HATUNAYE TENA SHOSE FIDELIS.

Mwanachama wa Wapendasoka Tanzania ambaye ni shabiki mkubwa wa Simba na Man UTD amefariki katika ajali ya gari iliyotokea Morogoro akiwa njiani kutokea Dodoma kuishangilia timu yake ya Simba ambayo jana ilicheza mchezo wa fainali ya kombe la ASFC dhidi ya Mbao FC.


Katika gari ambalo limechukua uhai wa Shose, alikuwemo pia nahodha wa Simba Jonas Mkude pamoja na wanachama wengine wa Wapendasoka ambao ni Jasmine Mdoe na Faudhia Ramadhan ambao wao wamenusurika.

Shose atakumbukwa zaidi na Wapendasoka pamoja na mashabiki wa Manchester United Tanzania kutokana na ukaribu wake kwa makundi hayo maarufu ya soka nchini.

Akizungumza kwa uchungu jioni ya leo, C.E.O wa Wapendasoka Tanzania ambao ndiyo wamiliki wa tovuti hii ambaye alikuwepo pia kwenye msafara wa mashabiki wa Simba Aly Shatry amesema Faudhia na Jasmine wamenusurika kutokana na kufunga mikanda.

"Shose amefariki kweli, nimemuona akikata roho, ni huzuni lakini ndiyo imeshatokea. Faudhia na Jasmine wapo Hospitali Morogoro wanaendelea vizuri"

Akizungumzia pengo la Shose, Katibu Mkuu wa Wapendasoka, Richard Leonce alisema ni kubwa sana na halitozibika.

"Tulimsajili Shose miaka miwili iliyopita na amekua mwanachama hai wa taasisi yetu kwa kipindi chote, tutamkumbuka sana kwa upole na ushirikiano wake"

Kwa niaba ya idara ya habari ya Wapendasoka Tanzania, tunatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Shosesharuwa Fidelis.

"Bwana alitoa, bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe."

No comments

Powered by Blogger.