VIGOGO HALI MBAYA KOMBE LA FA, YANGA NAYO YATUPWA NJE NA SINGIDA
Mabingwa wa Soka Tanzania bara Dar es Salaam Young Africa maarufu kama Yanga wameaga rasmi mashindano ya kombe la FA maarufu kama Azam Sports Federations Cup baada ya kutolewa Kwa changamoto ya mikwaju ya penati 4-2 na Singida United.
Mechi hiyo ya mwisho ya hatua ya Robo fainali ya michuano hiyo ambayo msimu huu ni wa tatu kwake ilimalizika Kwa sare ya bao 1-1 hivyo changamoto ya mikwaju ya penati ikatumika kuamua mshindi.
Mvua kubwa iliyopiga katika dimba la Namfua hapa mjini Singida ilipoteza ladha yake hasa dakika 30 za mwanzo baada ya uwanja kuwa na Maji hivyo mpira kushindwa kutulia.
Yusuph Mhilu wa Yanga ndiye aliyeipatia Yanga bao la kwanza kipindi cha kwanza lakini dakika 2 tu baada ya kuanza kipindi cha pili Singida walisawazisha bao Hilo kupitia Kwa Mshambuliaji wake Kenny Ally na kufanya mchezo huo kumalizika Kwa sare hiyo ya bao 1-1.
Kipindi cha Pili baada ya mvua kutulia Singida walionekana kuwa bora wakilishambulia vilivyo lango la Yanga na kama si uhodari wa kipa Youth Rostand basi Yanga walikua wapoteze ndani ya dakika 90.
Ikiwa imebaki dakika moja kabla ya mchezo kumalizika kocha wa Singida alimtoa Kiggy Makasi na nafasi yake kujazwa na Elinywesia Sumbi ambaye ndiye alikua shujaa wa Singida United Leo akifunga penati ya ushindi na kuipeleka Singida United hatua ya nusu fainali ambapo watacheza na JKT Tanzania huku Mtibwa Sugar wao wakipangwa kucheza na Stand United.
Bingwa wa michuano hiyo ndiyo atakayeiwakilisha Tanzania katika michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika na msimu ujao ni dhahiri tutapata mwakilishi mpya nje ya Yanga, Azam FC na Simba.
No comments