KUNA CHA KUJIFUNZA CECAFA
NA ASHA MUHAJI
MWANAFUNZI shujaa haogopi kupiga chabo! Maisha pamoja na
kufanikiwa ni lazima kujifunza. Kama unataka mafanikio basi huna budi kuiga kwa
mtu anayefanya vizuri zaidi yako. Huo ndiyo ukweli wa mambo ulivyo.
Hali si nzuri sana katika soka la Tanzania na kila mdau amekuwa
akitoa mawazo yake ili tu kuhakikisha mchezo unapiga hatua na kamafikio
kupatikana.
‘Nani amfunge paka kengele’? Hakuna muda wa kusubiri kwani mengi
yameshasemwa na bado kasi ya kufika katika nchi ya asali waliko wengine ni
ndogo mno, hivyo kuchepua mwendo na kuongeza kasi ni lazima iwe isiwe.
Nchini Ethiopia kuna michuano ya ….. ya Kombe la Chalenji
inaendelea ambapo kwa nchi kama Tanzania kuna kitu muhimu sana cha kujifunza
kutoka kwa nchi zingine.
Katika michuano hiyo inayoshirikisha jumla ya timu za mataifa 12
ambapo 11 kati ya hizo ni kutoka ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati na moja
iliyobakia Malawi ikishiriki kama timu mualikwa kutoka ukanda wa Cosafa (Kusini
mwa Afrika).
Nchi zote hizo zinapishana sana kiwango lakini cha msingi
kinachotakiw ani kila moja kujitathimini na kufahamu malengo yake ni nini
kufika wazlikofanikiwa wengine.
Katika michuano hiyo nchi za Uganda ‘The
Cranes’ na Rwanda ‘Amavubi’ zimepeleka vikosi vya wachezaji wengi vijana lengo
likiwa kuitumia michuano hiyo kutengeneza vikosi vyao kwa ajili ya Michuano ya
CHAN ambayo fainali zake zinatarajiwa kufanyika Januari mwakani nchini Rwanda.
Kuna tofauti kubwa za vikosi hasa kile cha Uganda kilichoshiriki
mechi za mtoano kuwania kupangwa katika makundi kwa michuano ya Kombe la Dunia
pamoja na hiki cha sasa kinachoshiriki Chalenji. Katika kikosi cha The Cranes
wachezaji wengi ni vijana wenye umri chini ya miaka 23 isipokuwa wachache sana
waliochomekewa ili kuiongezea nguvu timu hiyo.
Kitendo cha nchi hizo kupeleka vikosi vya wachezaji wao wengi
vijana ni dhahiri wanalenga mafanikio katika timu kwa kuwa hao watakuwa hazina kubwa
kwa nchi zao miaka mchache ijayo. Hakika soka la vijana ndiyo suluhisho ya
matatizo ya kisoka yanayoikabili Tanzania hivi sasa.
Mpango kama huo umetumiwa na Nigeria ambayo mwaka huu timu yake ya
taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17 imetwaa ubingwa wa dunia na baada
ya miaka miaka miwili au mitatu ijayo itakuwa na timu bora.
Bila shaka kikosi hicho kitafanya makubwa katika fainali za
wakubwa za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2020 nchini Qatar.
Nchi kama Senegal ilifanikiwa kuwa na timu bora ya taifa kutokana
na msingi madhubuti waliouweka katika timu za vijana kupitia Bruno Metsu na
akafanikiwa kuwazalisha kina Khalilou Fadiga ma El Hadji Diouf wengi sana.
Vilevile nchi kama Mali nayo ilifaidika sana na programu za timu
za vijana na mwisho wa siku ikatengeneza wachezaji wengi sana tegemeo kwa
kikosi chake cha wakubwa kama vile Seydou Keita.
Wadau wa soka wa Tanzania pamoja na taasisi zinazosimamia mchezo
huo zinapaswa kujifunza kitu kutoka Michuano ya Chalenji hasa kuhusus uwekezaji
wa soka la vijana.
Nchi nyingi zimekuwa zikiitumia michuano hii kuzitengeneza timu
zao kwa ajili ya michuano mingine mikubwa kama ile ya AFCON na Kombe la Dunia.
Kulaumu Serikali hakuna tija tena kwani kila mdau ana nafasi yake.
Kabla ya kuilamu Serikali tujiulize kila mdau kwa nafasi yake amefanya
nini?
Lakini nini msaada wa klabu za Tanzania katika mchango huu ili
kuleta mageuzi ya mchezo huu hapa nchini. Ikumbukwe Ligi Kuu ndiyo chimbuko la
timu ya taifa, lakini je zina mkakati gani na timu za vijana? Nini mchango wake
kuinua soka?
Klabu hazina malengo mazuri kwa soka la Tanzania kwani ziko
kibiashara zaidi kuliko kuwa na mikakati ya kukuza kiwango na mchezo huo kwa
ujumla na badala yake zimekuwa zikishindwa kupata faida kwakuwa kiwango kiko
chini hivyo zinaishia kufanya vibaya tu.
Ni aibu kubwa sana kutumia mamilioni ya fedha lakini miaka nenda
rudi kiwango bado kiko chini tu badala ya kukua eti kinaporomoka tu.
Nchi kama Uganda iliyokuwa inanyanyaswa na Tanzania kuanzia ngazi
za klabu mpaka taifa leo hii imekuwa tishio kwa soka la nchini. Kilichowakomboa
ni kujitathimini na kuweka malengo ambayo yamefanukiwa kupitia hazina ya
uwekezaji wa soka la vijana.
Sasa ni wakati wa kuacha kuingiza siasa katika michezo hususani
soka. Msingi wa kuwa na timu bora ya taifa siku zijazo ni kuwa na mfumo
unaozalisha timu za vijana ambao kadri siku zinavyokwenda wanapata nafasi ya
kupandishwa.
Kuna ubaya gani wa kujifunza? Si vibaya kwa Tanzania kujifunza
kutoka kwa wengine hasa majirani zake wanaoonesha kila dalili ya kufanikiwa.
No comments