MAMBO KUMI NILIYOJIFUNZA BAADA FAINALI YA LIGI YA MABINGWA ULAYA
1. Claudio Marchisio ni mchezaji bora zaidi asiyetajwa zaidi katika mashindano haya. Huyu ndio roho ya Juventus katika kiungo kuliko mwingine yeyote, ni rahisi kwa wao kumuuza Pogba kuliko huyu, bahati mbaya sana hana walau staili ya nywele kama wenzie, angeshamulikwa sana, si ajabu ukamkosa hata kwenye kikosi cha Uefa.
2. Neymar ana tabia na harufu ya Ballon D'or. Neymar atabaki kuwa mchezaji anayenufaika zaidi katika Muunganiko wa MSN. Ndiye mchezaji ambaye uzito wa kumkaba haukaziwi kutokana na uwepo wa wale watu wengine wawili. Usitegemee ataacha kufunga, kama Kaka zake wataendelea kuishi pale Barcelona naye ataendelea kuwa mfungaji bora zaidi, bahati nzuri kule kwao nako anafanya vyema. Hii ndio tofauti yake na Hazard, Hazard anatakiwa ajifunze kufunga zaidi, wakati Neymar anatakiwa azoee kufunga zaidi. Hana muda mrefu kwenye Ile tuzo akiendelea hivi.
3. Dani Alves? Hapana yule Lichtensteiner anakupa unachokitaka. Anakukaba, anakufanyia uhuni, halafu anakushambulia. Beki bora wa upande wa kulia kwa Sasa. Muda mwingine hakuna lililo sahihi katika ulimwengu huu, natamani kujua mshahara wake huyu kisha nikatizame na ule wa Sagna pale Man City.
4. Naendelea kuhesabu na naomba Mungu anipe afya nimtizame De Gea akifikisha miaka 37. Si ajabu atakuwa kastaafu, ule umahiri wa Gigi Buffon ni wa kipekee, katika umri ule kumkosesha amani Suarez unatakiwa uwe kipaji hasa. Cha kustaajisha anaonekana anatakiwa kuwepo pale hata miaka 3 ya nyongeza. Kuna baadhi ya watu wanastahiki tuzo ya heshima tu.
5. Kuna wakati maisha yanahitaji bahati kama ya Gerrard Pique. Utaendelea kununa tu yeye kuingizwa kwenye vikosi bora lakini ataendelea kuwepo na anastahiki. Sio kwa sababu ana uwezo wa Koscielny wa Arsenal ila kwa sababu ameishi Barcelona ya Messi na Iniesta, Xavi na Sasa Suarez.
6. Walikuwepo akina Riquelme, Figo, Zidane, Scholes, Gerrard, Lampard, Ronaldinho, Pirlo, Kisha Xavi na Muda sio mrefu Iniesta. Bahati mbaya sana nipo katika dunia ambayo hata Jordan Henderson na Ramsey wanaonekana wanastahiki kucheza Barcelona. Lile tabasamu Kati ya Pirlo na Xavi ilikuwa kwaheri nzuri sana.
7. Pep Guardiola alitengeneza Barcelona iliyokuwa inakukera unayecheza naye, Luis Enrique katengeneza Barcelona inayokusisimua unayecheza naye. Napata shida kuamua ipi bora zaidi.
8. Kama Jana ingekuwa mwaka jana, Real Madrid isingemuuza moja kwa moja Morata, Wenger angeongeza dau wakati anamtaka, na Del Bosque asingemuacha timu ya taifa. Baada ya kumsajili Dybala, Juventus wanaweza kumuachia sasa Tevez, yule Morata kakomaa kabla ya muda wake, na saa ingekuwa inaweza kusogezwa mbele haraka Perez angemrudisha haraka nyumbani.
9. Babu yangu alimshuhudia Pele, Baba yangu alimfaidi Maradona, mimi hapa najivunia kumuona Lionel Messi. Wengi wanaweza kusema Jana hakuonekana sana lakini huyu ndio chanzo cha ushindi. Anakuwepo pale unapomtaka, lile goli la Suarez Jana ni uwezo binafsi wa Lionel Messi. Bahati iliyoje ndo kwanza ana miaka 28. Huyu alikomaa akiwa tumboni.
10. Niseme nini. Ulitaka Real Madrid awe pale jana? Ulitaka iwe Ronaldo V Messi. Hii inaweza kuwa chachu ya kurejesha ubora wa Serie A. Ni aibu kumtamkia mdogo wangu au mwanao wewe uliyebahatika kupata miaka Hii mitano kuwa Serie A hii ndo ilishuhudia Maldini, Van Basten, Del Piero, mpaka kwa kina Ricardo Kaka. Serie A ambayo Gervinho ni star wa kutupwa.
NB.
Sergio Busquet angekuwa na tabia za Matic au jirani yake yule Mascherano angekuwa ni moja ya watu wanaokubalika zaidi, tatizo lake ni mkimya sana kiuchezaji, hana fujo. Na Ile tabia yake ya kumfanya refa kuamini kuwa baadhi ya wachezaji wamebeba nyundo uwanjani ndo mbovu zaidi, ni mdanganyifu sana.
Ahsanteni.
By Nicasius Coutinho Suso
No comments