MWAKA WA MABADILIKO : TAIFA STARS YAIANGAMIZA MALAWI KUFUZU KOMBE LA DUNIA



Kauli mbiu ya Mwaka wa mabadiliko inazidi kushika kasi baada ya Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars kuiangamiza Malawi "The Flames" kwa bao 2-0.

Mechi hiyo ya kuwania nafasi ya kufuzu kucheza katika fainali za kombe la Dunia mwaka 2018 kule Russia ilipigwa katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.

Taifa Stars mpya ikiwa na kocha mzawa iliweza kucheza mpira safi na pasi fupi fupi na ikifanikiwa kupata bao la kwanza kupitia kwa Mbwana Samata aliyeitendea haki pasi ya Thomas Ulimwengu aliyewapiga chenga mabeki wa Malawi na kumtangulizia Samata ambaye hakufanya ajizi.

Bao la pili liliwekwa kimiani na Thomas Ulimwengu akitumia vizuri makosa ya kipa wa Malawi aliyeshindwa kuudaka mpira uliopigwa na beki wa pembeni wa Stars Haji Mwinyi.

Mpaka mapumziko Stars walikua mbele kwa bao hizo 2 na kipindi cha pili hakukua na nyongeza ya bao baada ya Stars kucheza kwa tahadhari kubwa huku kipa Ally Mustapha akiokoa michomo ya wazi na kufanya mchezo huo kumalizika kwa ushindi wa bao 2-0.

Mechi ya marudiano itapigwa nchini Malawi wikiendi hii na kama Stars watafanikiwa kupita hapa watakutana na Algeria katika hatua inayofata.

No comments

Powered by Blogger.