YANGA YAONYWA ABDI BANDA ASIMAMISHWA
Kamati ya Usimamizi na
Uendeshaji wa Ligi Tanzania au Kamati ya Saa 72, ilifanya kikao chake juzi
Ijumaa Aprili 7, 2017 jijini Dar es Salaam na kufikia uamuzi ufuatao.
Kuhusu kupulizwa dawa
vyumbani Uwanja wa Kambarage
Daktari wa Uwanja wa
Kambarage, Dk. Abel Kimuntu amekataa kuwasilisha taarifa yake kuhusu tuhuma za
kupuliziwa dawa kwenye chumba cha kubadilishia nguo cha timu ya Majimaji katika
mechi namba 170 ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya wenyeji Stand United. Klabu ya
Majimaji iliwasilisha malalamiko yake kwa Bodi ya Ligi kuhusu suala hilo.
Hivyo, Kamati imeagiza
suala la daktari huyo lipelekwe kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya hatua za kinidhamu dhidi yake kutokana na
kukataa kutoa ushirikiano kwa mwendeshaji wa Ligi juu ya jambo hilo. Kamati ya
Nidhamu inatarajiwa kukaa wakati wowote wiki ijayo.
Kuhusu Mchezaji Abdi
Banda
Mechi namba 194
(Kagera Sugar 2 vs Simba 1). Beki wa
Simba, Abdi Banda jezi namba 24 amesimamishwa kucheza Ligi Kuu wakati akisubiri
suala lake la kumpiga ngumi kiungo wa Kagera Sugar, George Kavilla jezi namba
15 wakati akiwa hana mpira kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu
ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Alifanya kitendo hicho
ambacho hakikuonwa na waamuzi katika mechi hiyo iliyofanyika Aprili 2, 2017
kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Uamuzi wa Kamati umezingatia Kanuni ya
9(5) ya Ligi Kuu.
Pia Kamati ilibaini kuwa
Banda alifanya kitendo cha aina hiyo kwenye mechi namba 169 kati ya Simba na Yanga
iliyofanyika Februari 25, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Awali, Klabu ya Kagera
Sugar iliwasilisha malalamiko dhidi ya kitendo cha beki wa Simba, Abdi Banda
kumpiga ngumi kiungo wao George Kavilla wakati akiwa hana mpira, na Mwamuzi wa
mechi hiyo kutochukua hatua yoyote.
Kwa vile kosa hilo ni la
kinidhamu, Kamati imemsimamisha Abdi Banda kwa mujibu wa Kanuni ya 9(5) wakati
akisubiri suala lake kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Kamati ya Nidhamu inatarajiwa
kukaa wakati wowote wiki ijayo.
Kadhalika Klabu ya Simba
iliwasilisha malalamiko ikitaka ipewe ushindi wa pointi
tatu na mabao matatu
kutokana na timu ya Kagera Sugar kumchezesha mchezaji Mohamed Fakhi Gharib
wakati akiwa na kadi tatu za njano katika mechi yao namba 194 iliyofanyika
Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Kamati baada ya kupitia
malalamiko hayo, imeahirisha shauri hilo hadi Alhamisi Aprili 13, 2017 kwa vile
bado inafuatilia baadhi ya vielelezo kuhusu malalamiko hayo kabla ya kufanya
uamuzi.
Mechi namba 195 (Yanga
1 vs Azam 0). Yanga haikuingia kwenye
chumba chake cha kubadilishia nguo, kutokana na kuwa na maji yaliyomwagwa na
wanachama wa klabu hiyo (makomandoo) muda mfupi kabla ya timu hiyo kuwasili
uwanjani.
Kamati imeelekeza klabu
ya Yanga iandikiwe barua ya onyo, na kuitaka kuhakikisha wanachama wake
wanaacha mara moja mtindo wa kumwaga maji vyumbani baada ya kuwa vimeshafanyiwa
usafi na wafanyakazi wa uwanja tayari kwa ajili ya matumizi ya timu yao.
Mechi namba 200
(Majimaji 4 vs Toto Africans 1). Katika
mechi hiyo, timu ya Toto Africans ilifanyiwa vurugu ikiwa njiani kurejea
hotelini baada ya mechi hiyo ambapo viongozi wake wawili waliumizwa. Tukio hilo
liliripotiwa Kituo cha Polisi, na kesi tayari iko kortini.
Kituo cha Songea (Uwanja
wa Majimaji) kiandikiwe barua ya kuhakikisha hazitokei vurugu uwanjani hapo
baada ya mechi ikiwemo kuhakikisha timu ngeni inatoka uwanjani salama hadi
kwenye hoteli ilikofikia. Iwapo vurugu zitaendelea, Bodi ya Ligi itasimamisha
matumizi ya kituo hicho kama ilivyoainishwa katika Kanuni ya 9(2) ya Ligi Kuu.
KUPITIA MATUKIO YA
LIGI DARAJA LA PILI (SDL Play Off)
Mechi namba 7 (Mawenzi
Market 2 vs Transit Camp 0). Klabu ya
Transit Camp imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) baada ya timu yake
kuchelewa uwanjani kwa dakika 45 katika mechi hiyo iliyochezwa Machi 18, 2017
katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Adhabu dhidi ya Transit Camp imetolewa
kwa kuzingatia Kanuni ya 14(1) na 14(47) kuhusu Taratibu za Mchezo.
Kocha Msaidizi wa Transit
Camp, Thomas Gama amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 (laki
tatu) baada ya kutolewa nje na Mwamuzi katika mchezo kutokana na kumtolea
maneno ya kashfa Mwamuzi Msaidizi Namba Moja.
Mechi namba 8 (JKT
Oljoro 1 vs Cosmopolitan 0). Klabu ya
Cosmopolitan iliwasilisha malalamiko kuwa mechi hiyo iliyofanyika Machi 20,2017
kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha
ilichezeshwa na Mwamuzi wa Arusha, badala ya Mwamuzi kutoka Singida aliyekuwa
amepangwa awali.
Kamati imetupa malalamiko
hayo kwa vile si ya kweli, na Mwamuzi aliyechezesha mechi hiyo alitoka Mkoa wa
Manyara, na si Arusha kama walivyodai katika malalamiko yao.
Mechi namba 12
(Transit Camp 1 vs Cosmopolitan 1).
Daktari wa Cosmopolitan, Najim Mtoro amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya
sh. 300,000 (laki tatu) baada ya kutolewa kwenye benchi la ufundi kwa kosa la
kumtukana Mwamuzi wa Akiba.
No comments