HAKUNA ALIYE SALAMA KWA SIMBA: YANGA NAYO YAKUMBANA NA KICHAPO TAIFA
Vinara wa ligi kuu soka Tanzania bara Wekundu wa Msimbazi Simba wameendelea kugawa kwa kila timu inayojaribu kuizuia kuchukua ubingwa wa ligi kuu msimu huu baada ya kuwatandika watani zao Yanga bao 1-0 katika mchezo uliomalizika hivi punde kwenye dimba la Taifa Jijini Dar es Salaam.
Tangu kuanza kwa mchezo huo ni kama mashabiki wa Simba walikuwa wakijua kabisa wataibuka na ushindi katika mchezo wa leo wakiujaza vilivyo uwanja wa Taifa huku kukiwa na mapengo katika jukwaa la yanga.
Dakika ya 37 Simba walipata bao la kwanza baada ya Shomari Kapombe kuangushwa na Kelvin Yondani na kusababisha mpira wa adhabu ndogo ambayo ilipigwa na Shiza Kichuya na kumkuta Erasto Edward Nyoni ambaye aliunganisha na kuiandikia Simba bao la kwanza na bao pekee katika mchezo huo na mpaka mapumziko Simba walikua mbele kwa bao hilo 1.
![]() |
Kichuya akiukontroo mpira mbele ya wachezaji wa Yanga |
Kipindi cha Pili kilipoanza tu Benchi la Ufundi la Yanga lilimtoa Raphael Daudi na kuingia Juma Mahadhi lakini dakika ya 48 Yanga walijikuta wakicheza pungufu baada ya Hassan Kessy Ramadhani akipata kadi ya pili ya njano kufuatia kumfanyia madhambi Asante Kwasi.
Dakika ya 50 James Kotei wa Simba alipata kadi ya njano kufuatia kumfanyia madhambi Kelvin Yondani na mwamuzi kumzawadia kadi hiyo ikiwa ni kadi pekee waliyopata Simba katika mchezo wa leo.
Dakika ya 62 Yanga walimtoa Ibrahim Ajibu na nafasi yake kuchukuliwa na Pius Buswita na dakika ya 80 Emmanuel Martin aliingia kuchukua nafasi ya Papy Tshishimbi wakati Simba wao walifanya mabadiliko mara moja pekee walimtoa Nicholous Gyan na kuingia Paul Bukaba Bundala.
Simba ambayo haijafungwa mchezo wowote mpaka sasa inahitaji pointi 4 tu kuweza kutawazwa mabingwa wapya katika msimu huu na Mchezo ujao watacheza dhidi ya Ndanda FC.
No comments