MIWANI PANA YA EDO ~ DAKIKA 20 ZA KUMMALIZA MTANI TAIFA.



Pambano la Watani wa jadi wa soka la Tanzania Simba na Yanga litapigwa leo Jumamosi katika dimba la Taifa Jijini Dar Es Salaam.
Tofauti na michezo mingine ya watani hao wa jadi mchezo huu unaweza kuleta balaa kubwa kwa Simba kwani licha ya kuanza kwa kusuasua lakini timu imegawanyika katika makundi mawili kuna wanaomuunga Mkono Rais wa klabu hiyo Evans Aveva na uongozi wake na wale ambao hawakubaliani na maamuzi ya Rais huyo kuwatimua baadhi ya Wanachama ambao walienda Mahakamani kupinga kuenguliwa kwa Michael Wambura katika uchaguzi mkuu uliopita ambao wanajiita UKAWA.

Sasa Simba inaingiwa uwanjani ikiwa imejigawa nje ya uwanja hali ambayo wataalamu wa mambo wanasema inaweza kuaathiri matokeo ya ndani ya uwanja japokua linapokuaja swala la mechi ya Simba na Yanga mambo huwa tofauti sana na hali halisi.



Nakumbuka katika mechi ya Mtani Jembe mwaka jana Simba iliingia ikiwa na matatizo lukuki nje ya uwanja hasa kuhusu aliyekua mwenyekiti wa Klabu hiyo Ismail Aden Rage ambaye mashabiki waliona anawazingua kuhusu uhamisho tata wa Okwi kwenda Yanga lakini baada ya dakika 20 tu za mchezo huo tayari Simba walishatupa mabango ya kutokua na Imani na Rage. Kwani walijikuta wakishangilia magoli matatu dhidi ya moja la Yanga na kusahau shida za siku hiyo.

Mchezo wa wa leo Jumamosi unazikutanisha Timu ambazo kuna mabadiliko mengi yamepita.
Kama kawaida ya timu hizi kupenda sifa kwa kushindana kusajili na kubadili makocha na ndicho kilichotokea wakati msimu huu unaanza.

Wakati Arsenal inakimbizana na majeruhi kikosini wakiwa wameshapata majeruhi zaidi ya laki 8 tangu mwaka 2002 pengine ikionekana ndo sababu kubwa iliyochangia kushindwa kupata kombe lolote kwa kipindi hicho huku Tanzania mambo ni tofauti kushindwa kufurukuta kwa vilabu hivi mara zote hutokana na mabadiliko ya mara kwa mara na sio majeruhi kama Arsenal.

Wakati timu kubwa za Ulaya zikiwapa makocha na wachezaji mikataba ya muda mrefu hapa kwetu hali ni tofauti kwani mawazo ya hizi klabu zetu ni matokeo mazuri ya mechi ya watani wa jadi na hapo utakuta kila msimu kikosi kinabadilika.
Yuko wapi Musoti,Christopher Edward n.k

Wakati Yanga wao wakibadilisha kabisa benchi la Ufundi tangu kocha mkuu mpaka wasaidizi wake ambao wameamua kumleta Maximo na msaidizi wake wote Wabrazil hawa upande wa Watani zao Simba wao wamebadili tu kocha mkuu Patrick Phiri Mzambia huyu akichukua uongozi lakini Simba imeleta wachezaji wengi wageni kikosini tofauti na msimu uliopita.

Mpaka mwalimu wa Hisabati na Fizikia pale Tambaza ambaye atakua refa wa mechi hiyo atapuliza filimbi  kuanza pambano hilo Yanga wameshapata pointi 6 katika mechi 3 walizocheza huku wakiwa wameshafunga magoli manne na kufungwa magoli manne, wanakamata nafasi ya 3 wakiwa wameshinda mechi mbili na kufungwa mechi moja.
Simba wao wanakamata nafasi ya 10 wakiwa na pointi 3 baada ya kutoka sare michezo yake  yote ikiwa imeshafunga magoli manne na kufungwa magoli manne pia.

TAKWIMU ZINASEMAJE?


Katika mechi 6 zilizopita baina ya timu hizo Simba imeshinda mechi 2 ikiwemo ushindi  Maarufu wa bao 5-0 ambao ulikua katika mechi ya mwisho wa ligi msimu wa mwaka 2012/2013 na ule ushindi wa mechi ya mtani Jembe ambapo Yanga ililala kwa bao 3-1.

Kwa Upande wao Yanga wameshinda mechi moja baina ya timu hizo ikishinda bao 2-0 katika ligi na mechi mbili ziliisha kwa sare ya bao 1-1.
Simba imefunga Jumla ya magoli 13 huku Yanga ikifunga magoli 8 katika mechi hizo 6.

Matokeo ya Mechi 6 zilizopita za Watani wa Jadi
Simba 5-0 Yanga
Simba 1-1 Yanga
Simba 0-2 Yanga
Simba 3-3 Yanga
Simba 3-1 Yanga ( Mtani Jembe)
Simba 1-1 Yanga

MATARAJIO KATIKA MECHI HIYO.


Mimi Edo naamini dakika 20 za mwanzo ndizo zitakazoamua nani atakua mshindi katika mechi hiyo.

Upande wa Simba kama watafunga goli ndani ya dakika hizo zitaamsha kelele na kuwapa hamasa wachezaji wakiamini Safari ya Afrika Kusini ilikua na manufaa mno kwao na hii pengine inaweza kuwapoteza kabiaa Yanga mchezoni kwani wanaweza kupanic na kudhani Kule Afrika Kusini kulikua na kitu cha ajabu.
Kama ningeweza kuwasiliana na Phiri ningemshauri ampange Kiemba aanze na Tambwe pale mbele halafu Okwi na Singano waanzie mashambulizi pembeni kama winga.

Kwa upande wa Yanga dakika hizo hizo 20 za mwanzo zinaweza kuwasaidia kushinda mechi hiyo tena kwa mabao mengi kwani kama Yanga watapata bao la mapema itawahamasisha wachezaji na mashabiki kutaka kuwaambia Simba walienda "Bondeni" kuogelea tu na sio kucheza mpira.
Maximo anapaswa kutambua Jaja sio msaada sana kwa timu inayohitaji ushindi na hapo ndipo ninapodhani kuwa Simon Msuva angekua bora sana kuanza pale mbele acheze na Kiiza kama wako fiti. Yanga inahitaji watu wajanja kuihadaa ngome ya Simba na kuzitumia vyema krosi za Ngasa.

Yote kwa Yote pambano la leo linaweza kuwa kali mno kuwahi kutokea ila ikumbukwe DAKIKA 20 ZA MWANZO NI MUHIMU KUMUUA MTANI

Asanteni.......

Edo Daniel Chibo : C.E.O Wapenda Soka
Www.facebook.com/wapendasoka-kandanda
mobile: 0715 127272
×××××××××××××××××××××××××××××××××××××××××××××××××××××××××××××××××

No comments

Powered by Blogger.