LIGI KUU TANZANIA BARA ~ SIMBA NA YANGA KUANZA NA WALIOPANDA DARAJA
Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara itaanza rasmi leo kwa viwanja saba kuwa katika wakati mgumu. Timu zote 14 zitaingia katika viwanja 7 kuwania point 3 muhimu katika mechi zitakazoanza saa 10 na nusu jioni.
Ligi kuu msimu uliopita ilimalizika mwezi Mei ambapo Yanga ya Dar Es Salaam waliweza kua mabingwa wapya baada ya kuwapokonya watani zao Simba huku Azam fc ikikamata nafasi ya Pili.
Msimu uliopita ulishuhudia timu 3 zikishuka daraja ambazo ni Toto Afrika ya Mwanza, African Lyon ya Dar Es Salaam na Polisi ya Morogoro huku timu zingine 3 zilipanda daraja ambapo zitacheza katika ligi kuu msimu huu ambazo ni Ashanti ya Dar Es Salaam, Mbeya City ya Mbeya na Rhino Rangers ya Tabora.
Ligi kuu Inaanza kwa Mabingwa watetezi Yanga kuialika Ashanti ya Ilala Dar katika mchezo utakaopigwa katika uwanja wa Taifa Jijini Dar mchezo ambao unategemewa kuwa wa ushindani kwani Ashanti ina vijana wengi ambao ni watundu wa kuchezea mpira huku wakiongozwa na winga wa zamani wa Yanga Said Maulid.
Simba wao watakua Tabora kuikabili timu iliyopanda daraja ya maafande wa Tabora hii ni Rhino Rangers. Baada ya muda mrefu kupita bila kuingiza timu ligi kuu Rhino imepanda na kuwapa matumaini mapya wana Tabora kuishuhudia ligi kuu Tanzania bara.
Azam Fc wao watakua uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro kuwakabili Mtibwa Sukari huku katika uwanja wa Shekhe Amri Abeid JKT Oljoro ya Arusha ikiwaalika Coastal Union timu inayotarajia kuleta upinzani mpya msimu huu baada ya kuwaongeza wachezaji watatu toka Simba ambao ni Haruna Moshi Boban, Juma Nyosso na Uhuru Suleiman.
Mkoani Tanga, Mgambo JKT watawaalika maafande wenzao wa Ruvu JKT katika mchezo utakaopigwa katika uwanja wa Mkwakwani huku ukitarajiwa ubabe katika mchezo huo wa Wanajeshi.
Katika Dimba la Sokoine jijini Mbeya wageni wa ligi timu ya Mbeya City wataialika Kagera Sukari tuka mkoani Kagera wakati katika Uwanja wa Mabatini pale Pwani maafande wa Ruvu Shooting watawalika maafande wa Magereza timu ya Prisons ya Mbeya.
Ligi kuu msimu huu inaendelea kudhaminiwa na kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom Tanzania huku Azam Media wakitarajia kurusha mechi za ligi hiyo japo mpaka leo hawajaanza kurusha matangazo yao.
Unadhani timu gani itaibuka bingwa wa msimu huu mpya?
~~ Edo ~
No comments