LIGIKUU TANZANIA BARA KUENDELEA WIKIENDI HII
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
(VPL) inatarajiwa kuendelea wikiendi hii kwa michezo sita kuchezwa katika
viwanja mbalimbali nchini, ikiwa katika mzunguko wa saba timu 14 zitapambana
kusaka pointi tatu muhimu.
Young Africans watawakaribisha Azam FC katika uwanja wa
Taifa jijini Dar es salaam siku ya Jumamosi, huku timu zote zikiwa na pointi 15
kileleni zikitofautiana kwa magoli ya kufunga na kufungwa.
Kabla ya mchezo wa Yanga dhidi ya Azam, kutakua na mchezo
wa utangulizi wa kuombea amani kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge
na Madiwani utakaofanyika Oktoba 25, 2015.
Mchezo huo utawakutanisha viongozi wa dini watakocheza
dhidi ya mabalozi wanaofanya kazi nchini, mechi hiyo itaanza saa 8:25 mchana na
kumalizika saa 9:15 alasiri.
Majimaji FC ya mkoani Ruvuma watakua wenyeji wa African
Sports kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea, huku Ndanda FC wakiwakaribisha
Toto African kutoka jijini Mwanza katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini
Mtwara.
Jijini Mbeya, watoza ushuru wa jijini hilo Mbeya City FC
watawakaribisha Simba SC katika uwanja wa Sokoine, Chama la wana Stand United
watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, huku
Coastal Union wagosi wa kaya wakiwakaribisha wakata miwa wa Mtibwa Sugar katika
uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Ligi hiyo itaendelea Jumapili kwa michezo miwili
kuchezwa, Mgambo Shooting watakua wenyeji wa Kagera Sugar katika uwanja wa
Mkwakwani, huku Mwadui FC wakicheza na maafande wa JKT Ruvu katika uwanja wa
Mwadui Complex.
No comments