HII NI NAFASI KUBWA KWA ARSENE WENGER KUFUTA UTEJA DHIDI YA MOURINHO NA MANCHESTER UNITED.


Na Frank Lelo

Jumamosi ya tarehe 19 mwezi septemba 2016, mida ya saa tano na nusu asubuhi Jijini Manchester, Uingereza na saa tisa na nusu alasiri saa za Afrika mashariki, Manchester united itaikaribisha Arsenal kwenye mechi ya Ligi kuu ya uingereza mzunguko wa 12.

Hii daima ni mechi kubwa. Ikitaliwa na matukio ya kuchekesha, kuvutia na  matukio ya kibabe kwa miaka ya hapo nyuma kidogo. Lakini inaweza kua na makali zaidi hivi sasa kwa sababu ya uwepo wa makocha hawa wawili, Jose Mourinho na Arsene Wenger ambao wamekua na upinzani wa ndani na nje ya uwanja kwa miaka ya hivi karibuni.

Kihistoria, kwa miaka mingi kuanzia miaka ya mwishoni ya 1980's ligi ya uingerera ilikua ikitawaliwa na Manchester united na Arsenal. Kabla ya hapo upinzani ulikua kwa Manchester united na Liverpool.

Kocha George Graham wa aliyeanza kuifundisha Arsenal mwaka 1987 nae aliongeza ushindani lakini aliachishwa kazi mwaka 1994.

Lakini uhasama wa Manchester united na Arsenal ulipamba moto zaidi alipowasili Uingereza Mfaransa Arsene Wenger mwaka 1996 kipindi ambacho Liverpool ilikua imepungua makali kuanzia miaka ya mwanzoni ya 1990's na kuendelea.

Manchester united walikua wakitawala ligi hiyo kwa kutwaa mataji mengi zaidi chini ya Sir Alex Ferguson.

Lakini yote haya yalibadilika baada ya kuwasili kwa mfaransa Arsene Wenger. Alibadilisha tamaduni nyingi za soka nchini Uingereza kama aina ya  vyakula na vinywaji wanavyotumia wachezaji, ufanyaji wa mazoezi n.k

Lakini kubwa, alipunguza utamaduni wa Manchester United kutawala ligi hiyo. Alipofika tu moja kwa moja alishika nafasi ya tatu na msimu uliofata alinyakua ubingwa wa ligi kuu ya Uingereza. Alex Ferguson alipata mpinzani na uhasama ulipamba moto zaidi miaka ya mwanzoni ya 2000.

Kwa sababu mbali mbali ambazo hatutaziongela kwenye makala hii, kuanzia mwaka 2004 alipowasili Jose Mourinho na bilionea wa Kirusi Roman Abramovich Chelsea, rekodi ya klabu ya Arsenal chini ya Arsene Wenger dhidi ya vilabu vikubwa Uingereza hususani Manchester united na Chelsea imekua siyo nzuri.

Tangu mwaka 2006, Arsenal imeifunga Manchester United mechi 3 tu. Huku ikishinda mechi 1 tu katika uwanja wa Old Trafford kwenye mechi za ligi kuu ya Uingereza.

Rekodi ya Arsene Wenger dhidi ya Jose Mourinho ambae ndie kocha mkuu wa Manchester united hivi sasa ni mbaya na haitamanishi kwa mashabiki wa Arsenal.

Arsene Wenger hajawahi kumfunga Jose Mourinho katika mechi 13 za ushindani tangu timu zao zianze kukutana mwaka 2004. Alifanikiwa kumfunga Jose Mourinho mwaka 2015 mwezi August kwenye mechi ya ngao ya hisani. Arsenal ikishinda 1-0 dhidi ya Chelsea.

Ngao ya hisani au ngao ya jamii sio taji lenye uzito mkubwa sana kwenye ramani ya soka ulaya na hata Uingereza hasa zama hizi za miaka ya karibuni tofauti na enzi za  zamani. Hivyo Arsene Wenger anayo kazi jumamosi ya kuuonesha ulimwengu wa soka kuwa yeye si mtaalamu wa kufeli kama Jose Mourinho alivyomuita mwaka 2014.


Mechi hii itakayochezwa jumamosi ni fursa kubwa kwa Wenger kufuta rekodi hiyo mbovu dhidi ya Mourinho na Manchester United.

 Arsenal tangu ilipopoteza mechi ya ufunguzi wa ligi dhidi ya Liverpool haijapoteza mechi yoyote tena.
Mechi ya mwisho waliyotoa sare dhidi ya Tottenham ilikua mechi ya 16 mfululizo bila kupoteza katika mashindano yote.

Arsenal ina wachezaji kama Granit Xhaka na Shkodran Mustafi ambao wamesajiliwa hivi karibuni na wamekua msaada mkubwa msimu huu.

Wasiwasi wa Arsenal upo kwa mfungaji wao bora msimu huu Alexis Sanchez ambae anatoka Chile kukiwa na wasiwasi wa afya yake, Hector Bellerin akipata majeraha yatakayomweka nje kwa wiki 4 na kiungo muhimu Santi Carzola akiwa na majeraha yasiyojulikana yatapona lini.

Kwa upande wa Manchester United pamoja na kufanya usajili mkubwa kwa kununua wachezaji wenye majina makubwa kama Paul Pogba na Zlatan Ibrahimovic  hali bado si shwari sana. Walianza ligi vizuri lakini mechi za hivi karibuni wamekua wakipata matokea ya aina tofauti tofauti.

Jose Mourinho pia inaonekana bado hajajua ni kipi kikosi chake bora cha kuanzia mechi, akichezesha wachezaji tofauti tofauti katika mechi tofauti tofauti kwa sababu za majeraha n.k

Mshambuliaji Zlatan Ibrahimovic ataikosa mechi hiyo akiwa amefungiwa mechi moja baada kupata kadi 5 za njano msimu huu huku mabeki wa kati Eric Bailly, Chris Smalling na beki wa kulia Antonio Valencia wote wakiuguza majeraha.

Pia kuna mashaka ya kushiriki mechi hii kwa  kiungo Marouane Fellaini aliyeumia akiwa na timu ya taifa ya Ubelgiji  na beki wa kushoto Luke Shaw ambae inasemekana alipishana kauli na Jose Mourinho.

Kukosekana kwa Zlatan Ibrahimovic kutampa Marcus Rashford nafasi ya kuhamia nafasi yake ya asili kama mshambuliaji wa kati, akiwa ndiyo mchezaji aliewaletea Arsenal madhara mara ya mwisho walipocheza Old trafford akifunga magoli mawili.

Umati wa Old Trafford watatarajia vijana wa Mourinho kuanza mechi iyo kwa kushambulia na hii inaweza kuwakidhi Arsenal wakicheza kwa mchezo wa kushambulia kwa kushtukiza wakiwatumia wachezaji kama Alexis Sanchez na Theo Walcott.

Arsenal ina wachezaji wenye kasi ambayo inaweza kuwaletea matatizo beki ya Manchester United.
Kama Wenger atafanikiwa  kushinda mechi ya kwanza ya ushindani dhidi ya Mourinho, mashabiki wa Arsenal wanaweza  kuanza kuamini huu ni mwaka wao. Kazi kwao vijana wa Arsene Wenger.

No comments

Powered by Blogger.