KARATASI ZA KITABU CHA MSIMU ULIOPITA RANIERI ALIZIFUNGIA KITUMBUA.
Wakati Danny DrinkWater akiwa mchezaji bora Wa Klabu ya Leicester City msimu Wa 2013-2014 masikio yangu yalianza kulazimisha shingo kugeuka kuangalia kwenye kikosi cha Nigel Pearson lakini nilishupaza shingo.
Sikukubali macho yangu ya nyama kunifanya niendelee kushupaza shingo pale niliposikia Cambiasso amejiunga na Leicester city, niliamua kugeuza shingo nikajiuliza kwanini Cambiasso amekuja Leicester city? Sikupata jibu sahihi nikaamua kuendelea na safari bila kuwatazama tena nikiamini Mwisho Wa Msimu nitapata jibu la swali langu.
Mwisho Wa msimu nilipata jibu, moyo wangu uliniambia Cambiasso hakujua alichokifuata kwani aliambuliwa kuwa mchezaji bora Wa klabu kwa msimu huo na baada ya hapo akaondoka.Baada ya moyo wangu kunipa lile nilitabasamu kisha jicho langu likatoka kwa muda kwao.Lilirudi tena niliposikia Ranieri kateuliwa kuchukua nafasi ya Nigel Pearson.
Safari hii ilibidi niwe mtulivu kiasi utulivu wangu uliongozwa na swali lile ambalo nilijiuliza kwa Cambiasso, na hapa nilijiuliza kwanini Ranieri kaja Leicester city ? Kipi amekiona? Sikupata jibu sahihi zaidi ya moyo wangu kuniambia safari hii usishupaze shingo geuka na umkodolee Ranieri uangalie kilichomfanya aje Leicester City.
Mwisho Wa msimu ulipoisha alinionesha alichokiijia, kile alichoshindwa kukipata Chelsea alikuwa amekipata Leicester City tena na kikosi kilichokuwa kimeundwa na wachezaji Wa kawaida waliokuwa wamenunuliwa kwa pesa ndogo sana.
Baada ya msimu kumalizika nilijua Ranieri angekichukua kitabu cha msimu Wa 2015-2016 ili aangalie madhaifu yake kisha ayafanyie kazi itakayomfanya awe na msimu mzuri tena lakini madhaifu yake aliyaangalia kwa jicho huku jingine akiwa amelifumba na mwisho wa siku akazalisha matatizo yanayomsumbua mpaka sasa.
Msimu uliopita Ranieri alikuwa ndiye kocha pekee wa Ligi kuu ya England aliyekuwa amechezesha kikosi kifinyu kuzidi makocha wote wa ligi kuu ya England. Hii tafsri yake ilikuja na matokeo gani?
Kwanza wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza walichoka.Mchezaji anapokuwa na uchovu kuna vitu vifuatavyo tegemea kuvipata kwake.Mosi, Majeraha ,Pili kupungua kwa kasi na nguvu uwanjani, tatu na mwisho kiwango cha mchezaji kushuka sana.
Wachezaji wengi ambao msimu uliopita walionekana ni wachezaji muhimu (Kama Drinkwater, Mahrez, Albrighton, Vardy) wengi wao msimu huu wanaonekana wamechoka.
Hii imekuja kuathiri matokeo ya timu kwa ujumla. Mfano kabla hujaanza kujiuliza kwanini Vardy hafungi msimu huu jiulize msimu uliopita Vardy alikuwa amezungukwa na nani?? na msimu huu hao watu wanaomzunguka wakoje?
Kante ndiye alikuwa mhimili wa timu sitaki kumzungumzia sana ila nataka nikuoneshe mtiririko mzima Wa Leicester City ulivyolegezwa. Kante aliwafanya wachezaji wafuatao kuwa kazi nyepesi sana msimu uliopita.Drinkwater na Mahrez.
Hawa ndiyo waliomfanya Vardy afunge goli 11 kwenye mechi 13.Drinkwater alitengeneza nafasi za magoli kwa sababu hakuwa na wasiwasi kwenye eneo la ulinzi kwa sababu Kante alikuwepo.
Drinkwater alipata mipira mingi baada ya Kante kupokonya mipira.Mahrez alikuwa na uhakika wa kupata mipira mingi kutoka kwa DrinkWater na kufanya alichokuwa anakitaka(Iwe kufunga au kutoa pasi za mwisho kwa Vardy).
Hapo ndipo tunapopata somo la Pili ambalo Ranieri hakutakata kulisoma vzuri ndiyo maana anaonekana kama atafeli, somo lenyewe la kuondoka kwa Kante.Ranieri alitakiwa ajue kwamba yeye ndiye bingwa mtetezi kwenye ligi yenye ushindani, hivyo asingeogopa kuingia sokoni kwa nguvu zote kununua mchezaji mwenye kariba ya Kante ili kuziba eneo lile muhimu kwenye timu.
Kwa kuchezesha kikosi finyu msimu uliopita nilitegemea msimu huu angeteneza kikosi kipana.Tafsiri halisi ya kikosi kipana haimanishi kuwa na wachezaji wengi, ila maana halisi ya kikosi kipana ni kuwa na wachezaji wengi wenye viwango vikubwa vinavyokaribiana. Lakini kwa Leicester City hilo halipo.
Mfano, katika nafasi za wachezaji Wa nyuma kuna mapungufu makubwa sana kwa upande Wa wachezaji Wa akiba kwani hawasadifu maana halisi ya kikosi kipana.
Beki Wa kulia Danny Simpson hana mbadala mzuri, mchezaji ambaye anayetumika kama mbadala wa Simpson ni Marcin Wasilewski ambaye kiuhalisia ni beki Wa kati ila wakati mwingine hucheza kama beki wa kulia na umri wake unamtupa(ana miaka 36).
Beki Wa kushoto Christian Fuchs mbadala wake ambaye ni Jeffrey Schlupp asili yake ni mshambuliaji wa pembeni (Kushoto) ila huwekwa tu kama beki Wa Kushoto. Ben Chilwell ni beki mwenye umri Mdogo sana ambaye huwezi kumwamini msimu mzima kwenye eneo la ulinzi.
Ligi ya Uingereza ni ndefu , ngumu na haina mapumziko hivyo unapokuwa huna kikosi kipana na ukizingatia wachezaji wako walitumia nguvu kubwa msimu uliopita kubeba ubingwa, mwisho wa siku pumzi itakata na utawaacha wengine waendelee kukimbizana.
Kwa hiyo Ranieri hajachelewa sana, anachotakiwa kukifanya ni kuwapumzisha wachezaji baadhi nyota kama Mahrez na kumwamini Gray.Acheze kamari kwa Gray kwanza.Hakuna mchezo mzuri kama kamari ingawa unapocheza kamari kwa mara ya kwanza utaanza kwa kushindwa lakini ukiendelea matunda yake yatakuja kulipa gharama zote ulizozitumia uliposhindwa.
Tumeona kamari ilivyozaa matunda kwa Celtic na Borrusia Dortmund kwa kuwaamini kina Dembele, Rashford kwa Manchester United, Iwobi kwa Arsenal.Misimu miwili iliyopita Pochettino alicheza kamari ya Kane mbele ya Adebayor, Dier na Delle Alli.
Pia Slamini na Mussa wanatakiwa wawapumzishe Vardy na Ozakazi.
Asanteni sana na MUNGU awabariki.
Martin Kiyumbi.
Facebook na Instagram utanipata kwa jina la Martin Kiyumbi.
(E-mail: Martin Kiyumbi@gmail.com, 0744080891, 0657771077)
No comments