AMRI  KIEMBA NA SURA MBILI ZA FRANK LAMPARD.

         
Ukiniuliza kiungo bora Duniani niliyewahi kumshuhudia akicheza mpira sitasita kumtaja Frank Lampard.Kiungo mwenye nguvu,stamina ya kutosha,Pasi za uhakika bila kuusahau mguu wake ambao ni rafiki wa nyavu.Frank lampard ni kiungo aliyefunga magoli mengi kwenye historia ya soka. Ameifungia Chelsea magoli zaidi ya 200,Kwenye ngazi ya klabu hakuna alichokibakiza baada ya kushinda karibu kila kombe akiwa na Chelsea.

           Huyo ndio Super Frank Lampard,Kiungo mwenye sura mbili.Sura ya kwanza akiwa na timu za vilabu na sura ya pili akiwa kwenye timu ya Taifa ya Uingereza.Alipokua akiitumikia Chelsea alikua roho ya Chelsea,siku asipokuwepo frank lampard  lazima utagundua udhaifu wa Chelsea.
Mafanikio yake ya kuwa mchezaji bora wa Dunia na Mchezaji bora wa ulaya nyuma ya Ronaldiho mwaka 2005 yote aliyapata akiwa kwenye sura yake ya kwanza na Chelsea. Lakini Frank Lampard yule yule wa Chelsea anakuwa tofauti na lampard wa Timu ya Taifa ya uingereza.Lampard wa uingereza amefeli.Ameshindwa kuwapa waingereza kile walichokiona anawapa Chelsea.Mpaka mwaka huu anastaafu kuchezea timu ya taifa hakuna cha ziada alichofanya kuwashawishi Waingereza wamkumbuke kama mmoja wa mashujaa wa timu ya taifa ya uingereza.Hiyo ndio sura ya pili ya Frank Lampard,Ni tofauti na ile sura yake ya kwanza ya ushujaa,sura yake hii ya pili imekuwa karaha kwa waingereza.



           Jamie Redknapp,Mchezaji  wa zamani wa uingereza na mmoja wa wachambuzi bora Duniani,Yeye ni miongoni mwa watu walioumia kwa kustaafu kwa lampard bila ya mafanikio yoyote akiwa na timu ya Taifa.Redknapp anawatupia zaidi lawama makocha wa Lampard ,Ericksson,Cappello na Mc Claren.Anaamini hawa ndio walisababisha kufeli kwa Lampard.Tatizo la Lampard timu ya Taifa ilikua ni mfumo,haswa ule wa  kumlazimisha acheze na Gerald  kwenye sehemu ya kiungo.Licha ya kukosa maelewano bado Makocha hao walikua wakiwalazimisha jambo lililopelekea tukose kuuona ubora wa Lampard akiwa na timu ya taifa.

          Huku kwetu Tanzania yupo kiungo anayevaa sura mbili kama Frank Lampard.Huyu si mwingine bali ni Amri Kiemba.Licha ya kuwa umri umemtupa mkono lakini bado mguu wake unataka kucheza mpira.Licha ya damu yake kupoa lakini bado ubongo wake unafanya kazi vizuri.Amri kiemba ni miongoni wa viungo bora kuwai kutokea nchini.

Kiemba licha ya kupata mafanikio akiwa na timu za Yanga na Simba lakini sasa anaonekana kuchoka akiwa kwenye klabu yake ya Simba.Kiemba amekuwa si lolote si chochote kwenye kikosi cha Patrick Phiri.Lakini Juzi wakati Taifa stars wanacheza na Benin niliiona sura ya pili ya kiemba kwa dakika alizocheza.Mpaka kipindi cha kwanza kinaisha alikua mmoja wachezaji wangu wa3 bora wa kipindi hicho cha kwanza.Ukiachana na goli lake murua alilofunga alikuwa msaada mkubwa kwenye timu haswa kwenye kuunganisha mashambulizi ya timu.Kiemba niliyemuona dhidi ya benin amenifanya niamini kuna kiemba wawili,Kiemba wa Simba na Kiemba wa Stars.

            Nafahamu takribani misimu miwili iliyopita timu ya simba ilijengwa kupitia kwa kiemba.Lakini mimi namzungumzia kiemba wa msimu huu anayepewa dakika 10 mpaka 20 tu  na kocha phiri.Katika mechi zote za Simba msimu huu Amri Kiemba ametumika kama mchezaji wa akiba na hakuna hata mechi moja aliyoingia na kuleta uhai kwenye timu ya simba.Amekuwa kiemba mwenye kiwango kibovu kuwai kumshuhudia akiwa kwenye vilabu.Lakini nikenda mbali nikagundua kuwa kiemba anavyotumiwa simba ni tofauti na kocha wa stars anavyomtumia.

           Kocha wa Stars amegundua kiemba wa sasa umri umekwenda,hana pumzi wala kasi aliyokua nayo miaka mitatu iliyopita.Alichokifanya kocha wa Stars ni kuweka watu nyuma ya kiemba wamkabie huku yeye akiwa huru kupandisha mashambulizi.Kiemba wa stars anacheza mbele ya Erasto nyoni na Mwinyi kazimoto huku  kazi  yake ikibaki kusaidiana na Ulimwengu kuhakikisha stars inapata ushindi.Amri kiemba wa sasa si mchezaji wa dakika 90,Mfumo wa kocha wa stars wa juzi umetufanya tuone dakika 45 bora za amri kiemba kwa msimu huu.

Kiemba wa pili ni kiemba wa simba.Kiemba wa Simba ana majukumu mengi ambayo hayazingatii hali yake.Kiemba akiingia anapewa jukumu la kuchezesha timu na kuhakikisha anawalisha washambuliaji wa simba na wakati huo huo anahakikisha anakaba vyema kwenye zone(kanda) yake kuhakikisha mipira haipiti kuelekea kwenye lango la simba.Huo ndio mfupa uliomshinda lampard akiwa kwenye timu ya taifa.

Anapewa majukumu mengi mno.Yeye mwenyewe aliwai kukiri kuwa mfumo wa 4-4-2 wanaopenda kutumia England ndio unamfanya ashindwe kutakata.Mfumo huo unafanya katikati ya uwanja kazi zote za kukaba na kupandisha mashambulizi zifanywe na watu wawili ambae ni yeye na Gerald.Wakati Chelsea anacheza na na Ramires na Matic,au Obi,City anacheza na Yaya toure na Fernandinho au Fernando kwanini kusiwe na tofauti na timu ya taifa anapocheza na Gerald tu?. Ubora na sura moja ya Babu Andrea pirlo unatokana na uwepo wa Pogba na Marchisio juventus,pia uwepo wa Marchisio,Rossi na Montollivo katika timu ya taifa ya Italia

           Kiemba akiwa na Umri wa Pirlo anahitaji msaada mkubwa ili aweze kuleta matunda kwenye timu.Simba kama inataka Sura ya kiemba ifanane na sura yake akiwa na Taifa Stars inabidi ibadili mfumo unaompunguzia majukumu uwanjani Amri Kiemba. Huwezi kuuona ubora wa kiemba kwenye mfumo wa 4-4-2 wanaopenda kuutumia Simba.Juventus leo wangekua wanatumia  4-4-2 kusingekuwepo na nafasi ya pirlo uwanjani.Kocha  Phiri hana Budi kubadilisha mfumo kama anataka kuuona ubora wa kiemba japo kwa dakika 45 tu.Kama Simba wataendelea na mfumo wao huu watarajie kuendelea kuona sura mbili za kiemba kama ilivyokuwa kwa Super Frank Lampard.


                                                                 Na allen kaijage (admin. Wapenda Soka Group)
                                                                       0655106767
                                                                 kaijagejr@gmail.com

No comments

Powered by Blogger.