KIPIGO CHA GREEN WARRIORS CHAMFUKIZISHA KAZI OMOG


Siku moja baada ya kutolewa kwenye michuano ya kombe la Azam Sports Federation Cup na timu ya Green Warriors hapo jana klabu ya Simba imeamua kumfuta kazi kocha wake Joseph Omog.

Simba ilitolewa kwa mikwaju ya penati 4-3  baada ya kutoka sare ya bao moja katika muda wa kawaida mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Azam Complex jana.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano wa klabu ya Simba Hajji Manara inasema Uongozi umeamua kuachana na raia huyo wa Cameroon kutokana na kutoridhika na kiwango cha uchezaji hasa kwenye mchezo wa jana.

Licha ya Simba kuongoza ligi kwa tofauti ya mabao wakifungana pointi na Azam FC, Omog amekuwa akipigiwa kelele na washabiki na wanachama wa Wekundu hao kutokana na kupata ushindi kwa tabu.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa kwa sasa kikosi cha Simba kitakuwa chini ya kocha msaidizi Masoud Djuma mpaka atakapo patikana kocha mkuu.

Mchezo wa kwanza wa kocha Djuma kukiongoza kikosi hicho utakuwa dhidi ya Ndanda FC utakaofanyika kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona wikiendi ijayo.

No comments

Powered by Blogger.