TFF MNAJUA KIINI CHA TATIZO LA MAREFA NCHINI , MAREFA JE?.

Na Mandala J.

USIOMBE  ikuguse na kukumbusha kuwa nawe ni mmoja wa watu waliochangia na kukuza matatizo ya kuchezesha vibaya michezo ya Ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara( VPL) na Ligi zingine zilizochini ya TFF.



Leo naomba nisiongelee kuhusu mchezo wa YANGA na SIMBA kimchezo maana iko wazi kuwa upenzi na ushabiki umeendeleza uongo wa kuonyesha kutojua kanuni na maana ya mchezo wa soka hapa  nchini. Kuna vitu vingi vidogo vidogo vimekuzwa na kufanya mambo ya soka kuonekana si mambo mazuri na mema michezoni. Kimchezo March 31, 2002 Madaraka Selemani alifunga goli upande wa goli la Kusini sehemu ambayo SIMBA hukaa na likashangiliwa kwa nguvu sana , lilikuwa goli baada ya kuutengeneza mpira kwa mkono na kupiga shuti lililoenda nyavuni moja kwa moja, ni tofauti na Amissi Joselyn Tambwe aliefunga goli upande uleule wa goli baada ya mpira kugusa mkono na kutengenezwa katika himaya lakini likapokelewa na mashabiki wa SIMBA kama ni uonevu mkubwa na ukandamizaji uliopitiliza, hawa ndio wale walioshangila la mkono la Madaraka Selemani  wakamua kung'oa viti vya uwanja kuonesha hasira na kutokukubaliana na maamuzi ya refa. Magoli haya mawili kwangu yanabakia kuwa magoli bora yaliofungwa na washambuliaji wenye nidhamu ya nidhamu ya kufuata kanuni za ushambuliaji na kufunga na hongera yao kwa kutimiza wajibu wao na katika hili marefa  ilikuwa haiwahusu kabisa.

Uchezeshaji wa Mpira wa miguu ni fani ya taaluma ya busara ya imani ya uaminifu na ujuaji na uendelezaji wa Mpira wa miguu na kinyume ya hapo ni uzoroteshwaji na uuwaji wa Mpira wa miguu Tanzania.

Tatizo la uchezeshaji mbovu ni kubwa na limeendelea kutesa ushiriki wa timu zetu katika michuano ya kimataifa na kurudisha maendeleo ya Mpira wetu hapa Tanzania ni Mara nyingi mazoea ya uchezeshaji mbovu katika hali ya kubebana yamewahadhibu wachezaji wetu dhidi ya marefa wa nje katika mashindano ya kimataifa kwenye timu ya Taifa au Timu ya VPL inapowakilisha ligi hiyo.

Ukiangalia kwa undani tatizo kubwa limeanzia katika ushabiki wa vilabu vya SIMBA na YANGA kwa maana ya kwamba kila Mtanzania anaependa Mpira wa miguu ana upande wa SIMBA au YANGA hata viongozi nao wa Vyama vya Mpira ni hivyo hivyo kwa madhara haya ya kimfumo na kiasili.

Mashabiki na ushabiki ndio kiini kikubwa maana wao bila kuangalia uwekezaji na kiwango cha timu yao huhitaji matokeo ya ushindi tu hata kama timu yao ni mbovu ili mradi iwe ni SIMBA au YANGA, huu ndio mfumo uliopo na ulishajengeka na kibaya ni utani wa kishabiki baada ya timu mmoja wapo kupata matokeo mabovu. Hili limepelekea viongozi wa vilabu kujua siri yao ya kuongoza timu mbele ya wanachama na mashabiki wao kuwa njia rahisi ya kukubalika ni kupata ushindi kwa njia yoyote maana mashabiki wanataka matokeo kwa njia yoyote ili mradi timu yao SIMBA au YANGA ishinde.

Katika hili kibaya zaidi wale viongozi ambao huongoza timu hizi kwa wakati huo huwa wanatafuta matokeo ya timu yao kwa njia yoyote ndio viongozi wa kamati mbalimbali za TFF au aliekuwa kiongozi wa timu hizi wakati ule na alikuwa anatafuta matokeo kwa njia yoyote ile ili kuwaridhisha mashabiki ndio kiongozi wa TFF wa sasa au kamati ya TFF tatizo kubwa hapa ni mahaba na ushabiki na mara ngapi unasikia haa sisi ni zaidi ya Tp Mazembe au timu ya Taifa ya Tanzania itawatoa Algeria ya akina Mahrez na tutawafunga  huu ndio kiini cha marefa wabovu kuwa unajua uwezo wa timu lakini unahitaji matokeo vyovyote vile. TUSAHAU KABISA MAFANIKIO YA KIHIVYO.

USHABIKI unabakia kuwa kiini kikubwa kilichochangiwa na ushabiki wa marefa wetu juu ya hizi timu na ni Mara nyingi utasikia haa yule refa ni Yanga au utasikia yule refa ni Simba na wengine ni wanachama kabisa wa hivi vilabu hili ni tatizo mama.
Tatizo lingine kubwa ni marefa wenyewe kukosa utashi na uelewa mpana wa mahitaji sahihi ya kazi yao na ya wengine kwa ujumla na hili limesababisha wao kuchukua rushwa kwa kuendekeza ubinafsi na rejea kashfa ya upangaji wa matokeo ya michezo ya mwisho ya kupanda LIGI KUU. 
Suala la ubinafsi hasa umimi umechangia kwa kiasi kikubwa uchezeshaji mbaya maana katika vikao vya maamuzi vya marefa unakutana na viongozi wale wale MASHABIKI WA SIMBA AU YANGA angalia mfano wa kikao cha kamati ya masaa 72 angalia washiriki wake ni mashabiki na wengine wanachama wa vilabu hivi hapa sisemi kuwa wao ndio wahusika ila tuangalie muundo wa kamati hizi na wajumbe wake wanatokana na nn? Hitaji la mashabiki wao ni nini walikotoka na wanasimamia nini? Au nini kwanza kwao katika uwakilishi wao yaani timu yao au Mpira?  Na Mara nyingi utanielewa pale wanapoamua demokrasia ndio itumike kufanya maamuzi ya kamati. Hoja kubwa hapa ni uwakilishi wao ni uwakilishi wa mashabiki wao na lengo la mashabiki wao ni matokeo na ili waendelee kuthaminiwa ni timu yao ipate hitaji lao bila kuangalia mahitaji ya ukuaji wa Mpira.

Suala lingine ni hatua za marefa hawa hupitia mpaka kufika kuchezesha ligi kuu ni ndogo na muda mdogo usiotoa uzoefu wa kutosha kufanya kuwa na uwezo wa kuchezesha mchezo wenye ushindani mkubwa, hebu fananisha na waliotutangulia kama England refa anaechezesha akina Mark Clattenburg , Mike Dean pale unapowaona wamepitia  ngazi saba ambazo humfanya kuwa na uzoefu wa akili timamu kumudu michezo yote yenye ushindani mkubwa sana japo makosa ya kibinadamu katika Mpira hayakosekani, tusisahau pia  kiasi cha malipo wanayolipwa marefa haviendani na wanachozalisha ndani ya  dakika 90 au 120.

Marefa ni moja ya rasilimali kubwa inayotumika kuvuna pesa nyingi kutoka kwa mashabiki na vyanzo vingine kama utangazaji na biashara  maana wao ndio wafanikishaji wa bidhaa inayouzwa sokoni.

Hebu angalia mchezo wa Yanga na Simba wa juzi uliingiza zaidi ya tsh 400m lakini wale akina Ferdinand Chacha, Samwel Mpenzu na Martin Saanya nina uhakika haikufika hata 1m kwa  kila mwamuzi.Hili huwezi kuliona kwa urahisi ila ni  tatizo kubwa sana kisaikolojia katika utendaji maana hata moja ya kumi haijafika kwa mwamuzi kwa anachozalisha. Mi naona kabisa marefa wakilipwa vizuri na kupewa usafiri mzuri watakuwa na thamani ya kutokurubunika na watachezesha Mpira vizuri sana.

Marefa pia wajue kuwa kufanya kwao vibaya ni kutokana na hitaji kubwa la matokeo la mashabiki na wakijua hilo wajue kuwa ni wao wenye mamlaka ya kuaharibu Mpira wa miguu au kuboresha mpira na kuachana na mambo yote yanayofikisha huko.
Uwekezaji katika suala la marefa hapa kwetu hakuna na ukijiuliza tunawatoa katika maisha yapi na katika nidhamu ya elimu ya Mpira ipi? Hili nalo ni tatizo pia.

NINI KIFANYIKE.

Kwangu Mimi kuwafungia waamuzi sio suluhisho la tatizo hili ila ni mashabiki kuwa na elimu sahihi ya sheria za Mpira na mazingira ya Mpira na hasa kujitambua maana sidhani kuvunja viti au kumpiga mwamuzi ndio suluhisho ya maamuzi mabovu. 

Chukulia mfano wa goli la Amiss Tambwe na goli la Laurent Koscienly dhidi ya Burnley na maamuzi ya marefa na sheria ya Mpira, mashabiki waangalie timu zao zinauwezo kiasi gani wasizitwishe timu uwezo ambao timu zao hazina na kutengeneza mwanya wa viongozi kutafuta matokeo .

Kamati za ligi na zile za makocha kuwa kamati huru zisizohusisha viongozi wa klabu na vilabu waliopo au waliopita ila kuwepo na watu waliocheza mpira pia katika kamati hizo .

Uwekezaji ufanywe kimaadili katika upatikanaji wa marefa hasa watumiwe wale walioajiriwa katika sekta za serikali na kanuni zihusishe uwajibikaji wao katika utumishi wao ili kupunguza mianya inayoonekana kuwa na rushwa.

Kuwepo na Sera ya Mpira Tanzania inayofanya Kazi kwa wakati wote kimalengo na sio kila mtu kuja na aina yake ya ujuzi katika utawala ili kupata mwendelezo wa upangaji wa mafanikio na si vinginevyo, ili alipoishia aliepita ndipo aanzie aneingia.
Mfano , alipoishia Tenga ndipo angeanzia Jamal Malinzi na ukiangalia mwendelezo wa matumizi ya Kim Poulsen kama kocha yangeendelezwa tungekuwa mbali kimwendo.

Semina endelevu za uadilifu na utumiaji wa kanuni 17 za mchezo katika uchezeshaji Mpira ziwe za Mara kwa Mara zikiambatana na malipo sahihi kulingana na uzalishaji na iwekwe katika asilimia.

Waamuzi wajue kwa utambuzi wa nafsi kuwa wao ndio chanzo pia cha tatizo la marefa na waelimishwe na kujielimisha kuwa madhara ya Kazi yao ni makubwa kuliko kitendo chao cha kupokea rushwa na kuchezesha mpira vibaya na TFF ndio wawe wasimamizi wakubwa wakuibua marefa wazuri na kuwatengenezea mazingira ya uaminifu ya uadilifu na nidhamu ya Mpira pia.

"... TUMESIKIA UMEPEWA PESA NA TIMU PINZANI , SISI HATUNA HIYO PESA ILA CHUKUA HII CHEZESHA FAIR....".

Ahsanteni.
0717-713403.

No comments

Powered by Blogger.