TATIZO NI MFUMO AU MAKOCHA WA KIGENI

INAWEZA kuwa mshtuko kama siyo zaidi ya utani kusikia kuwa eti idadi kubwa ya makocha wanaokuja nchini kufundisha timu ni wale wenye viwango vya chini sana. Hali hiyo ndiyo inayodaiwa kuchelewesha ukuaji wa viwango vya wachezaji na hatimaye kuzorotesha maendeleo ya timu ya taifa.


Inadaiwa idadi kubwa ya makocha wanaokuja nchini ni wale wenye elimu ya taaluma hiyo kidogo sana tena waliyoipata kwa kozi za viwango vya kawaida sana na hata wengine zikiwa ni za chini. 
Mtazamo huo unaweza kuwa pigo kwa wadau wengi wa soka ambao kwa sasa wana imani mabadiliko na mageuzi katika soka yataletwa na makocha wa kigeni hasa wale wa kutoka barani ulaya.

Hivi karibuni Kocha Mkuu wa muda wa timu ya soka ya taifa, ‘Taifa Stars’ na kocha msaidizi wa klabu ya Yanga, Charles Mkwassa alifunguka kuhusiana na aina ya makocha wanaokuja nchini kuwa siyo wale wa kiwango cha juu.

Katika kuonesha uchungu wake kutokana na suala hilo, Mkwasa alisema kinachowasaidia ni makocha hao kutoka katika nchi zilizopiga hatua kubwa katika masuala ya teknolojia hivyo kuitumia ipasavyo kujipatia kazi katika nchi zilizo nyuma kisoka ikiwemo Tanzania. Kwa maoni yake, makocha wenye viwango vya juu wapo isipokuwa hakuna klabu inayoweza kuchukua makocha hao kutokana na gharama zao kuwa kubwa sana. Ni kweli chochote kilicho bora na kizuri ni wazi kina gharama kubwa. Lakini ili ufike hatua hiyo ni lazima upitie katika hatua kama hizi.

Kauli hiyo ya Mkwasa inaweza kuwa na ukweli ndani yake lakini tujiulize hivi akiletwa kocha mwenye kariba ya Sir Alex Fergerson anaweza kuleta abadiliko katika mfumo huu huu wa soka Tanzania uliopo sasa? Nchi za jirani zetu zinapigaje hatua zikiwa na makocha wa kiwango kama hawa waliopo nchini kwetu, lakini kila ikija mechi Tanzania inapigwa?

Makocha kama Mosses Basena, Patrick Phiri, Jack Chamangwana, Mitcho nk ni baadhi ya makocha waliofundisha hapa nchini na sasa wako wanafundisha timu zingine katika nchi za ukanda huu wa Afrika Mashariki lakini wakipata mafanikio.


Sipingi fikra zake lakini pia hilo linaweza kuwa siyo tatizo sana hasa ikizingatiwa kuwa kuanzia klabu mpaka vyama vya soka migogoro na mivutano huchukua sana nafasi kuliko mipango ya maendeleo.
Zimeshuhudiwa timu zikifanya vizuri zikiwa na makocha wa aina hiyo. Mfano mzuri ni marehemu Tambwe Leya aliyeleta mafanikio kwa timu ya Yanga. Mwingine ni Cirvoci Milovan aliyeing’arisha Simba miaka iliyopita tu.
Kimsingi tukiachana na makocha tatizo kubwa la kutofanya vizuri kwa timu kadhaa ni mfumo mbovu wa soka kuanzia katika vilabu, vyama vya soka vya mikoa mpaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Tukiendelea na dhana ya kutafuta mchawi katika mazingira kama haya soka la Tanzania halitapata mageuzi na badala yake itabakia kulaumiana kwa kila mmoja kumnyooshea mwenzake kidole.


Lakini pia hata ukiangalia aina ya wachezaji  wanaochukuliwa na timu zetu toka nje ya nchi kuja kucheza nchini ni aina ya hao hao makocha tu.
Ndiyo hata wachezaji nao si ni hawa hawa wa gharama nafuu? Kwa sasa hakuna timu inayoweza kumchukua mchezaji japo wa Afrika tu mwenye gharama kubwa kama vile Tresso Mputu wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Hivyo basi hata aina ya makocha wanaokuja kufundisha ni wale wale wanaoendana na aina ya wachezaji waliopo au wanaozalishwa.
Kitu cha msingi ni usisitizwaji wa sera makini na zenye tija zitakazoleta mageuzi ya soka kuanzia chini katika klabu hadi taifa kuanzia kwa viongozi, waamuzi, makocha, wachezaji mpaka mashabiki.


Vile vile kuwepo na mipango ya muda mfupi na mrefu itakayozifanya klabu zijitegemee na kujiendesha hasa kibiashara kulingana na mfumo wa sasa wa soka duniani.
Ni kocha gani wa kiwango cha juu duniani atakayekubali kuja kufundisha katika timu ambayo haina msingi mzuri wa kuzalisha na kukuza wachezaji wake, kocha gani atakayekubali kufundisha wachezaji wasiojitambua na kujua thamani yao,vilevile hata mashabiki wake wakiwa ni wale wasiojielewa.


 Imeandaliwa na Asha Muhaji.

No comments

Powered by Blogger.