NINACHOAMINI MAESTRO :PROF. WENGER ALIJIANGALIA KWENYE KIOO MARA MBILI MBILI.


Na: Ayoub Hinjo
E-mail: hinjo38@gmail.com

Kufahamu thamani yako ni jambo bora katika maisha. Unapoifahamu na kuitunza thamani yako malipo yake ni kupata zaidi ya ulicho nacho. Wakati mwingine kuanza upya si ujinga inategemea muda tu wa jambo lako kukamilika hili mambo mengine yaendelee.




Arsene Wenger ni mmoja wa makocha bora duniani. Ni kocha aliyekuwa anaombewa mabaya karibu muda wote na mashabiki wake wa Arsenal hili atimuliwe kwenye timu hiyo. Ni kocha ambaye amedharirika kwa vipigo vikubwa kutoka kwa wapinzani lakini hakukata tamaa na timu yake. Maisha ndani ya Emirates yamebadilika ghafla. Maisha ndani ya Emirates ni matamu tena yasiyo na mfano kwa Wenger mwenyewe,wachezaji na kwa mashabiki wale ambao walikuwa wanatamani aondoke. Mchawi wa Wenger alikuwa ni Wenger mwenyewe na mtu wa kumsaidia Wenger alikuwa ni Wenger mwenyewe pia. Profesa ameifahamu thamani yake sasa. Profesa alianza upya kila kitu na sasa kinaelekea mwishoni kumalizika.

Rejea miaka 5 nyuma kisha ifananishe Arsenal ya ile ambayo kumiliki mpira ni silaha bora kwao kuliko matokeo uwanjani. Arsenal ambayo Patrice Evra alidiriki kuwaita Wavulana. Arsenal ambayo ilikuwa haina ubavu wa kupambana na timu kubwa na mwishowe waliambulia vipigo vitakatifu. Arsenal ambayo mastaa wa timu waliikimbia na kuitelekeza timu kwenye wakati wa shida kwa tamaa ya kushinda makombe na kuvaa medali mbalimbali. Ukiachana na hayo yote rejea kwa Wenger huyu na Arsenal yake hii ya sasa. Maisha yamebadilika ghafla ndani ya Emirates. Arsenal ya sasa inacheza mpira wa kupata matokeo kwanza kisha mambo mengine yatafuata. Inawezekana shughuli ya kuijenga upya Arsenal ilianza baada ya deni kubwa la uwanja kumalizika,baada ya kumalizika kwa deni hilo Wenger alirejea kwenye kioo na kujitazama tena na tena. Aligundua alikuwa anajiroga mwenyewe na dawa alikuwa nayo yeye mwenyewe. Mabadiliko makubwa ya Arsenal yalianza baada ya Wenger kuvunja rekodi ya usajili klabuni hapo kwa kumsajili Mesut Ozil ambaye alikuwa Real Madrid na muhimili wa timu kwenye mashambulizi. Hakuishia hapo tu aliendelea kufanya usajili kwenye nafasi za lazima kwenye timu kwa kuwasajili Gabriel Paulista,Danny Welbeck na Alexis Sanchez ambao alitumia pesa nyingi kwao pia. Mabadiliko hayo yamebadilisha mambo mengi kwenye timu kuanzia mfumo wa uchezaji hadi mfumo wa kupata matokeo. Baada ya msimu wa 2014-15 kuisha Wenger alifanya usajili wa kushtukiza kwa kumsajili Petr Cech kutoka Chelsea. Usajili ambao mashabiki wa Arsenal na wapinzani walishangaa lakini kwa imani yake mwenyewe Wenger naamini aliamini Arsenal haitokuwa salama kwenye mikono ya makipa ambao wapo ila kwa Cech itakuwa kwenye usalama zaidi. Uzoefu wake na ubora wake wa kudaka ndio umeifikisha Arsenal hapo ilipo sasa. Matumizi mazuri ya Ozil yanaleta matunda kwenye timu. Arsenak ni timu yenye kasi sana wakati wa mashambulizi kwa kupitia pembeni au kati kati kasi yao inatoa presha kubwa kwa wapinzani na pia nidhamu ya timu pindi inapokutana na timu kubwa.

Arsenal ni timu iliyokuwa na uwiano sawia kwa sasa ndio maana inacheza mpira na kupata matokeo chanya kwa sasa. Mtihani uliobaki kwa Wenger ni kuhakikisha timu ipo kwenye mstari na hakuna kitu kingine kitaharibu mipango yake japo majeruhi yamekuwa kikwazo kwenye timu yake. Kwa uchawi huo wa Wenger ataweza kuivusha Arsenal hatua inayofuata kwenye mashindano ya Klabu bingwa Ulaya!!? Wenger atatupa jibu mwezi wa Februari. Maisha ni kama kioo ukicheka nayo yanacheka. Asante Wenger kwa kurejea kwenye kioo na kujitathimini wewe mwenyewe. Asante sana Profesa.

No comments

Powered by Blogger.