KIPAJI CHA NEYMAR KITAWEKA UFALME WA MUDA MREFU KATIKA SOKA
Muda unasogea na kutoa nafasi ya vizazi kubadilishana nyakati za kuishi duniani.
Huwezi ishi milele na ndiyo maana inakuwa ni vigumu kwa mtu yoyote kukaa sehemu moja milele kwa kiwango kile kile cha ufanisi.
Nguvu huisha kila umri unapohesabu namba, na ndiyo maana unapomaliza kuhesabu moja midomo hupewa nafasi ya kutamka namba mbili.
Ndivyo ilivyo kwenye maisha. Maisha ni nafasi, na nafasi hudumu kwa muda cha muhimu ni kuangalia namna unavyotumia nafasi unayopata kwa muda uliopangiwa.
Nafasi ya ufalme wa Saul iliishia mikononi mwa kijana mdogo Daudi ambaye naye alipoteza nafasi kwa Sulemani.
Hekima, busara na utajiri wa Sulemani haukumpa nafasi ya kutawala milele Israel.
Alikuwa na vitu vyote vya kumhakikishia atawale milele, lakini alikosa uwezo wa kuzungumza na muda.
Muda ndiyo hakimu wa falme mbalimbali, muda uliwahi pindua ufalme wa Pele, muda huo huo ukatengeneza ufalme wa Maradona.
Maradona alikuwa bora lakini ubora wake haukudumu milele. Sanaa za mpira wa Ronaldino zilikuwa zina ubora wa kutengeneza nyimbo yenye ala zote za music na sikio likaburudika.
Lakini sanaa zake hazikudumu mpaka leo ambapo macho yetu yanatamani kushuhudia tena ubora wa sanaa wa kuchezea mpira kama wa Ronaldinho.
Gaucho aliondoka Barcelona, hakuondoka mikono mitupu, alituachia mtu ambaye alituomba tumwangalie kwa jicho la ziada.
Mtu ambaye aliamini yeye ndiye atakuwa Mfalme wa soka.
Mtu ambaye ataweka kila aina ya kumbukumbu , kumbukumbu ambazo zitachukua vizazi vingi kuja kuzivunja pale Barcelona.
Messi ameibuka wakati ambao kuna mpinzani, mpinzani ambaye amefanya kubadilishana kwa kijiti cha ufalme wa soka kwa muongo mmoja uliopita .
Messi na Criastiano Ronaldo wamekuwa wachezaji bora kwa muongo mmoja uliopita.
Wamefunga magoli watakayo, wamefunga idadi ya magoli wayatakayo , wamewatesa mabeki na makipa kila walivyojisikia.
Waweza kuwachukia kwa sababu mmoja kati yao anaweza akawa hayupo kwenye timu yako , lakini kwa sababu wanautumikia mpira ni lazima ufurahie wanachokifanya.
Wameutendea mpira haki na mpira ukawatendea haki.
Wameupa mpira thamani kubwa nao mpira ukawapa thamani kubwa.
Wamepokea kila aina ya tunzo, wamekuwa hawakosekani kwenye orodha ya wachezaji bora wa dunia kwenye tunzo ya Ballon D'or na tunzo ile ya FIFA.
Wamekuwa wakipokezana hizi tunzo kwa muda wa muongo mmoja.
Kitu ambacho kinaonesha hakuna kati yao aliyetengeneza utawala wa kudumu kwa sababu ya upinzani mkali kati yao.
Mesi ana miaka 30 na Ronaldo ana miaka 32 , hapana shaka mkono wa kwa kheri unawakaribia kwa sasa.
Muda wao unaelekea mwishoni, nyakati zao zinaelekea mwisho kuruhusu nyakati mpya.
Nyakati za Neymar, mchezaji pekee anayebaki kwenye nyakati hizi mpya ambaye yuko daraja moja na kina Messi na Ronaldo.
Neymar anabaki peke yake, wapinzani wenzake wanaonekana hawana ubavu mkubwa wa kushindana na yeye.
Neymar anabaki hana mtu wa kufanya wabadirishane kijiti cha Ufalme.
Kila anayeonekana ana uwezo wa kushindana na Neymar , anakua hana kasi kubwa kama ya Neymar.
Neymar amekamilika kila idara.
Ndiyo maana anafunga sana na kutoa pasi za mwisho nyingi za magoli.
Sifa ambayo inamtenganisha na wale ambao anabaki nao kushindana nao.
Ubora wa Neymar ( wa kufunga sana , kutoa pasi nyingi za magoli na kuibeba timu ) ndiyo kigezo kikubwa cha kuwa mfalme wa hizi tunzo za Ballon D'or pamoja na ile ya FIFA.
Kigezo hicho kipo maradufu kwa Neymar na kipo katika kiwango cha kawaida kwa wengine wanaobaki baada ya Messi na Ronaldo kuondoka. Na ndipo hapo ninapoamini ufalme wa Neymar utadumu kwa muda mrefu bila kubugudhiwa
Martin Kiyumbi
No comments