EUROPA LEAGUE : MECHI ZA UGENINI ZAENDELEA KUITESA MAN UNITED, GENK YA SAMATTA YALIZWA NA BILBAO

Klabu ya Manchester United imeendelea kufanya vibaya katika mechi zake za ugenini katika Michuano ya Europa League baada ya kukubali kichapo cha bao 2-1 toka kwa Fenebahce ya Uturuki.


United iliyosafiri mpaka katika jiji la Instabul ilijikuta ikifungwa bao la mapema sekunde kadhaa baada ya mechi kuanza likifungwa na Mshambuliaji Moussa Sow kwa tikitaka akiunganisha mpira wa krosi ya Hassan Alli.

Mpaka mapumziko United walikua nyuma kwa bao hilo moja na dakika ya 59 Fenebahce walipata bao la pili kwa mpira wa adhabu ndogo ukipigwa na Jeremain Lens na kupita ukuta wa United huku kipa David De Gea asijue la kufanya.

Nahodha Wa United Wayne Rooney baada ya mechi 11 bila kufunga jana aliondoa mkosi akifunga bao pekee la United katika mechi hiyo dakika za majeruhi kwa shuti la umbali wa nje ya box baada ya Safu ya ulinzi ya Fenebahce kuwazuia kabisa washambuliaji wa United kufurukuta.

Kwa matokeo hayo United imebaki na pointi 6 katika kundi lake huku Fenebahce na Feyernood wakiwa na pointi 7

Katika moja ya mechi nyingi za jana ni ile ya Athletico Bilbao waliokua wakicheza dhidi ya Genk ya Mbwana Samatta na mpaka mwisho wa mchezo Genk walikubali kichapo cha bao 5-3.

Katika mchezo huo uliopigwa nchini Spain Mbwana Samatta alikua mmoja wa wachezaji walioanza katika kikosi cha Genk akicheza kama mshambuliaji wa kati japo hakufunga bao lolote.

No comments

Powered by Blogger.