STARS YA TAFUTA "SUMU" YA KUIUWA IVORY COAST

Wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, wakiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana alfajiri wakitokea Morocco walikofungwa 2-1 katika mechi ya awali ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014. Kocha wa Stars, Kim Poulsen alisema jana timu hiyo inaanza mazoezi leo kwa ajili ya kuikabili Ivory Coast Dar es Salaam Jumapili hii
Kikosi cha timu ya taifa ya soka ya Tanzania (Taifa Stars) kilichorejea nchini jana alfajiri kikitokea jijini Marrakech, Morocco kinaanza mazoezi leo kujiandaa kwa mechi ya marudiano dhidi ya Ivory Coast itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuwania kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika Brazil mwakani.
Kocha wa Stars, Kim Poulsen alisema kuwa baada ya kurejea jijini Dar es Salaam, vijana wake walipata mapumziko ya siku moja na leo wataripoti na kuanza kujifua kwa nia ya kuhakikisha kuwa wanafanya vizuri dhidi ya Ivory Coast wanaoongoza katika kundi lao la C.
Alisema kuwa kikosi chake kitakuwa kinafanya mazoezi mara mbili, asubuhi na jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
“Wachezaji wanafahamu kuwa Ivory Coast ni timu nzuri na ndiyo wanaoongoza kwa ubora wa soka Afrika. Na wanatambua umuhimu wa kushinda mechi ijayo hivyo kila mmoja amepania kujiweka vizuri kwa kabla ya mechi hiyo,” alisema Poulsen ambaye kikosi chake kililala ugenini kwa mabao 2-1 licha ya kuonyesha kiwango cha juu dhidi ya mabingwa wa Afrika wa mwaka 1976, Morocco

Mungu ibariki Taifa Stars
Mungu ibariki Tanzania

Imeandaliwa na Bab Chicharito

No comments

Powered by Blogger.