WENGER NA AZIMIO LA ARUSHA
Azimio la Arusha si neno geni kwa Watanzania. Wengi wetu tumelisikia kama
hatukusoma sehemu, pia wachache kati yetu walikuwepo kipindi cha azimio la Arusha.
Azimio la Arusha ni tamko rasmi la kisiasa lililokusudiwa kuingoza nchi yetu
katika misingi ya ujamaa. Azimio hili lilipitishwa jijini Arusha chini ya
uongozi wa baba wa taifa hayati mwalimu Julius K. Nyerere mnamo mwaka 1967.
Lengo kuu la azimio la Arusha ilikua ni kupunguza au kuondoa unyonyaji na
uonevu wa mabepari. Kwa hekima za mwalimu nyerere akaona sera ya ujamaa na
kujitegemea ndo utakuwa mwarobaini kwa mabeberu na kuleta usawa na ustawi ndani
ya nchi.
Mwalimu alikua na imani kubwa na ujamaa haswa baada ya mwaka mmoja nyuma
kabla ya azimio hilo kwenda kumtembelea mjamaa Mao Ze Dong aliyekua kiongozi wa china. Nyerere
aliamua kuamishia madesa yake ya ujamaa nchini akiwa na matumaini na malengo mazuri
juu ya nchi yetu kupitia ujamaa ingawa hakufanikiwa.
Kambona na Profesa Babu waliona mbali na kumshauri aachane na misingi ya mfumo
wa ujamaa ili kunusuru viwanda lakini Nyerere aliweka pamba masikioni. Uzalishaji
ulipungua kwa kiasi kikubwa uliopelekea wananchi kuikatia tamaa sera ya ujamaa.
Labda ni kwasababu ya vita ya Kagera au anguko la bei ya bidhaa zetu, ama
tatizo la kimataifa la mafuta miaka ya mwanzoni mwa 1970. Hizo zote zinaweza kuwa
sababu ya kufeli kwa ujamaa. Mwalimu kwa busara zake ilipofika mwaka 1985
akatangaza kutogombea tena urais na kumwachia rais Mwinyi aliyeingia nchini na taratibu za soko huria
na huo ndio ukawa mwanzo wa kufa kwa ujamaa.
Soko huria (Open market )ndio
mfumo unaoendesha dunia ya sasa. Soko huria imefungua milango kwa
wafanyabiashara kuuza au kununua bidhaa kokote wapatapo soko. Wana uchumi
wanasema kuwa katika dunia ya sasa hakuna nchi ambayo ni wajamaa tu (pure
socialist) wala mabepari tu(pure capitalist) zaidi ya nchi nyingi
kuchanganganya ubepari na ujamaa (mixed economy). Huku misingi ya ubepari ikilenga ushindani wa kibiashara wakati ujamaa
ukilinda utu. Hapo utaona Dunia kwa ujumla imeruhusu ushindani huru wa
kibiashara kwa misingi isiyo ya unyonyaji. Utapata zaidi ya utakavyozalisha. Utapata
kiasi cha jasho lako huku lazima ukubali kuliwa ili ule.
Sera hii inatawala sekta zote duniani. Hata sekta ya michezo pia
inahitaji uwekezaji wa hali ya juu kufikia mafanikio. Ndio maana nchi
zilizofanikiwa sana kwenye michezo hasa soka ni zile zilizowekeza zaidi kwenye
mchezo huo. Hata vilabu vilivyofanikiwa Duniani ni vile vilivyowekeza zaidi kwa
wachezaji. Lakini bado kuna watu wabishi wanaoamini ujamaa katika soka . Wapo makomunist wanaofikiri watafanikiwa kwa sera
zao za kale. Wapo makomunist wengi lakini leo nitamzungumzia mmoja.
Huyu wanamuita Arsene Wenger. Muumini wa azimio la Arusha. Mkomunist
asiyekubali kushindwa, hataki mabadiliko wala kubadilishwa. Huendelea kuamini
kwenye kile anachokiamini hata kama hakina manufaa. Mwalimu Wenger kwa arsenal
ni kama mwalimu Nyerere kwa Tanzania, kama Nyerere alivyoleta uhuru kwa
Tanganyika ndivyo hivyo mzee Wenger alivyopigania uhuru wa arsenal na
kuirudisha kwenye chati baada ya kupotea kwa muda.Tofauti yao ni kuwa Mwalimu Nyerere maji yalipozidi
unga aliamua kujiweka kando lakini Wenger bado anakomaa na upishi huku kila
siku akipika ugali wa mabuja kwa ubahiri wa kununua unga. Wenger msimu uliopita
wa ligi kuu England alikutana na maswahiba mazito kutoka kwa Chelsea, Man City
na Liverpool lakini bado Wenger ni yule yule asiyetaka kujifunza kutoka kwenye
majanga yaliyomsibu.
Ukiangalia kikosi cha Arsenal utaona mapungufu kwenye nafasi ya
ushambuliaji bila kusahau nafasi ya kiungo mkabaji. Lakini Wenger bado
amefumbia macho swala hili na kuendeleza sera zake za ujamaa akiamini ujio wa
Welbeck akisaidiana na Sanogo watafunga magoli mengi huku akisahau mabepari Man
City wana Aguero, Dzeko na Djovetic , Chelsea wana Costa, Drogba na Remmy. Huku mabepari hayo
yakiwa na viungo wakabaji wa nguvu kama Fernandinho na Fernando kwa upande wa
city, Matic na mikel kwa upande wa Chelsea yeye mkomunisiti ana wazee
Arteta na Flamin ambao wote damu zimeshachoka. Hapo mjamaa Wenger kila
siku ataendelea kulalamika kuhusu
vitendo vya unyanyasaji na uonevu anavyofanyiwa mabepari wa City na
Chelsea ilihali ana uwezo wa kubadilisha mawazo yake ya ujamaa na kuingia moja
kwa moja kwenye Dunia ya ushindani kuwakabili mabeberu hayo. Wenger amejua
kuiga mfumo wa uchezaji wa Barcelona ila ameshindwa kugundua Barcelona pia
wameachana na sera ya ujamaa na kuingia kwenye mixed economy (kuchanganya ubepari
na ujamaa) ndio maana utaona Barcelona ya sasa inatumia bajeti ya usajili wa
wachezaji wote wa arsenal kumnunua luis suarez na kuacha utamaduni wao wa kuwaamini wakina
Tello na Bojan.
Dawa ya moto ni moto. Dawa ya bepari ni bepari na beberu ni beberu. Wenger
kama anataka kuondoa aibu ya vipigo vya magoli mengi anavyovipata kutoka kwa
city na Chelsea na kukabiliana nao jino kwa jino hana budi kuachana na misingi
ya azimio la Arusha na kuvaa roho ya ubeberu. Asikwambie mtu Arsenal haiwezi
kushindana na City na Chelsea, Arsenal ni timu tajiri kuliko City na Chelsea
tofauti yao inakuja kwenye sera ya usajili ya klabu.
Wenger ni mmoja wa makocha walioachwa huru na vilabu vyao kuhusu swala la
usajili. Yeye ndiye mwenye uamuzi juu ya mambo yote ya kiufundi. Lakini Wenger anautumia uhuru wake kuyaishi maisha ya kale
ya ujamaa. Ndio maana anaishi kwenye kile alichokiamini ingawa kimemdumaza yeye
na timu kwa ujumla. Hataki kukubali kuwa mpira sasa umebadilika ndio maana
hataki kubadilika ingawa anaona mbinu zake zinafeli. Kwa manufaa ya arenal Wenger
inabidi afanye kati ya hivi viwili, Aachane na sera zake za zamani ambazo mimi
nazifananisha na azimio la Arusha na sera ya ujamaa na aingie kwenye soko la
ushindani ili kukabiliana vilivo na mabepari Madrid, Barca, City na Chelsea
kama anataka kuirudisha Arsernal ya ushindani, ama Wenger inabidi afanye
alichokifanya Mwalimu Nyerere baada ya kuona ujamaa unaelekea kumlipua akaaamua
kukaa kando. Pia Wenger kwa busara kama za Mwalimu angekaa kando kupisha makocha
wa kisasa waendeleze mapambano yaliyomshinda.
Na
allen kaijage
0655106767
kaijagejr@gmail.com
No comments