APER ARDUA AD ASTRA BRENDAN RODGERS
Katika miaka ya 1912 ikiwa ni miaka kumi kabla ya kuzaliwa baba wa taifa hili Mwl. Julius K Nyerere, majeshi ya angani ya Uingereza chini ya kanali Frederick Sykes walipendekeza kutafutwe kauli mbiu ambayo ingewapa morali wanajeshi kupambana katika vita mbalimbali. Ni kipindi hiki ambacho maneno haya manne maarufu Per Ardua Ad Astra yalipopatikana na kuanza kufanya kazi yakiwa na maana ya KUPITIA MAGUMU MPAKA KUZIFIKIA NYOTA. Maana kubwa ikiwa ni kupigana kwa hali na mali kufikia mafanikio tarajiwa. Hii ni kauli ambayo kocha aliyeondolewa karibuni katika klabu ya Liverpool, Brendan Rodgers aliamua kuipa kipaumbele mpaka kuweka maneno hayo katika mlango wa kuingilia ofisi ya kocha wa Swansea.
Ndio, anabakia kuwa kati ya makocha wachache waumini wa falsafa mbalimbali zilizotumika kipindi cha nyuma. Pengine kazi ya Liverpool ilikuja kwake mapema sana, lakini kwa sasa dunia imetawaliwa na wingi wa makocha wengi vijana wenye mbinu, na wenye kuliteka hasa soka la kisasa. Hakuna siri kuwa hakuwahi kuwa chaguo la kwanza la wamiliki wa Liverpool lakini ukweli mwingine ni kuwa ndiye kocha pekee aliyekuwa anaendana ama kukubaliana na mipango na sera za klabu hiyo na wamiliki wake wakiongozwa na John Henry na Tom Werner hasa sera yao ya money ball.
Kama kuna kosa kubwa alilowahi kufanya Brendan Rodgers basi sio jingine bali ni pale ambapo ubongo wake uliamua kukataa kufanya kazi na Director Of Football (mkurugenzi wa mpira) na kuamua kukubaliana na Transfer Committee (kamati ya usajili). Vilabu vingi vimefanikiwa na makocha wengi wamefanikiwa hasa makocha vijana kwa kuwa na wasaidizi/viongozi wazoefu nyuma yao ambao husimamia mpira wa klabu kwa ujumla wake. Brendan Rodgers aliamini katika kichwa chake zaidi na kutaka kuwa kiongozi kamili lakini akasahau kuwa kamati ni kitu hatari zaidi ukizingatia kuwa kimsingi inaonekana sio kocha bora katika kutambua vipaji vinavyoendana na mifumo na falsafa zake.
Wakati anaamua kuichukua Liverpool chini ya kamati ya usajili, Rodgers aliamua kubeba mizigo ifuatayo. Mosi ni Liverpool iliyopotea kwa misimu takribani minne pasipo kurudi katika nafasi zake, hivyo alivaa vazi lililoshuka thamani kwa kiasi kikubwa. Pili alitakiwa kuthibitisha kuwa Liverpool ilikuwa sahihi kumfukuza mzoefu na mfalme wao Daglish, na tatu kumkumbatia rafiki mnafki Transfer Committee. Rodgers alisahau kuwa huyu rafiki alomchagua hakuwa katika nafasi mbaya hata kidogo, timu ikifanya vyema wangesifiwa wote, timu ikifanya vibaya angetizamwa peke yake.
Kufukuzwa kwa Rodgers kumechelewa, usalama wake ulitakiwa ukome pale Britannia stadium msimu ulioisha baada ya kufungwa goli 6. Timu ilikosa morali ya msimu mmoja uliopita, timu ilishuka kitakwimu katika maeneo mengi tangu ameichukua timu, kuanzia umiliki wa mpira mpaka idadi ya magoli. Pia ndio msimu ambao Liverpool ilitumia pesa nyingi zaidi kusajili wachezaji kuliko kipindi kingine chochote na wengi wakiwa aliowapendekeza yeye ikiwa ni baada ya kelele nyingi za kuingiliwa kimajukumu na wachambuzi na mashabiki.
Imani yangu ni kuwa wamiliki walikuwa na mawazo kama yangu, inawezekana ni bahati mbaya kama zilivyo bahati mbaya nyingine. Inawezekana aliwakosa Sturridge na Suarez kwa wakati mmoja. Inawezekana Gerrard hakuwa yule tena. Ndio tafsiri nyepesi zaidi unayoweza kuitengeneza. Lakini ukweli unabaki kuwa Rodgers ni kocha bora sana katika kufundisha mbinu na kuziweka uwanjani kwa wachezaji kuliko kupata wachezaji wake sahihi. Ndipo ninapopata imani kuwa angefanya vizuri zaidi chini ya director of football kuliko transfer committee. Bahati mbaya ni kuwa anabaki kuwa moja ya binadamu wabishi zaidi duniani, hata timu inapopoteza huamini kuwa kuna chanya ndani yake imeonekana, yaani atasifia chanya mbili hata kama kuna hasi nane zimeonekana pia.
Liverpool ilikwisha mshinda nguvu, ukiona uwanja wa anfield mechi inaanza ukiwa tupu ujue kuwa hutakiwi pale,ukiona goli linafungwa na kelele zinatoka upande wa Kop End pekee basi ujue wale watata wa Spion kop hawataki hata kukusikia. Ule unabaki kuwa moja ya viwanja vyenye mashabiki loyal (waaminifu) zaidi duniani. Mwingine ni ule wa Signal Iduna Park kule kwa Dortmund, na ile hekalu la Wenger pale Emirates.
Bado sina tatizo na Rodgers, makocha wanaajiriwa ili wafukuzwe, lakini bado anauzika sana, mvuto wake haujapata ukomo. Kuna mambo mawili kwa sasa, wakati anakula bata zake Hispania atizame kwa macho mawili ile timu ya taifa ya Uingereza kunamfaa kule sana. Lakini asikimbilie kwa kina sunderland. Ndio wakati anaandika yale maneno mbele ya mlango wake Swansea naamini aliyajua haya. Nami namwambia lazima tupitie magumu mpaka kuzifikia nyota, aendelee tu kuwa mbishi kama alomkopa hayo maneno kanali Frederick Sykes, kama hatoniamini akasome safari ya mrithi wake Jurgen Klopp akiwa Mainz 05 kabla ya Dortmund ilikuwaje.
Ahsanteni, by Nicasius N Agwanda ( Nicasius Coutinho Suso)
Instagram @Nicas.coutinho
No comments