WANACHAMA WANAODAIWA ADA MARUFUKU JUMAPILI ~ MANJI

Mwenyekiti wa Yanga Yusuph Manji amewaonya wanachama wanaodaiwa ada kutosogelea mkutano wa Yanga Jumapili hii.



Manji ameyasema hayo mchana huu wakati akiongea na waandishi wa habari katika ofisi yake iliyoko makao makuu ya klabu hiyo Jangwani Dar es Salaam.

Manji alitumia fursa hiyo kufikisha ujumbe kwa wanachama wa Yanga na kuwaasa kuhudhuria mkutano huo wa dharula siku ya Jumapili, mkutano utakaofanyika katika uwanja wa Kaunda Yalipo makao makuu ya klabu hiyo.

Aidha Manji amewataka wanachama kufika kwenye mkutano huo na wanaruhusiwa kuuliza chochote bila kuogopa kwa maslahi ya Yanga na kusisitiza ulinzi utakuwepo wa kutosha ila mwanachama ambaye hujalipia ada kwa miezi sita hutoruhusiwa kuingia kwenye mkutano huo muhimu kwa mustakabali wa klabu hiyo kongwe hapa nchini.

Aidha mwenyekiti amesema katika mkutano huo yeye baada ya kuzungumza mambo yake atatoka nje ili wanachama wapate uhuru wa kujadili na kutolea uamuzi.

"Nawaomba wanachama wa Yanga wajitokeze kwa wingi kwenye mkutano mkuu Jumapili waweze kuchangia masuala ya msingi kwa maendeleo ya klabu yao"

"Ndani ya siku 90 baada ya kupewa ridhaa ya wanachama, tutaanza ujenzi wa uwanja wa mazoezi kwa timu" Alisema Manji.

Yanga itakua na mkutano wake huo mkuu wa dharula agenda kubwa ikiwa ni mabadiliko katika klabu hiyo huku Yusuf Manji kupitia kampuni ya Yanga Yetu akitaka kukodishwa klabu hiyo kwa miaka 10.

No comments

Powered by Blogger.