THE GUNNING MACHINE ~ SIR. FERGUSON VS ARSENAL (SEHEMU YA PILI)
Wiki 2 zilizopita, tulianza kujikumbusha vita ya kwanza ya Old Traford iliyopigwa mwaka 1990 kisha tukajikumbusha pia mpambano mkali na wa kusisimua uliopigwa Highbury mwaka 1997.
Leo The Gunning Machine inaendelea kukukumbusha matukio na nyakati ambazo zinamfanya kocha anayestaafu wa Man United, Sir Alex Ferguson asiweze kuisahau Arsenal katika maisha yake.
Endelea...
Arsenal ni timu ambayo inapopitia wakati mzuri basi unakua mzuri kweli kweli. Unajua kuwa Arsenal waliwahi kucheza katika uwanja wao wa nyumbani (wa zamani) kwa miezi 20 bila kufungwa na timu yoyote?
Miezi 20 ni sawa na miaka miwili kasoro miezi minne. Hii ni rekodi ambayo Arsenal walijiwekea mwaka 1999. Kwa mtu mwenye wivu wa ushindani kama Fergie, bila shaka rekodi hii ilikua inamuudhi sana.
Basi August 22,1999 akiwa katika kampeni ya kusaka taji lake la 13 la ligi kuu, akakutana na Arsenal katika uwanja huo wa Highbury.
Arsenal wakiwa wanachagizwa na usajili wa Davor Sucker, mkali kutoka Croatia ambaye alikua anatisha sana wakati huo, kuja kuungana na wakali wengine wa Arsenal kama Vieira, Parlour, Henry nk.
Lee Dixon akachukua mpira dakika ya 41 ya mchezo kisha akamwona Nwankwo Kanu kwenye winga ya kulia, akamtangulizia. Kanu akaingia nao ndani, akataka kugonga One-Two na Bergkamp lakini alivompa Bergkamp One, hakumrudishia. Badala yake akampa Freddie Ljunberg ambaye alikua anachomoza mbele. Ljunberg akafanya kuusogeza tu mbali na golikipa kuandika goli la kwanza kwa Arsenal. Kipindi cha kwanza kikaisha.
Dakika 10 baada ya kipindi cha 2 kuanza, krosi ya David Beckham kutoka karibu na kibendera cha kona, ikatua kwenye kichwa cha Andy Cole aliyekuwa upande wa pili wa 'penalt box' ya Arsenal.
Mpira ukampita kirahisi golikipa Alex Manninger, ukawa unaambaa ambaa kwenye mstari wa goli, lakini kabla haujaingia, shetani akamtuma Dwight Yorke ambaye tayari alikuwa kwenye mtego wa kuotea. Akaugusa mpira huo na kusababisha bao hilo kukataliwa.
Ajabu na kweli, dakika tano tu baadaye, kwa 'muvu' ya vile vile, lakini safari hii ikimkuta Roy Keane, akafanikiwa kuutia mpira kambani na kuisawazishia Man United.
Arsene Wenger akafanya kosa kubwa kwa kumtoa Nwankwo Kanu ambaye ndiye aliyekuwa chachu ya mashambulizi ya Arsenal. Nafasi yake ikachukuliwa na Marc Overmas ambaye hakucheza vibaya lakini hakusumbua sana kama Kanu.
Davor Sucker akaingia kuchukua nafasi ya Thierry Henry.
Zikiwa zimesali dakika 2 tu mchezo kumalizika, Man United wakafanya shambulio kali langoni mwa Arsenal na Roy Keane kwa mara nyingine tena akafanikiwa kutikisa nyavu za Arsenal.
Fergie akawa amefanikiwa kukomesha rekodi ya Arsenal ya kutofungwa katika uwanja wa nyumbani kwa miezi 20. Siyo Wenger wala Fergie anayeweza kuisahau mechi hiyo.
VITA YA PILI YA OLD TRAFORD-2003
Ni katika kampeni ambayo Arsenal walimaliza msimu bila kufungwa. Ilibaki kidogo tu Man United watibue rekodi hiyo.
Kama kawaida ya Fergie, aliingia na mbinu za ushindi katika mchezo huu akijua kwamba Gunners watawakosa Robert Pires na Sylvain Wiltort waliokuwa majeruhi.
Pia kifo cha baba mzazi wa Sol Campbel kilimaanisha Martin Keown na Kolo Toure watasimama kwenye ulinzi.
Man United wakiwa na Christiano Ronaldo walipewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo.
Mchezo ulienda vizuri sana lakini vita hasa ilianzishwa na Ruud Van Nistelrooy dakika ya 80 ya mchezo baada ya kumrukia nahodha Patrick Viera.
Vieira akaanguka chini na Filimbi ikalia. Wakati Vieira ananyanyuka, akaugusa kidogo mguu wa Van Nistelrooy.
Basi Rud Van Nistelrooy akajitupa chini kama kafanyiwa rafu mbaya sana. Mpaka uangalie marudio ndo utagundua kuwa alidanganya.
Mwamuzi akamwonesha Vieira kadi ya njano ambayo ilikuwa ni ya pili kwake. Akaenda nje huku wachezaji na mashabiki wa Arsenal wakimlaani vikali Van Nistelrooy.
Mchezo ukaendelea huku Arsenal wakionekana kuzidiwa katika dakika za mwisho. Ule usemi kwamba Man United anabebwa ulionekana kuthibitika siku hiyo ingawa ukiitazama tena mechi hiyo leo, utagundua hakukuwa na hujuma zozote kwa Arsenal.
Hali ikawa mbaya zaidi baada ya Keouwn kumweka chini Diego Forlan na mwamuzi kuamuru Penati katika dakika ya 91.
Rud Van Nistelrooy akaenda kupiga penati lakini Mungu si Chardboy. Jens Lehman akaugusa, mpira ukagonga mlingoti ukaenda nje.
Baada ya tukio hilo ndipo wachezaji wa Arsenal wakiongozwa na Martin Keouwn walipomfuata Van Nistelrooy na kuanza kumzodoa kwa staili ya kukera huku wakishangilia.
Halikua tukio la kiungwana, na siku chache baadae FA iliwafungia wachezaji wanne wa Arsenal. Hali hiyo ilizaa chuki kubwa kati ya Ruud Van Nistelrooy na wachezaji wa Arsenal.
Wiki ijayo tutaona Arsene Wenger alisema nini juu ya Van Nistelrooy na Fergie alichomjibu. Pia tutaiangazia vita kali kati ya Vieira na Keane. Hapa hapa.
Imeandikwa na Richard Leonce Chardboy wa Wapendasoka Kandanda Group.
Nipate katika wapendasoka@gmail.com na @chardboy77 kwenye twitter. Au 0766399341
No comments