MIWANI PANA : KATIKA HILI LA SPORTPESA NAKUUNGA MKONO AVEVA.
Rais Aveva aliposaini Mkataba na Kampuni ya Sportpesa Ijumaa wiki iliyopita |
Pengine huu ndiyo mkataba mkubwa wa wazi kuwahi kuingiwa na klabu hiyo baada ya ule wa Kilimanjaro Lager ambao ulimalizika mwishoni mwa msimu uliopita na kuzua balaa katika malipo ya mishahara ya wachezaji na kupelekea klabu kuwa kama Omba omba mwanzoni mwa msimu uliopita hadi lilipokuja swala la ubinafsishaji ambalo lilikubaliwa kwa haraka na wanachama na viongozi ili kuinusuru klabu dhidi ya ukata mkubwa uliokua unaikabili.
Mohammed Dewji akajitolea kwa mapenzi yake kuweza "kuokoa jahazi" wakati ambao Simba ilipoanza mchakato wa "Kumpatia Timu MO" sakata ambalo baadae lilikuja kupigwa "STOP" na Serikali kupitia baraza la michezo la Taifa kwa sababu ambazo wao walizitoa japo Simba wao wanasema mchakato unaendelea.
Jana Jumapili siku mbili baada ya Simba kuingia mkataba na SPORTPESA mkataba ambao pengine utakomesha au kupunguza swala la Simba kuwa ombaomba kumeibuka mambo mengi yanayoleta hali ya mvurugano baina ya Viongozi kwani kupitia vyombo mbalimbali vya habari tumemsikia Mohammed Dewji akipinga Simba kuingia mkataba ambao kwake yeye anasema una thamani ya chini kwani tayari alishapata wadhamini wa kuweza kuwekeza mpaka bilioni 2 kwa mwaka endapo tu viongozi wangekamilisha mchakato wa yeye kupewa timu.
Yawezekana ni kweli MO amepata hao wadhamini lakini cha kujiuliza hapa kabla hatujapata taarifa rasmi toka kwa viongozi wa Simba hususani Rais Aveva ni jinsi gani Uongozi ungeweza kuachia Bilioni 2 kwa mwaka anazozisema MO hadi wakaenda katika mkataba huu wa milioni takribani 880 kwa mwaka? Katika Hili Aveva anapaswa kuja na utetezi ulioshiba ili wanasimba wamwelewe kwanini aliacha mkataba huu mnono wa MO na kusaini wa SportPesa.
MIWANI YANGU PANA Imegundua hapa kuwa pengine huo mkataba wa MO ni wa kufikirika zaidi ukitegemea na kukubalika kwa Mabadiliko ya Mfumo wa Uendeshaji na pengine ukachukua muda mrefu zaidi huku timu ikiwa haina vyanzo vya mapato ndiyo maana wakakubali kusaini na SPORTPESA.
Wapo watu wakiungana na MO ambao wamekuja na hoja za kuwapondea viongozi hasa Rais Aveva tena bila hata kumsikiliza kwanini basi alisaini mkataba huu na ni muda mfupi sana tunasahau jinsi viongozi wa Simba walivyohaha kupata fedha za kuendesha timu baada ya kujitoa Kilimanjaro Lager. Pengine huu ni mwanzo mzuri wa Simba kuepukana na maswala ya kuwa "ombaomba" kuendesha timu.
Vipi kama Aveva angekataa ule mkataba halafu kesho yake Swala la kumpa timu MO likashindikana na MO akaamua kutolipa tena mishahara timu ingekua katika hali gani? MO nae ni binadamu vipi kama akifa kesho (Siombei litokee hilo) ina maana Simba itakua kwenye hali gani wakati mkataba wa umiliki rasmi haujafanikiwa baina ya MO na Simba?.
Rais Aveva amesaini mkataba ule kwakua ndiye anayepata tabu ya kuomba wahisani wasaidie kulipa mishahara, Yeye ndiye anayetukanwa timu inapofanya vibaya na amefanya yale kwa Maslahi ya Simba na hata atakapokuaja kiongozi mwingine tayari atakua na pakuanzia.
Ni wakati sahihi sasa kwa Simba kuamka na kuangalia tena swala la Uwekezaji katika klabu yao hasa hili swala la Kumpa MO timu. Sipingi mabadiliko lakini aina ipi ya mabadiliko ya kiutawala yatafanikiwa na kutoleta mizozo kwa timu? Ikumbukwe tangu Simba ilipoanzishwa uendeshaji wa timu ni huu huu ambao kamwe haujawahi kuleta Machafuko zaidi ya kupingana kwa hoja.
Simba wanapaswa kubadili katiba yao ili iweze kuruhusu mwekezaji yeyote na sio lazima MO japo uwepo wa MO ni faida nyingine kubwa kwani ni Mwanafamilia wa Simba yatakua makosa makubwa kwa Mtazamo wangu kama mtazamo uliopo ni kumpa timu MO kwakua anaihitaji au kwakua Simba inamhitaji kwa sasa na kwa mtazamo wangu mimi EDO DC katiba ingebadilishwa ili kuruhusu uwekezaji na sio kumruhusu MO halafu ni vyema 50% zikaenda kwa wanachama na zilizobaki 50% zikaenda kwa Mwekezaji ambaye si lazima awe MO.
Heko Aveva na viongozi wote mmenikumbusha msemo wa Kiingereza unaosema "Something is better than nothing" (Yani kile kidogo ulicho nacho ni bora kuliko usichonacho) na wito wangu kwenu ni kuwaasa muendelee kutafuta wadhamini wengine kuipa nguvu Simba.
Klabu kubwa Ulaya hazina mwekezaji mmoja ni muda muafaka kwa klabu zetu kuacha kuuwategemea hawa matajiri lakini kutumia biashara zao kunufaika.
Simba kuingia mkataba na SPORTPESA hakumzuii Mohammed Dewji kuwa mmiliki wa Simba kwani klabu kama Manchester United wakati inaingia mkataba na makampuni makubwa kama CHERVELOT na ADIDAS haikuwazuia Familia ya Glazer kuendelea kuimiliki klabu hiyo tena wanapata faida kubwa sasa kutokana na mikataba hiyo.
Timu kama Simba leo inaweza kabisa kuingia mkataba mfano na kampuni ya Saruji ya Dangote kwaajili ya usafiri pekee, Bado wanaweza wakaingia mkataba mwingine na NSSF kwaajili ya ujenzi wa Uwanja pale Bunju lakini wakawa na zaidi ya wadhamini wawili katika jezi n.k. lakini bado wakawa na mmiliki kama MO ambaye naye atatoa mchango wake.
Sina hakika sana kuwa klabu kama Real Madrid zina wawekezaji mfano wa MO lakini klabu inajiendesha na kuongoza katika klabu zinazotengeneza faida, wao wanakua makini katika uchaguzi wa Rais wao kwani agenda kuu huwa ni jinsi gani Rais anaweza kuiongoza klabu kuweza kupata faida na vikombe na kuhakikisha Real inaendelea kupata wadhamini ndani na nje ya uwanja.
Wana Simba ni wakati wa kuwaaunga mkono viongozi wenu msifanye jambo hili kishabiki na kupoteza uhakika wa pesa katika mkataba wa Sportpesa. Pateni muda mwingi sasa kupitia vipengele vyote juu ya mkataba ambao MO anataka kuingia na Simba na pia wapeni muda viongozi wawaeleze kwanini wamesaini mkataba huu.
Kila la heri
Its me
EDO DC (Wapenda Soka Tanzania)
Kwa maoni na ushauri unaweza kuniandikia
Email: edodanieldc@gmail.com
Facebook & Instagram : @edodanielchibo
Twitter: @Edodaniel1
No comments