YANGA KAMA SIMBA JANA, YAIPIGA STAND NNE

Mabingwa watetezi wa ligi ya Vodacom timu ya Yanga imepata ushindi mkubwa msimu huu baada ya kuifunga Stand United mabao 4-0 kwenye uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Nyota Ibrahim Ajib ambaye yupo kwenye kiwango bora kwa sasa ameendelea kudhihirisha kuwa Yanga haikufanya makosa kumsajili kutoka Simba baada ya kufunga mabao mawili kwenye ushindi huo.

Yanga ambayo wiki ijayo itakutana na watani wao wa jadi Simba ilionyesha uwezo mkubwa huku kocha George Lwandamina akitumia baadhi ya wachezaji ambao alikuwa hawapi nafasi.

Kocha huyo raia wa Zambia aliwapanga nahodha Nadir Haroub 'Canavoro, Hassan Kessi na Pato Ngonyani ambao alikuwa hawapi nafasi sana tangu msimu ulivyoanza.

Matokeo hayo ni sawa na yale waliyopata Simba jana dhidi ya Njombe Mji hivyo kufanya mchezo baina yao utakaopigwa Oktoba 28 kuwa mkali kutokana na uwezo wa timu zote.

Mabao mengine ya Yanga yalifungwa na Pius Buswita na Obrey Chirwa na kuifanya Yanga kufikisha pointi 15 sawa na Simba lakini wakizidiwa mabao ya kufunga.

No comments

Powered by Blogger.