MIWANI PANA : SITETEI MASHABIKI KUVUNJA VITI,LAKINI AINA HII YA MAREFA KUNA SIKU ITALETA MAAFA KWA TAIFA.

Pambano la watani jadi Simba na Yanga ni moja kati ya matukio makubwa kuweza kukusanya watu wengi kwa wakati mmoja pengine kuliko tukio lolote lile hapa nchini.



Hakuna sehemu yeyote ambayo inatakiwa kuangaliwa kwa umakini linapokuja swala la usalama kama katika mechi hii kwani kwa wingi watu likitokea jambo lolote baya basi utakua msiba mkubwa sana kwa taifa.

Juzi katika pambano la Watani hao wa jadi katika uwanja mkuu wa Taifa jijini Dar es Salaam kulitokea mambo ambayo ni hatari kwa mustakabali wa maisha ya watu.

Kwanza utaratibu wa kuingia uwanjani haukuwa rafiki sana kwa Mashabiki baada ya msongamano mkubwa hali iliyopelekea kuvunjwa kwa geti watu wakilazimisha kuingia uwanjani lakini kibaya zaidi ni lile tukio la dakika ya 26 ya mchezo wakati Amiss Tambwe wa Yanga alipoifungia goli timu yake goli ambalo lililalamikiwa na mashabiki wa Simba kwamba mfungaji alikua ameushika mpira kabla ya kufunga baadae nahodha wa Simba Jonas Mkude akalimwa kadi nyekundu na mwamuzi wa mchezo huo.

Baada ya tukio hilo Taifa la Tanzania na dunia nzima ilishuhudia hasira za mashabiki wa soka wanaodhaniwa ni mashabiki wa klabu ya Simba waking'oa viti vya uwanja wa taifa na kuvirusha uwanjani kuonyesha kuchukizwa na kitendo cha refa huyo.

Mengi yamezungumzwa hasa kuwalaumu mashabiki waliofanya vitendo vile nami naungana na Wapenda Soka wengine wote kulaani vitendo vya uvunjifu wa amani wa namna ile na kamwe haviwezi kuvumilika kwani madhara yake ni makubwa leo imekua kung'oa viti lakini kesho yanaweza kuwa makubwa zaidi.

Lakini wakati tunakemea vitendo vya namna hiyo tunapaswa pia kujiuliza nini hasa chanzo cha mambo yote hayo nami kwa mtazamo wangu kwanza ukianzia na tukio la kuvunja geti ni kukosekana kwa usalama wa kutosha na kushindwa kujipanga hasa kwa zoezi la matumizi ya tiketi za kieletroni

Nilitegemea kuona milango ikiwa wazi mapema zaidi na watumishi wengi wanaoweza kuhimili uwepo wa watu wengi wakihudumu lakini pia haikuwa busara kuanza na jambo kubwa kama hilo katika mechi kubwa namna hii ilipaswa majaribio yaanze wakati ligi ikianza hata kwa mechi ndogo hii inaonyesha kabisa hatuna utaratibu wa kufanyia kazi mapungufu ya msimu uliopita.

Swala la kuzuia vurugu za Uwanjani ipo haja ya kuchukuliwa hatua kali kwa wanaosababisha vurugu hizo.
Pengine tutawalaumu waliovunja viti na kuwapa adhabu kali sana adhabu ambayo itarudi kwa timu husika Simba lakini kuna hatua gani zitachukuliwa dhidi ya Refa wa mchezo huo Martin Saanya?

Ni dhahiri kwamba refa huyo alishindwa kabisa kumudu kasi ya mchezo huo kwani licha ya goli la Tambwe lakini maamuzi yake ndiyo yaliyopelekea vurugu hizo hali kama hii ya marefa kujiamulia maamuzi yao na kushindwa kufata zile sheria 17 za soka ndiyo mara nyingi huleta vurugu.

Hebu fikiria gharama ambazo watu wanatumia kuandaa timu usafiri kwa wachezaji na benchi zima la ufundi,kambi ambavyo vvyote hivyo hugharimu fedha nyingi ukijumlisha na mashabiki wanaojichanga kupata fedha ya kununua tiketi hii yote inaonyesha jinsi gani watu wanataka kupata burudani ya mchezo huu ambao ndiyo unaopendwa zaidi duniani.

Mechi kibao Katika ligi yetu zimekumbwa na hii adha ya maamuzi mabovu kuanzia katika ligi kuu mpaka Mchangani ambako hali huwa mbaya zaidi. Tumesikia Juzi Kocha Jamhuri Kiwelu akitangaza kuachana na mpira jana pia Mmiliki wa African Lyon nae akalalama kuhusu maamuzi mabovu ya marefa wetu hili si jambo la kupuuzia.

Watu hawa wanahangaika kupata burudani watu wanatumia mamilioni ya pesa lakini mtu mmoja tu anakwamisha maendeleo ya soka letu na kuhatarisha amani ya nchi hii hivyo hili si jambo la mzaha na kuishia tu kuwalaumu mashabiki hawa marefa waangaliwe upya.

NINI KIFANYIKE
Mi nadhani kitu kikubwa kinachopaswa kufanyika kwa haraka ni kwa kuwafungia kutojihusisha na soka waamuzi wa namna hii.

Kuwakabidhi katika vyombo vya dola kubaini kama kuna rushwa yoyote ilitolewa ili mwamuzi apindishe sheria.

Kuwapa Chama cha Marefa Tanzania jukumu la kupanga nani achezeshe mchezo upi na kukitokea jambo lolote lisilofaa basi chama hicho kiwajibike.

Kuwe na elimu ya urefa katika vyuo vyetu ili tuweze kupata wasomi wanaoweza kutafsiri vyema sheria 17 za soka.

Vilabu viwe na utamaduni wa kuelimisha mashabiki wao umuhimu  wa kudumisha amani michezoni.

Kuwa na maaskari katika majukwaa ili kudhibiti aina yoyote ya Vurugu katika majukwaa.

Hakika tusipokua makini ipo siku tunaweza kushuhudia makubwa zaidi ambayo ni hatari.

ASANTENI
Edo DC

Unaweza kunipata
Instagram: @Edodanielchibo
Facebook : edodanielchibo
Twitter: @EdoDaniel1

No comments

Powered by Blogger.