MUDA MUAFAKA WA RASHFORD KURUDI DARASANI UMEWADIA.

Kamwe huwezi kuitwa shujaa kwa kufanya kile kinachoweza kufanywa na wengine. Ushujaa ni kufanya kile ambacho wengi wameshindwa kufanya na hata kama wakifanya wanashindwa kufanikisha.


Maisha yetu siku zote yapo katika mzunguko. Mzunguko huu wa maisha ndio unamleta Zlatan Ibrahimovic katika timu ya Manchester United. Unadhani katika mzunguko huu Rashford alipenda kuona jina tofauti na Cadabra linaingia United!!? La hasha moyo wake ulikuwa unakesha ukisali na kuomba United wamsajili Ibrahimovic sababu kwa akili ya kawaida ataendelea kupata nafasi katika timu na atapata dakika nyingi za kucheza.

Ibrahimovic yupo katika safari ya mwisho ya maisha yake ya mpira. Cadabra hataki Balloon D'Or kwa sasa anachotaka ni kufurahia maisha yake yanayoenda ukingoni akiwa katika mikono salama na ikiwezekana aondoke kwenye safari hii kwa heshima zaidi. United kuwa na Ibrahimovic kuna fungua fursa ya Rashford na wenzake kuonyesha walichonacho. Wakina Rashford watakuwa darasani kusoma kile anachofundisha Ibrahimovic anapokuwa uwanjani kisha wao kuongeza zaidi au kuchukua kama vilivyo na ikiwezekana kupunguza baadhi ya vitu watavyoona kwao havina mashiko.

Unadhani Mourinho anafurahi sana moyoni mwake!!? Hapana anajua safari yake ya kuendesha basi la Manchester United ni ngumu na katika safari hii alihitaji kuwa na abiria wa uhakika ambao watafanya safari iwe bora na mafanikio tele. Unadhani Mourinho hataki kuwa na Benzema,Lewandowski,Aubameyang,Higuain,Suarez na wengine katika timu yake!! Nadhani Jose anavyomwangalia Rashford anatoa tabasamu katika uso wake huku moyo ukivuja machozi. Mourinho ni kocha ambaye anatengeneza uhakika wa kila kitu kifanyike kwa usahihi ndio maana katika timu alizopita alisajili watu wa uhakika wa kusafiri nao katika basi lake huku akiwa na uhakika wa kufika salama popote atakapo kwenda.

Mzunguko huu wa maisha umemleta Rashford mikononi mwa Mourinho. Mara zote hajali anashambuliwa mara ngapi ila yeye anachojali ni uhakika wa timu yake kupata magoli. Hata pale unapo jaribu kumwangalia Mourinho huwa anatengeneza timu yenye ukuta mgumu ambao utahimili mikiki mikiki ya wapinzani bila ukuta kuvunjika. Uwepo wa Ibrahimovic unafuta machozi kwenye moyo wa Mourinho lakini W
wasiwasi ni Ibrahimovic kuendana na presha ya kila mwisho wa wiki pale Uingereza katika umri wake alionao sasa inaweza kuwa kamari kuamini atafanikiwa kwa asilimia 100.

Mourinho wa United anaweza kuwa tofauti na yule ambaye alikuwa anajulikana na wengi. Kutoka kwa Eto'o,Drogba,Benzema,Higuain,Costa hadi kwa Rashford ambaye ndio anaanza safari ambayo Ibrahimovic yupo karibu kuimaliza.

Sala za Rashford zimefanikiwa kumleta Ibrahimovic pale Old Trafford. Sala zake zitafanya Roy Hodgson apate muda wa kwenda Old Trafford kumwangalia kila mwisho wa wiki utakapofika. Rashford wa Mourinho anaweza kuwa na hatari zaidi ya yule wa Van Gaal ambaye alimnyima hamasa ambayo ataipata kwa Mourinho anayejua kumfanya mchezaji kucheza zaidi ya uwezo wake alionao.

Mwalimu Zlatan atamrudisha Rashford darasani kujifunza zaidi na zaidi. Kipaji cha Rashford si cha kuisha leo,uwezo wake utamfikisha alipofika Ibrahimovic sasa.

~ Ayoub Hinjo

No comments

Powered by Blogger.