ZOEZI LA KUSAKA VIPAJI : VIJANA 6 WAPATIKANA ILALA, JUMAMOSI HII NI ZAMU YA KINONDONI
VIJANA sita
wenye umri wa chini ya umri wa miaka 17 (U-17), wamefanikiwa kufuzu majaribio
yaliyoendeshwa na Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kwa wakazi
wa Wilaya ya Ilala leo Jumamosi.
Majaribio hayo yaliyofanyika
kwenye Uwanja wa Jakaya Kikwete Youth Park (JMK), Kidongo Chekundu, Dar es
Salaam, ni ya pili kufanywa na Azam FC katika programu ya kutengeneza timu ya
vijana chini ya umri wa miaka 17.
Kikosi hicho kinachojengwa
kupitia mradi huo utakaohusisha kusaka vipaji kwa mikoa 13 nchini, kitaundwa na
wachezaji 18 tu ambao watalelewa ndani ya kituo cha kukuza vipaji cha Azam FC
‘Azam Academy’, ambamo watapata elimu ya kawaida, ya soka pamoja na malazi.
Zoezi la majaribio kwa wilaya
hiyo leo, limehudhuriwa na vijana 448 likiwa ni ongezeko la vijana 25, hii ni
kutokana na vijana 423 kujitokeza kwenye lile la kwanza lililofanyika Azam
Complex Jumapili iliyopita likihusisha wakazi wa Wilaya ya Temeke na Kigamboni.
Kitu cha kuvutia zaidi kwenye
majaribio hayo, walijitokeza baadhi ya watoto wadogo chini ya umri wa miaka 13,
ambao nao walipewa nafasi ya kuonyesha uwezo wao huku wengine wakilivutia
benchi la ufundi.
Idadi hiyo ya vijana sita
inafanya kufikia 11, ambao wamechaguliwa mpaka sasa kwenye mchujo wa awali
wengine wakiwa ni wale watano waliopitishwa katika mchujo wa kwanza wiki
iliyopita.
Mara baada ya kumalizika kwa
majaribio hayo, Mkuu wa Maendeleo ya Soka la Vijana Azam FC, Tom Legg,
anayeshirikiana na John Matambala, kung’amua vipaji hivyo, alionyesha kuvutiwa
na vipaji vya Wilaya ya Ilala huku akidai kupata wakati mgumu kuchagua
wachezaji sita wa mwisho.
“Kumekuwa na mabadiliko makubwa
hapa kwa vipaji vingi kujitokeza tofauti na Temeke, lakini siwezi kusema Temeke
hakukuwa na vipaji, walikuwa wengi lakini hapa wamejitokeza wengi zaidi, zoezi
letu leo limekuwa gumu sana hadi tunakuja kupata vijana sita wa mwisho,”
alisema.
Kumalizia Kinondoni
Zoezi la kusaka vipaji vya umri
huo kwa mkoa wa Dar es Salaam, linatarajia kumalizika Jumamosi ijayo (Septemba
10, mwaka huu) kwa vijana wa Wilaya ya Kinondoni na Ubungo kujaribiwa ndani ya
Uwanja wa Tanganyika Packers, uliopo Kawe.
Kuelekea majaribio hayo ya mwisho
kabla ya kuhamia mikoani, Legg amesema kuwa ana matumaini ya makubwa ya kupata
vipaji vingine bora zaidi katika eneo hilo huku pia akitarajia vijana wengi
zaidi kujitokeza.
Azam FC inawaomba vijana
waliochini ya umri wa miaka 17, waliozaliwa mwaka 2000, 2001 au 2002 kujitokeza
kwa wingi kuonyesha vipaji vyao wakiwa na nakala ya vyeti vyao vya kuzaliwa
pamoja na wazazi au walezi wao siku hiyo kuanzia saa 1.00 asubuhi.
No comments