AZAM TV YAKUBALI KUIRUSHA YANGA TV KWA MIAKA MITATU
Wapenzi na mashabiki wa Soka hususani mashabiki wa Mabingwa watetezi wa ligi
kuu ya Vodacom Tanzania bara na wawakilishi pekee waliobaki katika michuano ya
kimataifa Dar es Salaam Young Africans maarufu kama Yanga kuanzia sasa wataanza
kuona habari za Yanga kupitia kipindi maalumu cha Yanga TV ambacho kitaanza
kuruka hewani kupitia king'amuzi cha Azam.
Leo Jumanne Yanga imeingia mkataba wa makubaliano na Uongozi wa Azam Media ya kurusha Kipindi cha luninga cha Yanga TV Show ambacho kitaanza kuonekana katika kingamuzi cha Azam kuanzia Aprili Mosi mwaka huu.
Makubaliano baina ya Yanga na Azam Tv yamefikiwa leo katika makao makuu ya klabu hiyo baina uongozi wa Yanga na Mkurugenzi wa vipindi vya michezo wa Azam TV, Baruhan Mhuza ambapo imetajwa kwamba mkataba huo utakua ni wa miaka mitatu ambapo kwa kipindi chote hicho Azam media watakua wakirusha kipindi hicho.
Baruhan amesema kipindi hicho kitaandaliwa na Yanga wenyewe na kutangazwa na watangazaji kutoka Yanga huku Azam TV ikirusha tu.
Hii si mara ya kwanza Azam Tv kurusha vipindi maalumu vya luninga kwa timu za Tanzania kwani tayari kupitia kituo hicho Wapenzi wa soka wanaweza kuona vipindi vingine vinavyohusu klabu zao ambazo ni Azam Fc na Simba
No comments