THE GUNNING MACHINE ~ MSIMU MPYA, MATATIZO YENYE BURUDANI ILE ILE.

 
Msimu wa 9 bila kikombe? Inawezekana. Kwa nini isiwezekane kama iliwezekana kwa miaka 8 iliyopita?
Kitu kizuri ni kwamba mpira tunaupenda kwa dhati. Tunaupenda kwa sababu unatupa furaha, burudani na unatupa watu wazuri. Hata katika kipindi chote ambacho tumeishi bila vikombe, mpira umeendelea kutupa burudani ile ile.
Tumeona magoli ya Robin Van Persie, chenga za Samir Nasri, ubabe wa Alex Song, pasi za Cesc Fabregas, kasi ya Theo Walcott, mashuti ya Thomas Rosicky na vingine vingi vinavyoufanya mpira uzidi kukaa mioyoni mwetu.
Raha ya aina hiyo imerudi tena mpenzi msomaji. Kikubwa ninachoamini kama mpenzi wa Arsenal ni kwamba tunakwenda kuona magoli, chenga, ubabe ubabe, pasi nzuri nk.
Wengi walitegemea mabadiliko makubwa msimu huu ambayo pengine hayajafanyika kama yalivyokuwa matarajio yao. Hii inawapa wasiwasi sana. Lakini kwa namna nyingine yapo mabadiliko kwenye kikosi cha Arsenal.
Kikosi kimepunguzwa kwa kiasi kikubwa, wachezaji wengi wameondoka kwa mikopo kama siyo kuondoka jumla na kujiunga na timu nyingine.
Watu kama Sebastien Squilacci, Francis Coquelin, Maroane Chammack, Andrey Arshavin, Vito Mannone, Gervinho, Ignash Miquel nk, hawatakuwepo London Colney msimu huu.
Kutakuwa na sura mpya kama Yaya Sanogo aliyesajiliwa. Thomas Eisfeld, Serge Gnabry na pengine Ryo Miyaichi (kama hawatapelekwa mahali kwa mkopo) ambao ni wageni kwenye kikosi cha kwanza.
Kwangu hayo ni mabadiliko, japo naelewa hitaji la kupata wachezaji wenye uzoefu na michuano mikubwa.
Kitu kizuri ni kwamba, sehemu yote ya wachezaji wetu tegemeo haijapotea. Hatujapoteza unahodha wa Thomas Varmaelen, roho ngumu ya Laurent Coscielny, ubosi wa Mikel Arteta, ufanisi wa Jack Wilshere, kasi ya Theo Walcott, chenga za Santi Cazorla, umahiri wa Thomas Rosicky, wala hatujapoteza mashuti ya Lucas Podolski.
Hawa ni wachezaji wenye uzoefu na mashindano makubwa.
Nikiwajumuisha hwa na damu changa za akina Gidion Zelalem, ninapata mseto mzuri tu.
Pamoja na uhakika huo wa kuona soka zuri, lakini niseme ukweli wangu kutoka moyoni kwamba mpaka sasa hatuna ubora wa kutosha.
Ubora wa timu unapimwa kwa vikombe vinavyopatikana na pengine ningepaswa kusema haya mwishoni mwa msimu lakini sipo hapa kuwadanganya wasomaji wangu kwamba nina uhakika wa Arsenal hii kufuta ukame msimu huu.
Sitaki kusema mengi kabla ya mechi ya kuwania kucheza hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa. Tunacheza na Fenerbahce ya Uturuki Agosti 21.
Zaidi tu niwatakie wapenda soka wote msimu mzuri wa burudani ambao tuliukosa kwa takribani siku 90.
 
Ahsante.
Imeandikwa na Richard Leonce Chardboy wa Wapenda soka (kandanda) Group katika Facebook
Nipate katika chardboy74@gmail.com na @chardboy77 kwenye twitter. Au 0766399341.
Usiache kulike page ya Wapendasoka-Kandanda kwenye Facebook.

No comments

Powered by Blogger.