LIGI KUU VPL 2015/16 KANYAGA TWENDE
Kipyenga cha Ligi Kuu ya Tanzania
Bara ndiyo hicho kimelia sasa ni wakati wa kila timu kuonesha nini ilichopanda
kuelekea msimu wa mavuno wa 2015/2016.
Kuanza kwa Ligi hiyo ni safari
nyingine ndefu ya matumaini ya kumpata Bingwa wa Tanzania siyo tu atakaeng’ara
kwa timu zingine 15 bali ndiye atakayekuwa mwakilishi wa nchi katika michuano
ya kimataifa ambapo atashiriki Klabu Bingwa Afrika 2016.
Licha ya kushirikisha timu 16 msimu
huu kuna kila dalili kuwa msimu huu utakuwa na ushindani mkubwa ukilinganisha
na uliopita kutokana na karibu kila timu ama kufanya usajili mzuri au
kuimarisha mabenchi yao ya ufundi achilia mbali kuwa na udhamini binafsi wa
uhakika.
Zoezi la usajili lililomalizika hivi
karibuni limeonesha wazi timu kusajili kwa mipango licha ya kuwa zipo timu
zilizomaliza mpango huo mapema sana na zingine zikikubali kulimaliza suala hilo
katika muda wa nyongeza kwa kukubali kulipa na faini sh. 500,000 kwa kila
mchezaji atakayesajiliwa katika muda huo.
Azam na Simba pekee waliokubali
kulimaliza zoezi hilo katika muda wa nyongeza baada ya kusajili wachezaji Pape
Abdoulaye Ndew na Boniface Maganga (Simba) na Diouf kwa upande wa Azam.
Bila shaka hiyo ilikuwa ni silaha
yao ya mwisho kuhakikisha hakuna ‘matobo’ katika usajili wao hivyo timu hizo
zitarajiwe kufanya makubwa katika msimu huu wa 2015/2016 ambapo bingwa ataweka
kibindoni kitita cha Sh. Mil 75.
Lakini Azam mabingwa wapya wa
michuano ya Kombe la Kagame, kupitia michuano hiyo imetosha kabisa kukisuka
kikosi chao hivyo kuwa moja kati ya timu zitakazoianza vizuri ligi ya msimu huu
japo hiyo haiwezi kuwa uhakika kwani cha msingi pia ni kujipanga na kucheza
vizuri karata zake.
Kwa upande wa Yanga wao waliungana na
timu zingine zilizosalia kufunga usajili wao katika muda wa awali uliotolewa,
hali inayoonesha wazi hawana wasi na vikosi vyao na ndiyo maana waliwahi
kumaliza.
Lakini kati ya hao zipo timu
zilizofunga mapema usajili wao kutokana na kukabiliwa na ukata kama vile Ndanda
na Majimaji hivyo hawakuwa na namna bali kukubaliana na hali kwa kusajili
wachezaji mapema kwa bei ya kawaida na wala hawakutaka kujipa presha zaidi
kufanya hesabu mapema na kulifunga zoezi hilo.
Uzoefu unaonesha kila wageni
wanapoingia katika Ligi Kuu wanaingia wakiwa na ushindani mkubwa, mfano mzuri
ni Mbeya city ilipopanda misimu miwili iliyopita ilikuwa katika kiwango kikubwa
kiasi cha kutishia uhai wa vigogo vya soka nchini. Hali kadhahalika Ndanda na
Stand United msimu uliopita zilifanya vema tu.
Kuna kila dalili African Sports ya
Tanga moja kati ya timu zilizowahi kuwika katika miaka ya 80 nayo ikirudi kwa
nguvu hivyo kurudisha ile hamasa ya upinzani wa jadi mkoani humo dhidi ya
Coastal Union.
Timu kongwe za ligi hiyo kama vile
Ruvu JKT, Coastal Union, Mtibwa na Kagera Sugar zinaonekana kutulia huku
zikijiandaa kuja na mbinu tofauti kabisa kuhakikisha nazo zinakuwa siyo
wasindikizaji tu bali kushika nafasi za juu na kupata tiketi ya kushiriki
michuano ya kimataifa.
Lakini pia uwepo wa timu nyingi
zenye udhamini binafsi mbali na ule wa Vodacom au Azam Televisheni utasaidia
sana kuifanya ligi hiyo kuwa na ushindani kwani sasa wachezaji wa timu husika
watakuwa na uhakika wa malipo yao hali itakayowafanya kupigana kufa na kupona.
Stand United chini ya udhamini mnono
wa Bilioni …..kutoka kampuni ya madini ya Acacia utaifanya timu hiyo
msimu huu kuja kivingine tofauti na changamoto iliyokutana nazo msimu uliopita
timu kukabiliwa na ukata kiasi cha baadhi ya wachezaji kuikimbia timu.
Mwadui ya Shinyanga nayo ikiwa chini
ya kampuni ya Madini pia ikiwa na kocha mwenye mbwembwe na maneno mengi bila
shaka licha ya ushindani vilevile kuwa chini ya kocha mwenye kuifahamu ligi
hiyo kutaibeba timu hiyo.
Mbeya City pengine inaweza kuja
kivingine hasa kutokana na kuondokewa na wachezaji wake kadhaa tegemeo
kutaifanya kuchukua muda katika kukijenga kikosi.
Lakini pia uzoefu wa wachezaji
waliobaki pamoja na kocha wao Juma mwambusi unaweza kuleta maajabu kama
ilivyofanya simu wa kwanza ilipopanda Ligi Kuu kwa kuzichachafya timu vigogo na
hatimaye kushika nafasi ya tatu.
Kilio kikubwa cha waamuzi
kimefanyiwa kazi kwa Bodi ya Ligi kuweka kanuni mpya zinazowafanya sasa kutumia
ushahidi wa picha za televisheni kuwahukumu waamuzi watakaokwenda kinyume na
kazi yao.
Ili kuipa hadhi ligi hiyo pamoja na
kuipandisha chati kuifanya kuwa moja kati ya Ligi bora barani Afrika suala la
uamuzi ni nyeti na linalopaswa kuangaliwa kwa jicho la tatu.
Lakini uzingatiwaji wa kanuni na
sheria za mashindano, bodi ya ligi na TFF kwa ujumla ndiyo silaya kubwa
itakayotoa taswira na ubora wa michuano hiyo katika kufikia kumpata bingwa
sahihi.
Mechi za ufunguzi zitatoa mwanga
fulani hata kama kama bado ligi itakuwa change. Mechi hizo ni Yanga na Coastal
Union, Ndanda na Mgambo, African Sports dhidi ya Simba, Stand na Mtibwa, Azam
dhidi ya Prisons, Mbeya City ikipambana na Kagera na Majimaji ikimenyana na
Ruvu JKT.
Kuanza kwa Ligi hiyo kutatoa picha
ya timu zipi zilitumia msimu mrefu wa usajili kwa manufaa ya klabu. Timu
iliyojiandaa vema bila shaka ndiyo itakayofanya vizuri msimu huuu kama si
kutwaa ubingwa.
Imeandaliwa na Asha Muhaji.
No comments