KARIBU VITANI FIRMINO,KLEBERSON AMEKUPA SALAMU?!

Wakati ukuta na nyakati zinaenda na kupita ni majuma mawili sasa kila ukiingia katika mitandao mingi ya kijamii mashabiki wengi wa Liverpool wanafurahia usajili wa fundi wa kibrazili Roberto Firmino,unaanzaje kununa wakati una uhakika atakutengenezea nafasi nyingi zaidi za kufunga akishirikiana na mbrazili mwingine fundi Felipe Coutinho,mtegemee akishindana na Cesc,Di Maria katika chati za kutengeneza mabao kitu kinachowapa faraja zaidi ya moyo mashabiki wa timu hiyo na ni wakati huu hata wacheza kamari wanaanza kuitamani Liverpool na kuiwekea mizigo ligi itakapoanza

Usajili wa mchezaji huyu na matumaini lukuki juu yake yananirudisha miaka 12 nyuma wakati ambao klabu ya Manchester United ilimsajili kiungo wa kibrazili Jose Kleberson aliyekuwa na miaka 23 tu huku akiwa na medali ya kombe la dunia katika kabati lake ambapo aliitwa baada ya kiungo Emerson kuumia katika mazoezi na kuchukua nafasi yake..ushirikiano wake na pacha wake Gilberto Silva uliwafanya Cafu na Carlos watembee wanavyotaka pembeni mwa uwanja huku hadaa za Juninho,Ronaldinho na Rivaldo zikimwacha El Phenomenon kuwa na kazi rahisi kabisa..Bahati mbaya kwa kwa Kleberson hakusajiliwa baada ya fainali za kombe la dunia  kuisha kama ilivyokuwa kwa pacha wake Gilberto Silva aliyeenda Arsenal yeye alibaki kwao kwa msimu mmoja zaidi kabla United hawajamchukua.

Katika umri ule ule na  matarajio yale yale Firmino tutakua nae kwenye ligi ya Uingereza msimu ujao lakini yeye akiwa katika hali na nafasi nzuri zaidi kuliko wakati ule wa Kleberson ambaye alikuwa mhimili katika kikosi cha Brazil kilichotwaa ubingwa wa dunia inasemwa alikuwa katika wachezaji watatu waliofanya vizuri zaidi ndani ya kikosi kile na pengine alipoenda United ilibidi apambane na Roy Keane,Paul Scholes,Nick Butt,Beckham,Ronaldo na Fletcher ukimtoa Giggs kwani kuna wakati  SAF alimtumia kama winga wa kukaba upande wa kulia au nyuma ya mshambuliaji nafasi ambazo hakuzimudu na kuishia kucheza mechi 20 tu katika misimu miwili huku akiandamwa na majeraha ya mara kwa mara pamoja na kwamba alikua ni mtu wa shoka.

Usimuangalie Coutinho ambaye alikuja kinda kabisa na kujiaminisha Firmino atang'aa moja kwa moja usajili wake haukuwa na msukumo sana kama huu ambao mashabiki hawa walioonja tamu ya kukaa  kileleni mwa ligi na kukaribia kuchukua kombe hilo wana matarajio na usajili kama Firmino kuwarudisha huko..namtazama kijana huyu wa kibrazili ambaye amebeba kila kifaa cha vita katika mkoba wake kuelekea vitani..ametoka kwenye ligi yenye kasi na ubabe wa kina Hojberg amekuja kwenye kasi zaidi na ubabe wa timu nzima hili atalijua siku atakayokanyaga pale Brittania..wakati Kleberson alikua ni mchezaji wa shoka zaidi aliyeshindwa kumudu ligi ya Uingereza Firmino yeye ana soka tamu ambalo ukiligeuza kuwa maneno utamg'oa hata yule binti wa Paul Kagame..karibu kwa wahuni na salamu za kaka yako Kleberson

Imeandikwa na Bilali

No comments

Powered by Blogger.