PENATI YA DAKIKA ZA MWISHO YAIPELEKA SIMBA KIMATAIFA


Hatimaye Wekundu wa Msimbazi Simba wamerejea katika michuano ya kimataifa baada ya kushinda ubingwa wa kombe la Chama cha soka Nchini maarufu kama Azam Sports Federation Cup wakiifunga Mbao FC ya jijini Mwanza bao 2-1.

Haikua Rahisi kwa Simba ambayo mara ya mwisho kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa ilikua mwaka 2013 kwani ilibidi kusubiri dakika 30 za nyongeza kuweza kupata ushindi huo.

Hadi dakika 90 zinamalizika hakuna timu iliyofanikiwa kufunga goli ndipo zilipoongezwa dakika 30 katika mchezo huo uliopigwa kwenye uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma.

Fredrick Blagnon ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Hamis Ndemla aliifungia Simba bao la kuongoza akitumia vizuri mpira uliopigwa na Abdi Banda na kupiga shuti kali lililogonga mwamba na kuzama golini na kuamsha shangwe uwanja mzima ambao 90 ulitawaliwa na mashabiki wa Simba.

Furaha ya Simba ilizimwa na goli safi la Mbao FC lililofungwa na Robert Ndaki na kufanya kila mmoja aamini pengine penati zingeamua bingwa.

Mpira wa kona upande wa Mbao FC ulimpa mwanya James Kotei kupiga shuti lililowababatiza mabeki wa mbao na kusababisha penati ambayo ililalamikiwa sana na wachezaji wa Mbao FC lakini walitulia na kuruhusu Simba kupiga penati hiyo huku Shiza Kichuya akiwa ndiye mfungaji.

Kwa matokeo ya leo Simba imeweza kushinda kombe pia imejikusanyia kitita cha milioni 50 sambamba na kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika.

No comments

Powered by Blogger.