AZAM KUKIPIGA NA MVUVUMWA KESHO CHAMANZI
Timu ya Soka ya Azam FC,
inatarajia kucheza dhidi ya Mvuvumwa ya mkoani Kigoma katika mchezo wa kirafiki
unaotarajia kufanyika Uwanja wa Azam Complex kesho Jumatano saa 1.00 usiku.
Mchezo huo ni wa pili wa kirafiki kwa Azam FC
katika kipindi hiki ligi iliposimama kupisha michuano ya Kombe la Chalenji
inayoendelea nchini Kenya, baada ya Jumamosi iliyopita kukipiga na Friends
Ranger na kutoka sare ya bao 1-1, bao la matajiri hao likifungwa na
mshambuliaji mpya Bernard Arthur.
Wakati Azam FC ikiutumia mchezo huo kujinoa
kuelekea mechi zijazo, Mvuvumwa itakuwa kwenye maandalizi kuelekea raundi ya
pili ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL).
Benchi la Ufundi la Azam FC chini ya Mromania,
Aristica Cioaba, limepanga kucheza mechi nne kali za kirafiki katika kipindi
hiki cha mapumziko ya ligi, ambapo tayari imeshacheza mechi moja tu wikiendi
iliyopita.
Mechi hizo ni sehemu pia ya mazoezi ya
kumuunganisha kwenye timu na wachezaji wenzake, mshambuliaji Arthur
aliyesajiliwa kwenye usajili wa dirisha dogo akitokea Liberty Professional ya
Ghana.
Mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi na Ngao ya
Jamii msimu uliopita wanaodhaminiwa na Maji safi kabisa ya Uhai Drinking Water,
Benki ya NMB ambayo ni bora kwa sasa nchini na Tradegents, wamekuwa na mwenendo
mzuri kwenye ligi baada ya kucheza mechi 11 na kujikusanyia jumla ya pointi 23.
Katika
mechi hizo imeshinda mechi sita na sare tano ikiwa kwenye nafasi ya pili sawa
na kinara Simba waliojikusanyia nao pointi hizo lakini wakiwa juu kwa tofauti
ya mabao ya kufunga na kufungwa huku ikiwa ndio timu pekee iliyofungwa mabao
machache ikifungwa matatu tu hadi sasa.
Source: Azam website
No comments