SHAFIK BATAMBUZE WA SINGINDA NDIE MCHEZAJI BORA ZAIDI MWEZI SEPTEMBA LIGI KUU
Mchezaji wa timu ya Singida United, Shafik Batambuze
amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Septemba wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2017/2018.
Batambuze anayecheza nafasi ya
ulinzi wa pembeni, alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili,
Ibrahim Ajibu wa Yanga na kiungo Mohammed Issa wa Mtibwa Sugar, alioingia nao
fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam.
Uchambuzi huo kwa mujibu wa
utaratibu hufanywa na kikao cha Kamati ya Tuzo ya VPL inayotolewa na Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na mapendekezo kutoka kwa makocha
waliopo viwanja mbalimbali ambavyo ligi hiyo inachezwa msimu huu.
Mchezaji huyo alitoa mchango
mkubwa kwa Singida United kupata pointi 10 katika michezo minne, ambayo timu
yake ilicheza kwa mwezi huo, matokeo ambayo yaliiwezesha Singida United kutoka
nafasi ya 10 katika msimamo na kupanda hadi nafasi ya nne kwa mwezi huo wa
Septemba. Singida United ndiyo timu iliyokusanya alama nyingi kwa mwezi huo
ukilinganisha na timu nyingine 15 zinazoshiriki VPL.
Singida United iliifunga Mbao FC
mabao 2-1 Uwanja wa Jamhuri Dodoma, ikaifunga Stand United bao 1-0 Uwanja
wa Kambarage, Shinyanga, iliifunga Kagera Sugar Uwanja wa Jamhuri Dodoma na
ilitoka sare ya bao 1-1 na Azam FC uwanja huo huo. Michezo yote hiyo Batambuze
alicheza dakika zote 90 kwa kila mchezo, ambayo ni sawa na kucheza dakika
360.
Kwa upande wa Ibrahim Ajibu
alitoa mchango mkubwa kwa Yanga uliowezesha kupata pointi nane kwa mwezi huo,
baada ya kushinda michezo miwili na kutoka sare miwili, ambapo pia Mohammed
Issa aliisaidia timu yake kupata pointi nane katika michezo minne iliyocheza
mwezi huo, ikishinda miwili na kutoka sare miwili.
Kampuni ya Vodacom, ambao ndiyo
wadhamini wa ligi hiyo ina utaratibu wa kuwazawadia wachezaji bora wa kila
mwezi, huku pia mwisho wa msimu kukiwa na tuzo mbalimbali zinazohusu ligi hiyo,
ambapo msimu wa mwaka 2016/2017 kulikuwa tuzo 16 zilitolewa kwa washindi wa
kada mbalimbali. Batambuze atazawadiwa Sh milioni moja kwa kuibuka Mchezaji
Bora wa mwezi.
No comments