WAYNE ROONEY, UINGEREZA NI YA WOTE NA NI YAKO PEKE YAKO.
Uingereza ni nchi ya watu wanaojipenda sana. Nchi ya watu wanaoamini kuwa Mwenyezi Mungu alitangulia kuumba nchi yao kisha zikafuata nyingine. Nchi ambayo watu wake wanaamini walibarikiwa kabla ya wengine wote.
Hii ni nchi ambayo kila inachozalisha inaamini kuwa ni bora kuliko kwingine kokote kule.Hii ndiyo namna inayowafanya kuwa wa kipekee na inayowafanya siku zote kuwekwa kwenye mazungumzo ya kila kilichokuwa bora, iwe watu, bidhaa mpaka michezo.
Katika hili Waingereza hawakuwahi kuwa na ndugu wa kudumu. Watakupenda leo kesho watakuchukia, watakushangilia asubuhi jioni watakuzomea na hata katika jua watacheka nawe lakini giza likitanda watakuchoma. Rafiki yao kila kukicha ni yule ambaye anayefanya vyema kwa wakati huo na kuwafanya kutembea vifua vikiwa mbele, wakimtisha kila aliyekuwa mbele yao na wala asiwepo ambaye atawapa shida.
Kwao Walcott alikuwa mchezaji ambaye alitakiwa kuvaa jezi ya David Beckham kabla hata ajastaafu huku akijitwalia namba yake uwanjani jumla. Kwao wao Ross Barkley aliwapa kiburi cha kuwasahau Steven Gerrard pamoja na Frank Lampard. Ndiyo ni hawa Waingereza ambao katika maisha yao kwenye soka Waliwahi kupatia ama kuwa na uamuzi sahihi mara moja pekee.
Walipatia kipindi ambacho waliamua kumpa sanamu mchezaji na nahodha wa Taifa lao Bobby Moore ambaye ndiye aliyewaongoza kutwaa ubingwa wa Dunia. Huyu waliweka sanamu yake nje ya ule uwanja wao mkubwa wa Wembley.
Baada ya kuwa na kizazi cha dhahabu kwa muda ambao waliishi Paul Scholes, David Beckham, Steven Gerrard pamoja na akina Ashley Cole, wazazi nchini mwao hawakuzalisha tena vipaji vya kutisha. Bahati nzuri pekee waliyoipata ni kuwa ndani ya kizazi hicho cha dhahabu alikuwemo kinda aliyeitwa Wayne Rooney.
Huyu ambaye aliwanyanyua vitini mashabiki wakati akiwa na umri wa miaka 16, akiwamaliza Arsenal na Wenger kwa goli la mtu mzima. Ni huyu huyu ambaye makali alikwenda kuyahamishia kwenye michuano ya Euro mpaka pale walipotokwa na machozi baada ya kupata majeraha na Uingereza kutolewa na Ureno.
Huyu pia ambaye amesimama kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Taifa hilo. Ni huyu Rooney pia ambaye kwa sasa anaishi katika jalala ndani ya Uingereza yaani amekuwa takataka. Hakuna anayempenda na wala hakuna anayekumbuka na wala hakuna ambaye anakumbuka kuwa rekodi zake zimepigwa muhuri wa moto.
Waingereza hawamtaki tena na kila jumba bovu linaangukia mgongoni kwake kwa sababu ya kuwa na kiwango ambacho sio chake ama kile walichokizoea. Bahati mbaya kwa Rooney ni kuwa anazeeka katika kikosi kibovu cha Waingereza. Mvi zinamkuta katika kikosi ambacho Jordan Henderson ndiye staa wa eneo la kiungo huku pia Dele Alli akiwa ndiye mchezaji wao mbunifu zaidi.
Rooney kwake hakuibuka hivi, aliibuka huku akiziba mapengo ya akina Michael Owen. Aliibuka kipindi ambacho Uingereza ilikuwa imetimia. Sasa hivi hawa makinda akina Sterling wamekuta hakuna akina Wayne Rooney japo 5 kikosini. Wamekuta kuna mgonjwa Daniel Sturridge ndiye anayemtua mzigo Rooney na wamemtangulia Vardy kikosini hivyo hana cha kuwaeleza kwa sababu wanamzidi ukongwe ndani ya kikosi hicho.
Bahati nzuri pekee ya Rooney ni kuwa kwa wakati huu ambao vyombo vya habari vinamuandama ni nadra sana kwa timu hiyo kufanya vyema aidha awemo au asiwemo kikosini. Hawana kizazi cha kutisha kama zilivyo nchi nyingine. Ni kipindi hiki ambacho ndicho kinamfanya Rooney awe mbovu zaidi kwa sababu hana mchezaji ambaye anaweza kugawana naye presha ndani ya uwanja.
Mashabiki wanamtizama yeye kama mchezaji mkongwe zaidi, anapewa majukumu mapya ya kuwa kiungo eneo ambalo amelicheza mara chache zaidi katika maisha yake ya Soka na kisha mashabiki wanahitaji miguu yake ilete matokeo.
Ni ngumu kwa Rooney wa sasa kufanya kile ambacho wengi wanataka afanye. Uwezo wake umeshuka lakini haujamalizika. Waingereza wanahitaji ambacho Rooney hawezi kuwapa na bahati mbaya zaidi ni kuwa hata kwenye benchi hakuna mchezaji anayeweza kutoa kile ambacho Rooney alizoea kuwapa muda mrefu wa maisha yake.
Waingereza hawawezi kubadilika. Wameishi hivi kwa miaka mingi, wameishi kinafiki miaka nenda rudi. Waliwahi kumsahau Ashley Cole, wakawahi kumtenga Beckham na hata kuna nyakati walipiga kelele kwa Steven Gerrard, japo sio kwa kiasi hiki cha chuki kwa Rooney.
Hasira zimejaa mioyoni mwao, sifa zao zinawasukuma kuishi hivi na bahati mbaya ni kuwa hawana kikosi cha kuwafanya waishi kwa starehe tena. Pole Wayne Rooney, ukifanya vyema timu hii lazima iwe wenu wote na ukifanya vibaya mzigo ni wako peke yako na inakuwa timu yako mwenyewe. Ukiona hawana adabu enenda zako tu, ingawa umri wako mdogo. Wanaye yule Rashford kwa sasa, hawezi kuvaa viatu vyako lakini kawapa kiburi tayari.
Nicasius Nicholaus Agwanda (Coutinho Suso).
No comments