VAN GAAL HUWEZI KUPIKA CHAPATI KWA UNGA WA MUHOGO



Tunamshukuru aliyeleta wazo la kila kata kuwa na shule ya sekondari. Shule hizi  kwa kiasi zimesaidia kufuta ujinga kwa walio wengi.Asilimia kubwa ya wanaomaliza shule za msingi wanapata nafasi za kuingia kidato cha kwanza tofauti na enzi zile za mwalimu na mzee Ruksa.

Heri nusu shari kuliko shari kamili,Ingawa shule hizi zina walakini lakini mchango wake kwenye jamii unaonekana. Tofauti ya sasa na zamani inaonekana kupitia shule hizi. Wengi hawajaelimika ila wamepunguza shari kwa kufuta ujinga. Wengi wao angalau wanajua kujieleza kwa lugha ya chakula,Pia wengi wanajua ukichanganya hydrogen na oxygen unapata maji,ukichukua sodium na chlorine unapata chumvi na ukitaka kupata chumvi na maji kwa pamoja ni lazima uchanganye acid na base. 

Hi ndio tunaita chemistry(kemia), kwa ufupi kemia ni masomo ya atomi na mkusanyo wa atomi kuwa molyekuli. Yaani hizo atomi ukizichanganya utapata kitu kizima kinachoitwa molyekuli, Hata ndugu zangu  wajenzi wanajua ili upate zege lazima uchanganye ingredients(vitu vinavyounda zege),Ili upate zege lazima uchanganye maji, kokoto,mchanga na simenti kwa viwango maalumu.

Kwenye soka  tumekuwa tukitumia maneno kama chemistry(kemia) huku wengi tukiwa hatujui chimbuko lake. Mchezaji ndiyo atomi yenyewe na timu ndio molyekuli. Kitendo cha kuwaunganisha wachezaji katika timu moja na wachezaji hao kuungana katika mfumo husika ndio tunaita chemistry(kemia). Kocha anaposhindwa kupata wachezaji husika kwenye mfumo husika hapo ndipo tunasema kashindwa kutengeneza chemistry kwenye timu.


Kocha wa Manchester United Louis van Gaal kama hakukimbia somo la chemistry basi anataka kutuonyesha staili mpya ya kupika chapati kwa unga wa muhogo.Van gaal amethubutu kutengeneza molyekuli ya 3-5-2 lakini amekosa atomi husika za kutengeneza chemistry. Watu wa mpira wanaelewa kuwa nafasi ya kiungo ndio muhimu kuliko nafasi nyingine uwanjani. Kama unavyojua tafsiri  ya Kiswahili ya neno kiungo pia ndio hivyo hivyo tafsiri hiyo hutumika katika soka.

Katika soka viungo ndio huunganisha mawasiliano kati ya mabeki  na washambuliaji.Timu nzuri ni ile yenye viungo imara. Kwenye kiungo ndiko kwenye siri ya mafanikio. Real Madrid,Bayern Munich, Man City na timu ya taifa ya Ujerumani wanaijua siri hiyo.
Louis van Gaal anajaribu kutuelewesha Darren fletcher ni mtu sahihi kwenye safu yake ya kiungo lakini Garry Monk (kocha wa Swansea) na Gus Poyet (Kocha wa Sunderland) wametuonesha uongo wa Louis van Gaal.
Na kama kocha huyo ataendelea kuwa king’ang’anizi na stori yake ya fletcher na Tom Cleverely basi ategemee watu kuendelea kupiga miayo na wakiichoka stori yake watamkimbiza kama hakukimbia mwenyewe.

Manchester United imemsajili Angel di Maria ambaye ni mchezaji bora wa Real Madrid nyuma ya Ronaldo na Bale lakini kiungo huyo si dawa ya gonjwa la united. Hapa van Gaal anajaribu kusoma vizuri stori ya dokta wa muhimbili aliyemfanyia mgonjwa  upasuaji  wa kichwa baada ya mguu. Kama ni ukimwi di Maria ni ARV. Ataongeza kitu katika timu ila hatatibu gonjwa la united. Manchester united inahitaji kiungo mkabaji mwenye roho ngumu mithili ya Nigel de Jong.Kiungo mwenye kariba ya de jong akisimama vizuri na Ander Herrera hapo ndipo utaona makali ya Wayne Rooney na Robin van Persie. Kwa  sasa washambuliaji hao wanaonekana si lolote si chochote kwasababu ya atomi walizounganishwa nazo.

Ukiacha kupwaya kwenye nafasi ya kiungo Manchester united imepwaya pia kwenye nafasi ya mabeki baada ya kuondokewa na wakongwe Nemanja vidic,Patrice Evra na Rio Ferdinand. Tegemeo pekee kwenye nafasi ya mabeki wa kati ni John Evans na Phil Jones. Hapa napo van Gaal inabidi apatazame kwa mapana na marefu kama anataka kuirudisha united ya sir Alex Ferguson.

Manchester haina tatizo la washambuliaji wala viungo wasaidizi wa washambuliaji bali wana tatizo la Kiungo mkabaji na mchezeshaji sambamba na mabeki wa kati.Haihitaji vyeti kugundua matatizo hayo.Macho yangu hayahitaji kuvaa miwani na hasilani hayanidanganyi.

Nakubali sina elimu ya ukocha kama Van Gaal ila hata yeye mwenyewe alikili kuwa timu yake haina uwiano mzuri(imekosa balance),wala siwezi ishi ndani ya kichwa cha Van Gaal kujua nini kapanga juu ya hatima ya Manchester united  ila ninachoweza kumwambia au kumkumbusha Van Gaal ni kuwa kamwe hawezi kupika chapatti kwa unga wa muhogo..

                                                                                 Na
                                                                       Alleen kaijage
                                                                            0655106767
                                                                  kaijagejr@gmail.com
                         

No comments

Powered by Blogger.