WADACHI WAMEZIMIKA GHAFLA KAMA MSHUMAA ULIOWASHWA BAHARINI

Na: Ayoub Hinjo
Umebahatika kukitazama kikosi cha Waholanzi kipindi hiki cha karibuni!? Kama hujapata nafasi hiyo shukuru sana kwa kukosa nafasi ya kuyanusuru macho yako sababu inaweza kukuumiza moyo wako kwa kuwaona Wadachi ambao wamepoteza uhalisia wao kama Samson aliyekatwa nywele.


Katika dunia hii Wadachi ndio wanadamu pekee ambao waliyafukuza maji ya bahari na kuamua kujenga makazi. Hilo si jambo geni kwa wale waliofanikiwa kusoma Geography kidato cha pili au tatu na hata huko elimu ya juu zaidi. Jeuri hiyo ya Wadachi ndio iliyowafanya kuamini kila kitu wanaweza wanafanya katika uso wa dunia hii.

Maisha ya ndani uwanja walifanikiwa kuyamudu kwa kiasi kikubwa sana hasa katika kuzalisha wachezaji bora duniani. Kila kizazi chao kilikuwa bora katika kushindana na timu zingine bora kama Ujerumani,Uingereza,Italia na wengine. Pamoja na kufanikiwa kuzalisha wachezaji hodari bado hawajashinda kombe la dunia licha ya kufika fainali mara tatu(1974,1978,2010).

Sasa hali ni mbaya kwa Waholanzi ambao walishindwa kufuzu EURO 2016 nchini Ufaransa. Kizazi bora cha Wadachi kimefika mwisho na tatizo ambalo linawasumbua ni kushindwa kuzalisha wachezaji bora ambao wanaweza kuziba nafasi za kizazi kilichofika mwisho.

Kadri siku zinavyosogea Wadachi ndio wanazidi kukera. Jaribu kukifikiria kizazi cha akina Cruyff kisha fikiria hiki cha aina Memphis. Baada ya kombe la dunia nchini Brazil 2014 ilitakiwa Wadachi wajitathimini zaidi licha ya kuishia nafasi ya tatu. Kizazi cha akina Robben,Sneijder na RvP hakina jipya tena. Lakini ni nani anaweza kuziba nafasi zao hata kwa kutoa nusu ya uwezo walionao sasa ikiwa wachezaji wenyewe ndio hawa wakina Memphis na Wijnaldum!?

Wachezaji wa sasa kutoka Uholanzi wanatia mashaka kutokana na viwango vyao kuwa kama moto wa kifuu. Mara chache wanakuwa vizuri lakini mara nyingi wanakuwa kwenye ubora wa maudhi yao hata hao wakina Memphis na Clasie wanashindwa kupata nafasi kwenye klabu zao halafu ndio wanapewa mzigo wa kubeba timu. Wijnaldum na yeye kiwango chake cha maji kupwa na kujaa haridhishi moja kwa moja bado ndio nyota anayetakiwa kuibeba timu.

Dalili za Wadachi kufika mwisho zilionekana baada ya kutoka Brazil. Hadi sasa wameshindwa kumtafuta RvP na Robben wao kama walivyofanikiwa kuziba nafasi ya Kluivert na wenzake. Ni kama mshumaa uliokuwa umewashwa baharini halafu ghafla upepo mkali ukavuma. Tuwasubiri tena Wadachi sababu ndio hawa hawa waliofanikiwa kuyafukuza maji na kuweka makazi.

No comments

Powered by Blogger.