika nchi ya BULGARIA katika mji unaoitwa RAZGRAD katika mkoa unaoitwa LODOGORIE kaskazini mashariki mwa nchi ya BULGARIA.LODOGORIE maana yake ni "Region of wild forest" yaani mji pekee unaopatikana wanyama wasiofugwa katika nchi hiyo. (Wanyama pori)
LUDOGORETS wakijulikana kwa jina lao la utani kama "The eagles" yaani "TAI",Jina hili walipewa zawadi kutoka katika mji wa LAZIO nchini Italia baada ya ushindi na pia kutokana na ndege aina ya tai wa kike aitwaye "FORTUNA" apatikanaye huko italia.
Klabu hii ilianzishwa June 18 2001 na watu wawili mashuhuri ambao ni ALEKSANDAR ALEKSANDROV na bwana VLADMIR DIMITROV kama LUDOGORIE FOOTBALL CLUB na jina hili ililipatikana kutoka katika timu iliyokuwepo hapo awali katika mji huo ambapo timu hiyo ilianzishwa mwaka 1945 na kuvunjika mwaka 2006.
PFC LUDOGORETS AU KIFUPI LUDOGORETS wakiongozwa na kocha wao aitwaye Georgi Dermendzhiev kocha mwenye falsafa nyingi za kufundisha soka la kushambulia mno kama "kundi la nyuki" ameweza kwa namna moja ama nyingine kuipa mafanikio makubwa timu hii,moja ikiwa ni kufuzu hatua ya makundi ya klabu bingwa ulaya.
Pia isitoshe tu hivyo! mafanikio makubwa waliyoyapata LUDOGORETS si kutokana na wachezaji na kocha wao tu,bali yupo mtu nyuma ya pazia ambaye si mwingine bali ni mmiliki wa klabu aitwaye KIRIL DOMUSCHIEV ambaye kwa namna moja ama nyingine amekuwa ni mhimili mkubwa wa timu akisifika kwa kumwaga mapesa kama "njugu" kusudi tu timu iweze kupiga hatua moja kwenda nyingine.
WAPI WALIPOTOKA NA YAPI MAFANIKIO YAO MAKUBWA???
Wakitumia uwanja wao wa nyumbani uitwao LUDOGORETS ARENA wenye uwezo wa kubeba watazamaji 8000 tu,yaani hata uwanja wa taifa wa Tanzania ni mkubwa mara nane yake!! wameweza kupiga hatua ndani na nje ya nchi yao.Wakipanda daraja kutoka katika mfumo wa ligi ya nchi yao ambao ni wa "MAKUNDI" waliweza kutoka chini na kufanikiwa kuingia katika Daraja la juu (KUNDI A) katika mfumo wa ligi wa nchi ya BULGARIA.
PFC LUDOGORETS ambao ni mabingwa wa bulgaria mara tatu wa Group A-Top division wa mwaka 2011-2012,2012-2013,2013-2014.
Kama hiyo haitoshi PFC LUDOGORETS waliweza kupata mafanikio makubwa mno baada ya kuchukua "TREBLE" yaani makombe 3 makubwa nchini humo kwa msimu mmoja mnamo mwaka 2011-2012,Walianza kwa kuwafunga wapinzani wao wakubwa CSKA SOFIA kwa 1-0 ugenini na kuchukua ubigwa wa ligi wa nchi yao maarufu kama Group A-Top division
Na katika mechi hiyo ambayo ndiyo ilikuwa ya kuamua nani awe bingwa wa msimu huo ikizingatiwa kuwa walikuwa nyuma kwa pointi 2 ya wapinzani wao hao na baada ya kuwafunga wakaweza kutwaa ndoo.
Na pia kombe la pili kubwa ndani ya msimu huo huo wao kutwaa lilikuwa ni mnamo may katika kombe la BULGARIAN CUP ambapo waliweza kuwafunga LOKOMOTIV PLOVIDIV kwa mabao 2-1 katika uwanja wa LAZUR STADIUM katika mji wa BURGAS.
Kombe lingine la mwisho la 3 kutwaa lilikuwa ni BULGARIAN SUPERCUP mnamo august kwa kuwafunga tena LOKOMOTIV PLOVIDIV kwa mabao 3-1 na hivyo kukamilisha ile "TREBLE" yaani makombe 3 makubwa kwa msimu mmoja.
VIPI WALIIANZA UEFA CHAMPIONS LEAGUE MPAKA KUFIKA HAPA WALIPO????
Waswahili wanasema "safari ni hatua" na ndivyo hivyo walivyoanza taratibu PFC LODOGORETS hatua moja baada ya nyingine mpaka hapa walipo,Wakiwa wamechukua "ndoo" nchini mwao msimu wa 2011-2012 wakiwania kushiriki LIGI YA MABINGWA ULAYA wakifanikiwa kupita katika hatua za mwanzo lakini siku zote waswahili wanasema "mkamia maji hayanywi" kwa bahati mbaya waliishia hatua ya play off hiyo na kuishia kutolewa na DINAMO ZAGREB ya nchini CROATIA kwa jumla ya mabao 4-3.
Lakini kama hiyo haitoshi PFC LUDOGORETS walijaribu bahati yao tena msimu wa 2012-2013 ambapo walikuwa ni mabingwa tena nchini mwao,na wakaianza safari yao ya kufuzu LIGI YA MABINGWA ULAYA kwa kuziondosha klabu kama PARTIZAN BELGRADE na SLOVAN BRATISLAVIA lakini lile "zimwi la mikosi" liliendelea kuitafuna timu hiyo baada ya kutolewa tena na FC BASEL katika hatua ya play off ya LIGI YA MABINGWA ULAYA lakini hata hivyo walifanikiwa kudondokea katika michuano ya EUROPA LEAGUE na kufanikiwa kuongoza katika kundi B wakiwa nafasi ya kwanza baada ya kuwa "unbeaten" wakishinda michezo 5 na kutoka sare mchezo 1.
Katika hatua ya 16 bora waliweza kukutana na LAZIO ya italia na kufanikiwa kuitoa kwa ushindi wa 1-0 ugenini na kutoka sare nyumbani ya 3-3 na hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 4-3.
Katika hatua iliyofuata ya robo fainali waliweza kukutana na VALENCIA na hapo ndipo safari yao ilihitimishwa baada ya kufungwa 3-0 nyumbani na kisha 1-0 ugenini na kuwa jumla ya mabao 4-0,Hivyo ndoto zao kutokutimia.
Lakini wanasema siku zote "asiyekata tamaa hufanikiwa" na hivi ndivyo bahati ya mtende ya aina yake ilivyowadondokea PFC LUDOGORETS katika msimu wa 2014-2015 wakiianza safari ya kwenda UEFA CHAMPIONS LEAGUE walifanikiwa kupita katika hatua za awali baada ya kuzitoa klabu kama F91 DUDELANGE na PARTIZAN BELGRADE na kufanikiwa kwenda katika hatua ya play off ambapo waliweza kukutana na STEAUA BUCURESTI ya ROMANIA na kufanikiwa kuiondosha bila huruma na kustaajabisha watu kama si kuwashangaza! kwa kuiondoa kwa mikwaju ya penalti ya 6-5 baada ya wote wawili kuwa kila mmoja ameshinda katika michezo yote 2 kwa 1-0 hivyo kuwa jumla ya mabao 1-1.
Na hapa ndipo walipofanikiwa kuingia hatua ya makundi ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE kwa mara ya kwanza na kuufuta ule mkosi wao waliokuwa nao huko nyuma ya kushindwa kufuzu.
CHUKUA BAADHI YA VITUKO AU MAMBO YA KUFURAHISHA KUTOKA KWAO.
Ama kwa hakika wewe mshabiki wa mpira ungependa kujua nini kinachovutia kutoka kwao basi sio kingine bali ni huyu beki wao wa katikati kutoka nchini ROMANIA aitwaye COSMIN MOTI ambaye ana mikasa kama 2 hivi, mkasa wa 1 ni pale siku moja walipokuwa wakicheza katika moja ya mechi za ligi yao ya nyumbani dhidi ya LEVSKI SOFIA ugenini aliwahi kumwomba mwamuzi asimamishe pambano ili aende kujisaidia haja ndogo iliyokuwa imembana na mwamuzi alipomruhusu huwezi kuamini alikaa chooni dakika takribani 7 na walipomfuatilia walikuta akiwa anaongea na mpenzi wake kwenye simu na hapo mwamuzi alimpa kadi nyekundu kwa kuwa mdanganyifu mpaka mashabiki wakampa jina la "desueyer" kwa kibulgaria yaani "mdanganyifu".Na tukio la pili ni hili la majuzi tu,baada ya kuonekana shujaa wa timu baada ya golikipa wao aitwaye VLADISLAV STOYANOV kutolewa kwa kadi nyekundu katika dakika za mwisho za mchezo katika mechi ya kuwania kufuzu UEFA CHAMPIONS LEAGUE dhidi ya STEAUA BUCURESTI na wakiwa wamemaliza substitutes zote,COSMIN MOTI tena aliweza kuingia golini na kuokoa penalti 2 na hivyo kuonekana shujaa wa usiku huo na kufanikiwa kuiwezesha PFC LUDOGORETS kufuzu kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE na wakiwa ni timu ya pili kutoka nchini BULGARIA kufanikiwa kuingia katika hatua hiyo.Huyo ndio COSMIN MOTI BWANAAA!!.
KIPI WANACHOTARAJIA KUKIONESHA NDANI YA UEFA CHAMPIONS LEAGUE???
Wakiwategemea wachezaji wao kama mshambuliaji namba 9 ROMAN BEZJAK,pamoja na kiungo wao mhispania kama DANI ABALO,pamoja na mreno kama FABIO ESPINHO labda wanaweza kuvuna kitu na kustaajabisha mashabiki wengi ndani ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE msimu huu.
Lakini nadhani kufika kwao tu hapo katika hatua ya makundi ya mashindano makubwa kama hayo ni faraja kubwa zaidi pamoja na mafanikio.
Na labda pia kutua kwa nyota wakubwa duniani katika uwanja wao wa LUDOGORETS ARENA kama CRISTIANO RONALDO,GARETH BALE,KARIM BENZEMA bila kusahau wachezaji kama STEVEN GERRAD,MARIO BALOTELLI pale tu watakapopambana nao itakuwa ni furaha kubwa kwa wapenzi na mashabiki wa PFC LUDOGORETS kuwaona kwa macho nyota hao wakubwa ulimwenguni.
VIVA PFC LUDOGORETS !! KARIBUNI UKUBWANI LUDOGORETS!
KARIBUNI TENA SANA LIGI YA MABINGWA ULAYA!.
Imeandaliwa na Fahim Wasso kutoka Wapenda Soka (kandanda) group katika facebook.
Powered by www.facebook.com/wapendasoka-kandanda
No comments