JOSE MOURINHO, NI NADRA KUISHUHUDIA NADRA.
Kuna usemi wa kiingereza unaosema “when it rains, it pours”, tafsiri yake ni kuwa jambo lisiliokuwa jema likitokea basi huambatana na mengine mengi ndani ya muda mfupi. Eva Caneiro, kuwa nje ya kumi bora, ulinzi mbovu na kiwango kibovu kwa ujumla ni kati ya mambo yanayoweza kukupa maana halisi ya huu usemi kwa maisha ya sasa ya kocha kichaa Jose Mourinho. Kuna nyakati hata binti mrembo huota upele, na nakshi yake huwa imeathirika. Ukitizama sura ya Jose Mourinho haijabadili ukaidi wake lakini walau unaweza kuamini kuwa hata Adolf Hitler kuna muda alihitaji huruma ya watu achilia mbali ukatili wake. Ndipo alipo mtu huyu mwenye maneno mengi. Unahitaji sababu zipi kujua kuwa yupo katika wakati mgumu? Kipindi kama hiki msimu uliopita alikuwa hakamatiki, kipindi kama hiki msimu uliopita Diego Costa alikuwa ni kanali wa majeshi ya anga pale Chelsea, na Terry aliongoza JWTZ yao pale nyuma. Edo Kumwembe moja ya waandishi bora zaidi Tanzania hupenda kusema maisha bila unafki hayendi. Ni Mourinho huyu leo anayeamini anatakiwa kuongezwa muda sio kwa kiwango cha sasa bali kwa alichowapa msimu uliomalizika.
Lakini ukweli unabaki kuwa hakuna mwanadamu anayeweza kutizama nyuma ya kisogo chake. Huu unaweza kuwa moja ya misimu mibaya katika maisha yake, kila alichogusa zamani kiligeuka dhahabu sasa lakini sasa ni tofauti, bahati mbaya hata aliowaamini muda wote nao hawampi kile alichotaraji. Mwanzo wa msimu ilikuwa ni rahisi kutabiri Marekani itafilisika kuliko Mourinho kufika katika nafasi ya 15, ungefanya hivyo ungekuwa na kila dalili ya kuhitaji daktari wa akili. Lakini watu wengi au wachambuzi wanamsema Mourinho, unajua kwanini? Jibu ni rahisi tu, huu ni upande mgumu sana kuhushuhudia kwa Mourinho, hiki ni kitu nadra sana kukiona kwa Jose Mourinho. Utamkuta vipi huko chini wakati anasajili anavyotaka, anasuka ulinzi kwa umakini kupita kiasi. Kwake yeye ni dhambi kubwa kufunga goli tatu kisha ukafungwa moja. Huyu ndiye kocha pekee anayeuishi usemi wa “ Offense gives you wins, Defense gives you Championships” (ushambuliaji utakupa ushindi lakini ulinzi utakupa vikombe). Yeye anamuhitaji zaidi Cahill aliyekuwa bora kuliko Willian, yeye anatamani zaidi Terry na Ivanovic warudi kwenye ubora kabla ya Hazard na Diego Costa. Ndio maana alihitaji magoli 73 tu kuchukua ubingwa dhidi ya Man City iliyofunga magoli 83. Ndio jibu ni Ulinzi pekee.
Na hili ndilo jambo kubwa zaidi linalomtesa Mourinho. Ile staili yake ya kuwakera watu kwa kukaba muda mwingi kuliko kushambulia imekwama, ile staili iliyomfanya aigeuze Inter Milan ya vibabu kuonekana miamba imegoma, Ngalawa imeshindwa kufuata upepo na sasa mawimbi yanaipeleka yanapotaka kwenda. Yupo katikati ya bahari chafu ambayo manahodha wengi hupata hofu nayo. Kila nikitizama Chelsea wanavyocheza naona Mourinho anajaribu kitu kipya. Alihisi Terry kachoka, akahisi Zouma anafaa, akahitaji Ramirez apunguze mzigo kwa Matic lakini bahati mbaya hata betri anazotumia Fabregas nazo zimepitwa muda wake. Timu nzima haina muunganiko sahihi, na ndio maana hata nyongeza za akina Pedro hazionekani kwenda na wakati. Wanaonekana wameshindwa (flops), na kitendo cha kutokuwepo kwa utulivu kwenye vyumba vya kubadili nguo ndio hatari zaidi. Hili ndilo eneo nyeti zaidi ambalo klabu inatakiwa kuwa na mshikamano nalo, hili ndilo eneo nyeti ambalo klabu hupoteza matoeko kama halieleweki. Hili ndilo eneo ambalo ni msingi wa uwezo wa timu uwanjani, lisipokuwa sawa maana yake hakuna maelewano ndani ya uwanja na nje ya uwanja kati ya viongozi mpaka kwa wachezaji.
Kwenye wakati kama huu Mourinho alihitaji wachezaji wake bora wacheze katika hali ya kunusuru maisha na mwenendo wa klabu, alihitaji Costa asifungiwe na aendelee kufunga, akahitaji Hazard aendelee kuwa walau wa msimu uliopita achilia mbali kufananishwa na Ronaldo, na pia Fabregas atoe assists kama msimu uliopita. Lakini haya yote yapo kushoto, kulia kwake ni Willian tu ndio anayefanya ustadi bora maradufu, mchezaji ambaye hajawahi kuwa mfungaji mzuri. Mpangilio wa kuizuia Chelsea umekuwa rahisi zaidi kwani meno yaliyotumika kung’ata msimu jana yameota kutu au ubutu. Safu yako ya ushambuliaji siku zote isipofanya kazi basi presha huwafikia walinzi na golikipa. Wataokoa sana na pia watafungwa sana, Fabregas na Hazard wasiposambaza mipira na kusogea kwa adui inavyopaswa basi Matic ataonekana si lolote, na ndicho kinachoendelea.
Nyakati kama hizi huwa ni nzuri sana kuzishuhudia katika soka, ni nyakati ambazo jeuri hupisha huruma ifanye kazi yake, ni nyakati ambazo jeuri hujiandaa kutoka kwa kasi ikipata nafasi. Hutoziona mara nyingi kamwe, kuishuhudia sura ya Abramovich ikiwa imejikunja katika chumba maalumu pale Stamford Bridge mfululizo ni jambo gumu hasa, kumuona Mourinho akiwa hacheki wala kununa ni jambo gumu pia. Najaribu kukusanya viganja vyangu nihesabu ni mara ngapi Mourinho kaishi hivi bado sina kumbukumbu nzuri, ni nadra na itabaki kuwa nadra sana. Ni kma ambavyo ni nadra kuona Abramovich akiendelea kuwa kimya pamoja na huu mwenenndo. Maisha ya soka ndivyo yalivyo, unakuwa na imani kabisa haya hayawezi kuwa maisha yamuda mrefu chini ya Jose Mourinho, yataisha karibuni tu. Ni vipindi nadra sana kuviona, uliona Hazard anaingia dakika ya 80? Yule ndiye Mourinho ninayemfahamu, anayeamini kuwa kabla yake hakuna mkubwa kumzidi, hata mmiliki wa klabu anatakiwa kumsikiliza yeye. Huyu aliyekuwa kimya hapa katikati ni nadra na tunaweza tusimwone tena, hii Chelsea tunaweza tusikute tena huko kwa mwongo mzima. Ni nadra sana kuziona nadra hizi, hata sura za mashabiki wa Chelsea nina imani zitacheka sio muda mrefu, chini ya Mourinho sura ya shabiki haikunjamani.
Ahsanteni , By Nicasius N Agwanda ( Nicasius Coutinho Suso)
Instagram: @Nicas.coutinho
No comments