OBREY CHIRWA WA YANGA NDIE MCHEZAJI BORA ZAIDI LIGI KUU MWEZI OKTOBA
Mshambuliaji wa Young Africans ya Dar es Salaam,
Obrey Chirwa amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Oktoba wa Ligi Kuu ya Vodacom
(VPL) msimu wa 2017/2018.
Chirwa raia wa Zambia alitwaa tuzo hiyo baada ya
kuwashinda wenzake wawili, beki Erasto Nyoni wa Simba na mshambuliaji Ibrahim
Ajibu pia wa Young Africans alioingia nao fainali.
Chirwa ameibuka kidedea katika uchambuzi uliofanywa
na Kamati ya Tuzo za VPL zinazotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) kutokana na mapendekezo kutoka kwa makocha waliopo viwanja mbalimbali
ambavyo ligi hiyo inachezwa msimu huu.
Mshambuliaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa Young
Africans mwezi huo ikipata pointi saba katika michezo mitatu iliyocheza na
kupanda katika msimamo wa ligi kutoka nafasi ya sita iliyokuwepo mwezi Septemba
hadi ya pili mwishoni mwa Oktoba.
Young Africans iliifunga Kagera Sugar mabao 2-1
Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, ambapo Chirwa alifunga bao moja na kutoa pasi ya
mwisho ya bao moja, pia Yanga iliifunga Stand United mabao 4-0 Uwanja wa
Kambarage, Shinyanga, ambapo Chirwa alifunga bao moja na kutoa pasi ya mwisho
ya bao moja.
Kiwango cha mchezaji huyo kilionekana pia katika
mchezo wa watani wa jadi Yanga na Simba uliofanyika Oktoba 28, 2017 Uwanja wa
Uhuru, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Bao la Yanga lilifungwa
na Chirwa, hivyo kwa mwezi huo alifanikiwa kuwa na kiwango cha juu katika kila
mchezo ikiwa ni pamoja na kufunga.
Kwa upande wa Erasto naye alitoa mchango mkubwa kwa
Simba uliowezesha timu hiyo kupata pointi nane katika michezo minne iliyocheza,
akitoa pasi za mwisho za mabao nne, ambapo Simba ilishinda michezo miwili na
kutoka sare miwili, huku Ajibu akitoa mchango mkubwa kwa Yanga ikiwa ni pamoja
na kufunga mabao matatu na kutoa pasi ya mwisho ya bao moja.
Wachezaji wengine ambao tayari wameshinda Tuzo ya
Mchezaji Bora wa mwezi wa VPL msimu huu ni mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi
(Agosti), beki wa Singida United, Shafiq Batambuze (Septemba).
Kampuni ya Vodacom, ambao ndiyo wadhamini wa ligi
hiyo ina utaratibu wa kuwazadiwa wachezaji bora wa kila mwezi, huku pia mwisho
wa msimu kukiwa na tuzo mbalimbali zinazohusu ligi hiyo, ambapo msimu wa mwaka
2016/2017 kulikuwa tuzo 16 zilitolewa kwa washindi wa kada mbalimbali.
Chirwa atazawadiwa Sh milioni moja kwa kuibuka
Mchezaji Bora wa Oktoba.

No comments