GUARDIOLA NI MWANAFUNZI WANGU TU - RONALD KOEMAN

Meneja wa Everton Ronald Koeman amesema wakiwa wote Barcelona enzi wakiwa wachezaji alikuwa akimfundisha Pep Guardiola 'mtindo wa kiholanzi' wa kucheza soka

Everton inayofundishwa na Koeman hivi sasa itavaana uso kwa uso na Manchester city katika uwanja Etihad Jumamosi ijayo.

Akielezea wakati wao walipokua pamoja Barcelona, Koeman ameelezea ni jinsi gani alikuwa na kazi ya kuwalea vijana wa  'Kicatalan' kwa kufuata maelekezo aliyokua akipewa na kocha mkuu wa Barcelona kipindi hicho, marehemu Johan Cruyff.

Akizungumza na gazeti la  Sunday Mirror, Koeman amesema:

"Mimi nilikua karibu sana na Cruyff na siku moja aliniita"

"Akaniuliza kama nitapenda kuishi chumba kimoja na kijana mmoja aliyemuona kwenye shule ya watoto ya Barcelona"

"Cruyff alisema amemwangalia kijana huyo kwa muda mrefu na alidhani wakati muafaka ulikua umefika wa kumpeleka kwenye  kikosi cha kwanza cha Barcelona"

"Kwa mujibu wa Cruyff kijana huyu alikuwa mkali sana wa kutandaza soka, alikuwa na ubongo mzuri wa kufanya maamuzi na kuelewa anachofundishwa kwa haraka na alihitaji uangalizi zaidi kutoka kwa mchezaji mzoefu atakaemsaidia kwa ukaribu"

Koeman aliongeza:

"Mimi nilimjibu Cryuff ni sawa tu, hakuna tatizo, Kama mchezaji alikuwa na kipaji na ni kijana mzuri, nitapenda kumsaidia"

"Basi akaniambia kwamba kuanzia sasa mimi nitakua na kazi ya kukaa karibu na kijana aitwaye Pep"

"Akaniambia mimi nitakuwa mwalimu wake, kumsaidia, kuendeleza soka lake na kuhakikisha anaijua  style ya kiholanzi ya kucheza mpira"

"Kuanzia hapo mimi na Pep tulikua tukishiriki katika vyumba vya hoteli, vyumba vya kubadilishia nguo kabla ya kila mchezo, kabla ya kila safari na  katika mechi za maandalizi ya msimu mpya. Kila tukisafiri kwenda nchi za Ulaya, Marekani na Asia mimi nilikua karibu na Pep"

"Johan alisema ni muhimu kwa wachezaji vijana kujifunza kutoka kwa wachezaji wazoefu"

"Pep alikuwa mtu wa  ajabu kabisa. Yeye alikuwa na hamu ya kujifunza tu, alitaka kujua kila kitu. Pep alitaka kujua kuhusu shule za kiholanzi za mpira wa miguu"

"Zaidi kuliko mchezaji mwingine yeyote alitaka kujua kuhusu aina ya mpira wa kugusa (tik-tak) na kuhusu kucheza kwa nafasi, kugusa mpira mara moja katika nafasi ndogo (one-two passes)"

"Pep alipenda sana mbinu za Johan Cruyff na alipenda mbinu hizo zitumike kuifundisha Barcelona"

"Lakini kilichonishangaza kabisa kutoka kwa Pep ni kwamba alikuwa mtu wa kawaida sana, anayependa kujishusha.

"Kamwe hakuwa na kiburi wala ubishi, wala hakuwahi kuishi kama mtu maarufu ati kwa sababu alikuwa akiichezea Barcelona"

"Huwezi amini wakati akiwa mchezaji wa timu ya wakubwa alikuwa akiendesha gari ya  mtumba aina ya Golf"

"Hata alipofikisha miaka mitatu kwenye kikosi cha wakubwa pamoja na kuongezewa mshahara bado alikua akiendesha gari hilo hilo moja"

No comments

Powered by Blogger.