KOCHA STARS ATOA SABABU ZA KUFUNGWA NA SWAZILAND
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imepoteza mchezo wake wa kwanza wa michuano ya COSAFA Castel Cup dhidi ya timu ya Taifa ya Swaziland, baada ya kufungwa bao 1- 0 mchezo uliochezwa katika uwanja wa Royal Bafokeng jijini Rustenburg.
Stars ilipoteza nafasi zaidi ya tano kipindi cha kwanza kupitia kwa washambuliaji wake Saimon Msuva na nahodha John Bocco ambao walishindwa kukwamisha mpira wavuni katika kipindi cha kwanza, ambacho Taifa Stars ilicheza vizuri.
Swaziland walipata bao lao la kwanza na la ushindi dakika ya 42 ya mchezo, kupitia kwa mlinzi wa kulia Sifiso Mabila aliyepanda kuongeza nguvu ya mashambulizi na kuachia shuti lililouacha mlinda mlango wa Stars akikosa cha kufanya kuokoa mchomo huo.
Kipindi cha pili Stars walizidiwa kwani mashambulizi yao hayakua na madhara langoni mwa Swaziland na kumuacha mlinda mlango Mphikeleli Dlamnini akiwa likizo kwa muda mrefu.
Mara baada ya mchezo kocha wa Stars Mart Nooij alisema, amepoteza mchezo wa kwanza ambao alitegemea kupata ushindi, vijana walicheza vizuri kipindi cha kwanza, lakini bao la mapema lilionekana kuwapoteza mchezoni.
“Presha ya mchezo ilikua kubwa hasa kipindi cha pili, kutokana na vijana wangu kucheza kwa kusaka bao, huku Swaziland wakimiliki zaidi mpira na kukuta mipango yetu kutokua na madhara” alisema Nooi.
Akiongelea michuano ya COSAFA amesema anashukuru kwa kupata mwaliko huu, kwani kwake anatumia michuano hii kama sehemu ya maandalizi ya kuwania kufuzu kwa fainali za mataifa Afrika (AFCON, CHAN) mwezi juni, huku akisema anaamini wachezaji aliowacha majeruhi nyumbani pamoja na wachezaji wa kimataifa wanaochezea klabu ya TP Mazembe, wataongeza nguvu katika kikosi chake watakaporejea Tanzania.
Baadhi ya watanzania waishio nchini Afrika Kusini walijitokeza uwanja wa Royal Bafokeng kuishangilia timu ya Taifa ya tanznaia Taifa Stars wakiwa sambamba na maofisa wa ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini.
Taifa Stars itacheza mchezo wake wa pili siku ya jumatano saa 11 za jioni kwa saa za Afrika kusini, sawa na saa 12 jioni kwa saa za Afrika Mashariki dhidi ya Madagascar katika uwanja wa Royal Bafokeng., ambao katika mchezo wa awali wamibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Lesotho.
Wakati huo huo kiungo wa Taifa Sars Said Juma “Makapu” ambaye anasumbuliwa na majeruhi, anatarajiwa kurejea nyumbani Tanzania leo kwa ajili ya kupata vipimo zaidi na matibabu.
No comments