BILA TSHISHIMBI NA YONDANI YANGA YATOA DOZI NENE KWA MBEYA CITY

Ikiwa bila ya wachezaji mahiri wa kikosi cha kwanza kiungo Mkongomani Papy Tshishimbi na beki Kelvin Yondani mabingwa watetezi wa ligi kuu timu ya Yanga imeibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Mbeya City.

Tshishimbi na Yondani ambao wamekuwa mhimiri mkubwa wa kikosi cha kocha George Lwandamina wamekosekana kwenye mchezo huo baada ya kuwa majeruhi.

Mshambuliaji Obrey Chirwa alikuwa nyota wa mchezo huo baada ya kufunga mabao matatu 'hat trick' akifisha mabao sita na kuwa wa pili katika orodha ya wafungaji wa ligi mpaka sasa.

Mzambia huyo alifunga mabao hayo dakika za 20,50 na 59 huku Emanuel Martin nae akifunga mawili na kuhitimisha ushindi huo kwa mabingwa hao.

Huu unakuwa ushindi  mkubwa wa Yanga baada ya ule wa mabao 4-0 dhidi ya Stand United majumaa kadhaa yaliyopita.

Mechi nyingine Azam FC imeendelea kupata ushindi kiduchu baada ya kuifunga Njombe Mji bao 1-0 uwanja wa Sabasaba.

Kagera Sugar imepata ushindi wake pili msimu huu na kupanda hadi nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi baada ya kuifunga Mtibwa Sugar bao 1-0 kwenye uwanja wa Manungu mkoani Morogoro.

Kagera ilikuwa mkoani mwa msimamo kwa muda mrefu baada ya kuanza ligi vibaya lakini wameanza kubadilika na kupata ushindi wa pili wakiwa na pointi zao 10.

No comments

Powered by Blogger.