KICHUYA AIBUKA SHUJAA WAKATI WATU 10 SIMBA WAKIIANGAMIZA YANGA TAIFA
![]() |
| Shiza Kichuya akishangilia bao la ushindi |
Kichuya mshambuliaji anayeichezea Simba msimu wake wa kwanza akitokea Mtibwa Sugar aliingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya beki Norvat Lufunga ambaye alionekana kabisa kushindwa kuwamudu washambuliaji wenye uchu na kasi wa Yanga.
Dakika ya 5 tu ya mchezo Mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia Obrey Chirwa alimzidi ujanja beki Norvart Lufunga ambaye alishindwa kuokoa mpira na kutaka kumiliki mpira huku mpira ukamshinda na ndipo Chirwa alipouwahi na kumzunguka beki huyo ambaye alishindwa kumzuia kwa usahihi na kusababisha penati iliyofungwa na Simon Msuva.
Kipindi cha kwanza kikaonekana kutawaliwa vyema na Yanga huku mipira ikishindwa kusogea mbele kwa upande wa Simba hali iliyopelekea kocha wa Simba Joseph Omog kumtoa Juma Luizio na kumwingiza Said Hamis Ndemla ambaye alibadilisha kabisa hali ya mchezo lakini mpaka mapumziko Yanga walikua mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa mkosi kwa Simba baada ya beki wake Janvier Bokungu kutolewa kwa kadi nyekundu akimchezea madhambi Chirwa ambaye alikua akielekea kufunga. Bokungu alirudi kucheza beki wa kati huku Mzamiru Yasin akicheza pembeni baada ya kuingia Shiza Kichuya
Dakika ya 66 kazi nzuri ya Shiza Kichuya aliyepokea pasi ya Ndemla na kuambaa nayo katika winga na kupiga krosi iliyotua katika kichwa cha Laudit Mavugo aliyefunga kwa urahisi na kumwacha kipa wa Yanga Deo Munishi akiwa hana la kufanya.
Bao hilo liliongeza kasi kwa Simba ambayo ilionekana kufufuka na kucheza vyema zaidi hasa baada ya kuingia Jonas Mkude aliyeingia kuchukua nafasi ya Mohamed Ibrahim na kumfanya James Kotei kurudi kucheza nafasi ya ulinzi huku kwa Upande wa Yanga wao walimpoteza mchezaji wao Kamusoko dakika za mwisho za kipindi cha kwanza baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Said Juma.
Shiza Kichuya aliwanyamazisha kabisa Yanga dakika ya 81 akifunga bao la pili akipiga mpira umbali wa mita 23 na kumshinda kipa Deo Munishi wa Yanga.
Kwa matokeo hayo Simba sasa imefikisha pointi 54 ikiendelea kushika uongozi wa ligi huku Yanga wakibaki na pointi 49 katika nafasi ya pili.

No comments