KATIBU MKUU MPYA SIMBA PATRICK KAHEMELE ANZA NA MAMBO HAYA

Natumai ujumbe huu utakufikia popote pale ulipo Mheshimiwa Patrick Kahemele.
Awali ya yote nikupongeze sana kwa kupata nafasi ya kuwa Katibu Mkuu mpya wa klabu yetu ya Simba SC (wekundu wa Msimbazi) ni matumaini yangu kwamba utafanya kazi kwa weledi ili kuitoa Simba hapa ilipo hivi sahivi

Mkuu kabla ya kuanza kutekeleza mipango yako mikubwa kwa Klabu yetu nataka kukumbusha tu (Simba na Yanga ni klabu za michezo mbalimbali na sio klabu za mpira wa miguu tu kama ilivyozeeleka) Nakuomba uyaangalie mambo yafuatayo:

1. Kuirejesha Tovuti ya klabu.

(www.simbasports.co.tz ) hewani.
Tovuti hii ya timu ilizinduliwa kwa mbwembwe sana Mwezi Juni, 2015 lakini kwa sasa haipo hewani .Wale jamaa wa EAG Group wakina Iman Kajula walitoa ahadi kibao kwamba tovuti itakuwa na habari motomoto za Klabu na kwamba itasaidia klabu kutangaza na kuuza bidhaa zake kwa urahisi.

Mwanzoni walianza na kasi nzuri kweli. Sasa katibu mkuu hakikisha ndani ya siku chache tovuti inarudi hewani na na inakuwa yenye habari za motomoto za Klabu. Tovuti kwa wakati huu tulionao ni muhimu sana. Tovuti inapaswa kuwa chanzo kikuu cha cha habari na taarifa za Simba ukizingatia gharama za kuendesha tovuti ziko chini ni aibu kwa Klabu ya kariba ya Simba kutokuwa na tovuti yake binafsi.

Kwenye hili Watu wa EAG Group wakina Iman Kajula wajitathimini/wajitazame maana ndo wasimamizi wa tovuti. Wakati wa uzinduzi wa tovuti hiyo Iman Kajula alisema yafuatayo:
“Tovuti hii sio tuitaiwezesha Simba kuwapa wadau wake taarifa mbalimbalibali pia itatumika kwa ajili ya uuzaji wa vifaa vya Simba, Bidhaa mbalimbali mpya na muhimu zaidi kuwaunganisha wanachama, mashabiki na wapenzi wa Simba kutumia mitandao ya jamii iliyo rasmi ya Simba Sports Club’’.

2. Utekelezaji wa Mikataba ya Klabu.

Simba iliingia mkataba wa udhamini na EAG Group mwezi April mwaka 2015. Pitia Mkataba huo ili kujua kama umetekelezwa kwa kiwango gani. Mfano, utoaji tuzo za mchezaji bora. Wakati wa utiaji saini, Rais Aveva alizitaja tuzo hizo ni ya mchezaji bora wa mwaka atakayepewa gari jipya, mchezaji kijana mwenye kipaji atakayepewa milioni 5 na mchezaji mwenye nidhamu atakayelamba milioni moja.

 Pia, wachezaji hao walitakiwa kupewa zawadi ya simu aina ya Huawei yenye thamani ya shilingi milioni moja ambao nao waliingia kwenye udhamini huo. Lakini mpaka sasa klabu ipo kimya mdhamini naye yupo kimya hakuna mchakato wowote unaoendelea kuhusu tuzo hizo maana kiuweledi ilipaswa hadi sasa hadi mchakato wa kuwapata uwe umeshakamilika au ushaanza. Maana suala hili lilitakiwa likamilike hata zoezi la usajili kuanza maana baada ya usajili kuanza kuna hatari ya tuzo kupewa wasiostahili kisa aliyestahili kaachwa na Klabu au kasajiliwana klabu nyingine halafu tuzo zikakosa uhalisia. Klabu nyingi duniani hutoa tuzo zake mara baada ya ligi kuisha. Tuzo ambazo mpaka sasa zilitolewa bila kukosa ni zile za mchezaji bora wa mwezi tu.

Hili suala la tuzo za wachezaji ni moja tu kati ya mengi ambayo naamini hayaendi sawa mpaka sasa kulingana na mkataba wa Simba na EAG Group. Vile tupia jicho mkataba wa TBL kama unatekelezwa kwa asilimia mia moja na kwenye mapungufu uboreshwe kwa maana huu sio wakati wa kufanya mambo kwa mazoea tena.

3. Duka la Simba

Duka la klabu lilifunguliwa kwa mbwembwe sana na lilitangazwa sana lakini sasa naona kimya hakuna mwendelezo wake. Biashara ni matangazo huwezi kukaa kimya watu wakawa wanakuja tu wenyewe kununua bidhaa za timu ni kujidanganya. Na kingine duka lile halijitoshelezi kabisa. Mfano, Kuna jamaa yangu alienda kununua jezi zinazotumika mazoezini akazikosa pale ilibidi akanunue kwenye duka la vifaa vya michezo la UHLSports la Dewji.

4. Uwanja Wa Bunju

Kipindi cha ukatibu mkuu wa Ezekiel Kamwaga alionyesha juhudi Fulani za kuipatia klabu hata uwanja wa mazoezi lakini mara bada ya yeye kuondoka uwanja ukarudi tena kuwa pori. Katikati hapa zilipigwa kelele za uwanja wa nyasi za bandia lakini mpaka sasa kimya. Pale Bunju Uwanja wa mazoezi sio lazima uwe wa nyasi za bandia jambo la muhimu ni uwanja mzuri wenye nyasi zinazohudumiwa vizuri basi. Ukiamua Kulifanikisha hili utalifanya ndani ya muda mfupi tu. Weka uwanja pale pamoja na hosteli zake ukiwa makini utalifanikisha hili.

5. Jengo la Klabu

Pitia Mikataba ya wapangaji na utuambie ni wakina nani wapangaji pale, kwa mikataba ya muda gani, wanalipa pango kiasi gani na pesa hizo zinatumikaje. Jingine, utafute wawekezaji pale ufanyike uwekezaji mkubwa na wa maana ili klabu inufaike na kuwa na umiliki wa eneo la ardhi lenye thamani kubwa katikati ya jiji. Majengo yaliyopo pale kwa sasa hayaendani na thamani ya eneo lile na hadhi ya klabu.

6. Wadhamini wa Klabu

Tafuta wadhamini wengi zaidi kwa ajili ya klabu kuliko kutegemea TBL peke yao. Tafuta wadhamini watakaodhamini jezi za mazoezi n.k. Simba ni Klabu kubwa haiwezakani ikawa inavaa tu vifaa vya Adidas, Nike, Uhl bila kunufaika kwa lolote zaidi ya kuyatangaza hayo makampuni.

Tafuta kampuni ambayo itakuwa tayari kutoa udhamini kwa Klabu kuna makampuni mengi tu ya vifaa ambayo yatakuwa tayari kujitangaza kupitia Simba ambayo sio lazima yawe haya yaliozoeleka. Tafuta wadhamini wa kila aina wakubwa kwa wadogo. Jezi za klabu zinapaswa kuchafuka na nembo za wadhamini,kama timu za wenzetu. Klabu iache kufanya mambo kwa mazoea.

Kwa leo naomba niishie hapa. Ni Matumaini yangu utaufanyia kazi “kajiushauri” haka.
Ni mimi Shabiki Kindakindaki wa Simba
 ‘’SIMBA NGUVU MOJA”
Na mwisho kabisa, Karibu kitaani kwetu Mtaa wa Ligi kuu ya Vodacom, Nyumba Namba 3, Ghorofa ya 3, Chumba Namba 3, Mkabala na kituo cha ma 3 ,hakika huwezi potea nipo hapo kwa mwaka wa tatu sasa.

~ Mwandishi wetu

No comments

Powered by Blogger.