PENATI YAIOKOA YANGA ISIPATE KIPIGO MBEYA, YAAMBULIA SARE

Mabingwa watetezi wa Ligi kuu nchini Tanzania Yanga imewabidi kusubiri mpaka dakika za mwisho kusawazisha bao kwa njia ya penati ili japo kupata sare jijini Mbeya.



Yanga ilijikuta ikilazimishwa sare ya bao 2-2 dhidi ya wenyeji Tanzania Prisons katika mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara uliopigwa katika uwanja wa Sokoine.

Amiss Tambwe wa Yanga alitangulia kufunga bao la mapema kwa njia ya kichwa akiunganisha krosi ya Haruna Niyonzima lakini goli hilo halikudumu sana kwani Jeremiah Juma wa Prisons alisawazisha kwa kufunga bao kwa kichwa pia na kufanya mchezo huo kwenda mapumziko matokeo yakiwa ni bao 1-1.

Kipindi cha pili Prisons waliongeza bao la pili likifungwa kwa njia ya faulo na mchezaji Wa Zamani  wa Mtibwa Sugar Mohamed  Mkopi.

Zikiwa zimebaki dakika chache pambano hilo kukamilika mpira wa faulo uliopigwa na Haruna Niyonzima uliipatia Yanga penati baada ya mabeki wa Prisons kuunawa wakiwa katika harakati za kuokoa ndipo Simon Msuva alipouweka mpira huo nyavuni na kupelekea mchezo huo kumalizika kwa sare ya bao 2-2.

Kwa matokeo hayo Yanga wamefikisha pointi 40 wakikamata  nafasi ya kwanza wakati Simba na Azam zinaifatia  zikiwa na pointi 39.

No comments

Powered by Blogger.