NDUGU YANGU MAGULI, MBUZI HANA KAMBA.

Image result for elias maguliSoka ni mchezo wa mahesabu sana, mchezo unaohitaji mipangilio sahihi kupita maelezo. Ni kiasi kidogo tu cha maisha yako ya soka ambapo hutohitaji kuishi kwa mahesabu makali. Soka linaanza kufuta urafiki na mchezaji kuanzia umri wa miaka 32, tofauti na ajira yoyote ile. Katika umri huu huna budi kuanza kupisha damu changa zichukue nafasi, na hata vyombo vya habari vinapunguza upendo wa dhati kwako. Ndio maana kile kipindi cha ukomavu (maturity age)  kuanzia miaka 25 lazima uwe na hesabu zinazoeleweka na unajua nini unafanya na wapi unaelekea, vinginevyo soka litakugeuzia mgongo ukiwa na miaka 28 tu hasa kwa nchi za Kiafrika ambazo kwao kama ni beki ukifungisha katika umri huo wanakuita Mzee,  mshambuliaji usipofunga katika umri huo kwa mechi kadhaa unaitwa Mzee na huku kwetu Tanzania dirisha dogo la usajili unatemwa na pesa unadhulumiwa kwa sababu hujui haki zako na wanaotakiwa kuzisimamia wapo mbali wanasubiri madili ya maana kama la Singano ndio wajitokeze kuwa wao ni wasimamizi na washauri wa mambo ya kimikataba ya wachezaji. Kala Jeremiah alisema katika moja ya nyimbo zake Wizi mtupu.


Eliasi Maguri wakati akiwa Simba 
Nilikuwa natizama suala la Elias Maguli lakini halikuwahi kunistua, nilikuwa nasikiliza na halikua jipya masikioni kwangu. Ni mfululizo tu wa Ile tamthiliya yetu Tanzania isiyoisha inaitwa ubabaishaji. Unaamka, unalala, Kisha unaamka tena ukitarajia mabadiliko katika sekta ya michezo unakuta afadhali ya jana. Wakati soka Taifa Stars na Twiga stars haieleweki zinadhaminiwa vipi mpaka michango itoke kwa wananchi, riadha timu ya Taifa hawajui wanavaaje viatu, cricket hawajui wanalipwaje na Maguli hajui anaachwaje. Roho inaniambia nisikitike lakini utimamu unanituma nicheke maana haya ndio maisha tuliyojichagulia. Maisha ya kusubiri wengine wafanikiwe kisiasa, kielimu, biashara, viwanda na michezo. Kwa sababu hakuna geni katika simba kumuacha Maguli sina haja ya kusikitika wala kuwaza juu yao bali nahitaji kufikiria mara mbili juu ya Maguli mwenyewe na namna ambavyo anaweza kusimamia miiko na tabia za mchezo huu. Kiwango bora cha mchezaji inabidi kiambatane na mambo makuu mawili, mkataba mnono na uwezekano wa kupata timu bora kama yupo kwenye timu ya kawaida (mid table team),  lakini Kuna ongezeko la tatu ambalo kwenye akili za wachezaji wetu halipo ambalo ni kuuzwa nje. Hapa tunazidiwa hata na malawi.

Tatizo kubwa hapa ni washauri sahihi kwa wachezaji wetu, Ivo Mapunda aliwahi kukiri nilipomuhoji katika kipindi cha Sports bar kuhusiana na yeye kuhitaji wakala au mshauri wa maisha ya soka. Alichodai yeye ni kuwa haitaji kwa sababu anajiamini katika kila maamuzi anayofanya. Hakujawahi kuwa na mtu huyu Kisha anafanikiwa sana,  na akifanikiwa basi tambua alitakiwa kufanikiwa zaidi ya pale. Soka ni kama biashara nyingine yoyote,  unahitaji wasaidizi kufika mbali. Unapomuona Cristiano Ronaldo au Neymar wanaingia mikataba minono ya kibiashara na pia kwenye klabu zao, hawa wanao watu sahihi nyuma yao wanaowafanya wawe vile na wanaojua kufanya tathmini ya kipi bosi wao anastahiki. Hawa ndio watu ambao wamemjenga Victor Wanyama mpaka anapata kiburi cha kuwatingisha Southampton wamuuze. Wakati wewe upo uwanjani wao wanakuwa na namba za maskauti wakubwa duniani wanafanya nao biashara kwa kila mpira utakaogusa na kila goli utakalofunga. Tunawaita Frying pan (kikaango), huwezi kukaanga wakati huna pa kuweka mafuta, na mboga yako. Bahati mbaya Tanzania yetu hata ukiwa na mshauri anawaza dili lake kabla ya mchezaji. Yupo tayari kukupeleka simba na sio Mazembe kisa cha juu na kufahamiana na bosi fulani.

Leo kalamu yangu inamuangukia Elias Maguli, sijui kama anatambua kuwa magoli 8 aliyofunga yanatakiwa yawe na thamani kwake na kwa Stand pia. Stand wanufaike na uwepo wake naye anufaike na uwezo wake. Wakati akiwafanya simba wajutie, anatakiwa awafanye Azam wavutiwe na anatakiwa awafanye Kaizer Chiefs wajiulize, ndio usishangae Ligi yetu sio ndogo tena.  Na hii hasa ndio kazi ya wakala mwenye utimamu. Hapa video za Maguli zilitakiwa ziwe Afrika Kusini Muda sana,  hapa Yusuph Bakhresa alitakiwa awe kawekwa mkao wa kula kitambo sana, na wakati huo huo ilitakiwa simba wawe wameshaonyeshwa maringo Muda sana. Ukifanya hivi maana yake mwisho wa msimu wewe huna haja ya kupimwa imani na Altezza mpya na milioni 20. Unakuwa na wateja 6 mezani wakimataifa kwa kitaifa, halafu unageuka unacheza gemu unaacha wakala mwenye akili azichange karata. Kisu chako (sahihi)  kinakuwa cha kukatia vyenye thamani peke yake na sio vibovu. Unaachana na njaa na kuwa uliyeridhika.  Hii ndio namna halisi ya maisha ya soka ya kisasa yalivyo. Bahati mbaya Maguli anaweza kubweteka na goli za Stand,  akanogewa na ACACIA kisha akasahau yeye ni Almasi baharini, maana kwenye mchanga zinaweza kuwa nyingi.  Waswahili wanasema mbuzi hula kulingana na urefu wa kamba yake,  lakini wanasahau kuwa hiyo kamba mpaka avikwe. Maguli hana kamba, na urefu anajiamulia mwenyewe wa kula,  inaniuma tu mbuzi wa Tanzania hupenda kuikimbilia kamba wenyewe.  Jipambanue Maguli.

Ahsanteni.
Nicasius Coutinho Suso

No comments

Powered by Blogger.